Mahakama yamng’ang’ania aliyemnajisi mwanaye, jela miaka 30

Arusha. Juhudi za baba aliyehukumiwa kifungo cha miaka 30 jela kwa kumbaka binti yake, kujinasua katika adhabu hiyo, zimegonga mwamba baada ya Mahakama ya Rufani kutupilia mbali rufaa yake.

Baba huyo mkazi wa Kijiji cha Buhingu, Wilayani Chato mkoani  Geita, alihukumiwa adhabu hiyo na Mahakama ya wilaya hiyo.

Hii ni rufaa yake ya pili ambapo rufaa ya kwanza ilisikilizwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Geita, baada ya Hakimu aliyekuwa akiisikiliza kuongezewa mamlaka, ambapo mahakama ilitupilia mbali rufaa hiyo.

Baba huyo alitiwa hatiani kwa kosa la kumbaka binti yake aliyekuwa na umri wa miaka 16, kosa alilodaiwa kutenda katika tarehe zisizojulikana kati ya mwaka 2020 hadi Januari 2021.

Alikata rufaa Mahakama hiyo ya juu nchini, akipinga hukumu ya mahakama ya chini ambapo pamoja na masuala mengine alidai upande wa mashitaka, haukuweza kuthibitisha shitaka hilo dhidi yake.

Jopo la majaji watatu wa Mahakama ya Rufaa walioketi Mwanza ambao ni Lugano Mwandambo,Abraham  Mwampashi na Dk Ubena  Agatho,walitoa hukumu hiyo Mei 26, 2025 na nakala ya hukumu hiyo kuwekwa kwenye mtandao wa Mahakama.

Mrufani huyo alikuwa na sababu saba za rufaa ikiwemo kesi hiyo ilitengenezwa dhidi yake na kikao cha familia alichodaiwa kuwa alikiri kutenda kosa hilo kiliendeshwa bila utaratibu.

Katika rufaa hiyo mrufani huyo hakuwa na uwakilishi wa wakili huku Jamhuri ukiwakilishwa na mawakili wawili wa Serikali Waandamizi, ambao walipinga rufaa hiyo.

Jaji amesema baada ya kuchunguza sababu za rufaa wanakubaliana na wakili wa Jamhuri kuwa isipokuwa sababu ya pili (haikuwa mpya) ila  sababu ya kwanza, tatu, nne na tano ambazo  zinaleta malalamiko mapya ambayo hayakuonekana kwenye rufaa ya kwanza.

Amesema kwa mujibu wa kifungu cha 7 (6) (a) cha Sheria ya Haki za Binadamu (AJA) na kwa kuzingatia baadhi ya maamuzi ya Mahakama hiyo, Mahakama haina mamlaka ya kusikiliza masuala mapya, ambayo hayakutolewa na kuamuliwa na mahakama ya mwanzo au Mahakama Kuu isipokuwa kama yapo kwenye misingi ya sheria.

Kutokana na sababu hizo amesema sababu ya kwanza, tatu, nne na tano haziwezi kuwasilishwa mahakamani hapo hivyo wanasikiliza sababu ya pili, sita na saba.

Kuhusu sababu ya sita ambayo mrufani huyo anadai mahakama mbili za chini hazikuzingatia utetezi wake ambapo majaji hao wamesema waliingia kwenye viatu vya mahakama hizo mbili na kufanya kilichopaswa kufanywa.

Jaji Mwandambo amesema rekodi ya rufaa inaonyesha wazi kwamba, si mahakama ya mwanzo wala ya kwanza ya rufaa iliyozingatia utetezi wa mrufani.

“Katika suala hilo, tuna wajibu wa kurejea utetezi na kuuzingatia.

Kwa urahisi, tunapendekeza kufanya hivyo wakati wa kubainisha sababu ya saba ya rufaa kuhusu iwapo kesi dhidi ya mrufani ilithibitishwa kwa kiwango kinachohitajika,”

Jaji amesema chini ya kifungu cha 158 (1) (a) cha Kanuni ya Adhabu alichoshtakiwa nacho mrufani huyo, baada ya wao kupitia upya ushahidi ulio kwenye kumbukumbu wanashikilia kuwa mwathirika wa tukio hilo ni binti wa kibiolojia wa mrufani na alikuwa na miaka 16 wakati kosa hilo linatendeka.

