Moshi. Mamia ya waombolezaji, wamejitokeza kuuaga mwili wa aliyekuwa Askofu Mkuu wa kwanza wa Kanisa la Assemblies of God Tanzania (TAG) Tanzania, Emmanuel Lazaro (88), katika ibada iliyofanyika Kanisa la Kilimanjaro Revival Temple, Moshi mjini.
Askofu Lazaro ambaye alizaliwa Oktoba 4, 1937, alifariki Mei 17, 2025 katika Hospitali ya Rufaa ya kanda ya Kaskazini KCMC, siku na mwezi sawa na aliofariki mke wake, Evagrace mwaka 2017.
Ibada ya kuaga mwili wa Askofu Lazaro imefanyika leo, Mei 26, katika kanisa la TAG -KRT, mjini Moshi, na kuhudhuriwa na mamia ya waombolezaji wakiwemo viongozi wa dini, Serikali na anatarajiwa kuzikwa kesho Jumanne Mei 27, 2025, kijijini kwao Masama Modio, Wilaya ya Hai, mkoani Kilimanjaro.
Askofu Lazaro alianza huduma za kiroho mwaka 1959, Modio Masama na mpaka anastaafu huduma hiyo mwaka 2019 alikuwa amefikisha miaka 60 ya utumishi wake.

Aliyekuwa Askofu Mkuu wa kwanza wa Kanisa la Assemblies of God Tanzania (TAG) Tanzania, Emmanuel Lazaro enzi za uhai wake.
Alifanya huduma katika mazingira magumu akitembea kwa miguu, baiskeli na pikipiki mara nyingi kutoka Mkoa wa Mbeya hadi Kilimanjaro katika kutekeleza majukumu yake ya kiaskofu.
Katika salamu zake za pole na faraja, Askofu Mkuu wa TAG Tanzania, Dk Barnabas Mtokambali ambazo zimesomwa katika ibada hiyo, amesema Askofu Lazaro atakumbukwa kwa ujasiri wake katika kuhubiri injili nchini kote.
“Atakumbukwa kwa moyo wake wa kujitoa katika kupanda makanisa katika maeneo mengi nchini na huduma yake imeweka msingi mkubwa kwa TAG, na kufanya kuwa moja ya makanisa yanayokua kwa kasi katika ulimwengu” ameeleza taarifa hiyo.
Ameongeza kuwa, “tunamuenzi kama kiongozi ambaye kujitoa, unyenyekevu na msimamo wake thabiti usioyumba ni mfano wa kuigwa na alidumisha mshikamano wa kanisa akisisitiza juu ya amani na ushirikiano.”

Baadhi ya waombolezaji wakiwa kwenye ibada ya kuaga mwili wa aliyekuwa Askofu Mkuu wa kwanza wa kanisa la Tanzania Assemblies of God (TAG), Askofu Immanuel Lazaro, ibada ambayo imefanyika katika kanisa la Kilimanjaro Revival Temple mjini Moshi.
Akihubiri katika ibada hiyo, Makamu wa Askofu Mkuu wa TAG, Dk Magnus Mhiche amesema kifo sio mwisho ni mwanzo wa maisha mengine hivyo akaitaka familia kuendelea kuyaenzi yale ambayo Askofu Lazaro amewaachia.
“Mzee wetu hajaondoka kwa bahati mbaya imeratibiwa na yeye Mungu mwenyewe, amepanga siku za kuishi na kumpa mipaka na hakuna anayeweza kuivuka,”amesema Dk Mhiche
Akitoa salamu za rambirambi katika ibada hiyo, mfanyabiashara maarufu mjini Moshi, Ibrahim Shayo amesema Askofu Lazaro alikuwa ni kiongozi ambaye alikuwa ni mwanga wa matumaini kwa wengi kwa kuwa alikuwa habagui dini wala kabila katika utumishi wake.
“Askofu Lazaro alikuwa ni zaidi ya kiongozi wa kiroho, alikuwa ni mtu mwenye hekima, ushirikiano wa dhati katika maendeleo ya jamii, katika maisha yake alisimama kama taa iliyoko juu ya mlima ikitoa mwanga na matumaini kwa wengi,”amesema Shayo
Amesema Askofu Lazaro hakujali dini katika maendeleo zaidi alikuwa anahitaji mahusiano ya kijamii bila kujali ni kabila, dhehebu gani na ameacha alama katika kanisa hilo.
“Tuendelee kumuenzi na kuendeleleza yale aliyoyaamini, aliamini mshikamano kwa maendeleo ya kweli katika jamii, ndugu zangu baba Askofu Lazaro ameondoka ametuachia kazi kubwa ya kutuunganisha na kuendeleza dini hii ndani na nje ya mkoa huu,”amasema Shayo.
Askofu Lazaro ameacha watoto watano, wajukuu 17 na vitukuu wanne.