Amesema suala hilo liliungwa mkono na fomu ya polisi namba tatu (PF3), na shahidi wa pili na nne ambao ni ndugu wa mrufani walioeleza kuwa alikiri mbele yao kwenye mkutano wa ukoo kwamba aliwahi kumbaka binti yake.

“Sheria imetatuliwa kwamba, ungamo linalofanywa mbele ya mashahidi wa kutegemewa, wawe ni raia au la, unaweza kuwa wa kutosha. Kwa sababu zilizotolewa hapo juu, tunaona kwamba kesi dhidi ya mrufani ilithibitishwa pasipo shaka kama inavyotakiwa na sheria,”

Majaji hao walihitimisha kwa sababu mrufani alitenda kosa hilo akijua mwathirika wa tukio hilo ni binti yake, wanaona rufaa yake haina mashiko na kuitupilia mbali.

Awali katika kesi ya msingi upande wa mashitaka ulikuwa na mashahidi watano na kielelezo kimoja ambacho ni PF3.

Shahidi wa kwanza (mwathirika wa tukio hilo), aliieleza Mahakama kuwa mrufani ambaye ni baba yake mzazi mara nyingi alikuwa akimwingilia na kuwa alitoa taarifa hizo kwa watu wengi wakiwemo wajomba zake na Ofisa Mtendaji wa Kijiji.

Aliieleza Mahakama kuwa siku moja kwenye mkutano wa ukoo ulioitishwa, kujadili vitendo alivyokuwa akifanyiwa na mrufani huyo ambapo baba yake alipewa adhabu ya kuchapwa viboko 10, ila hakuacha vitendo hivyo aliendelea navyo hadi alipokamatwa na kupelekwa polisi.

Baada ya kesi hiyo kuripotiwa polisi, mwathirika alipelekwa katika Hospitali ya Wilaya ya Chato Februari 12, 2021 ambapo alifanyiwa uchunguzi na Ofisa kliniki msaidizi ,Renatus Paschal ( shahidi wa tano) ambaye alithibitisha kuwa binti huyo alifanyiwa kitendo hicho.

Shahidi wa pili na nne ambao ni ndugu wa mrufani waliunga mkono ushahidi wa mwathitika wa tukio hilo na kuwa alishawahi kuripoti kwao kuwa baba yake alikuwa akimwingilia.

Mashahidi hao waliiambia Mahakama kuwa mrufani alikiri mbele ya kikao cha familia ambapo iliazimia mrufani huyo achapwe viboko 10 kama adhabu na shahidi wa nne ndiye aliyetoa adhabu hiyo.

Shahidi wa tatu ambaye alikuwa Mwenyekiti wa Kijiji hicho, Rugora Magoti, alieleza kuwa mwanzoni kulikuwa na uvumi kwamba mrufani alikuwa akimfanyia binti yake kitendo hicho.

Alieleza kuwa kwa mara ya kwanza Februari 7,2021 suala hilo liliripotiwa kwake ambapo yeye aliripoti polisi Februari 12, 2021 na mrufani kukamatwa.

Katika utetezi wake mrufani huyo alieleza kuwa shitaka hilo siyo la kweli na liliibuliwa kwenye kikao cha familia baada ya kuhudhuria mazishi ya kaka yake na kusisitiza hakuwahi kufanya mapenzi na biti yake.

Alieleza kuwa kesi hiyo  ilitengenezwa na binti yake na watu wengine huku akikanusha kuwa hajawahi kuadhibiwa na wana ukoo.

Mahakama hiyo ya chini baada ya kusikiliza pande zote mbili ilimkuta mrufani huyo na hatia na kufuatia ushahidi wa binti yake, shahidi wa pili na nne na kumhukumu adhabu hiyo.

Related Posts