Takukuru yazuia malipo ya makaburi hewa 123 Musoma

Musoma. Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) mkoani Mara imefanikiwa kudhibiti malipo hewa ya zaidi ya Sh70.2 milioni zikiwemo Sh49.2 milioni zilizotakiwa kulipa fidia ya makaburi hewa katika Kata ya Nyatwali wilayani Bunda.

Makaburi hayo ni sehemu ya malipo ya fidia ya zaidi ya Sh59 bilioni zilizotolewa na Serikali kwa wakazi wa Nyatwali ambao wanatakiwa kupisha eneo hilo ambalo ni mapitio ya wanyama kutoka katika Hifadhi ya Taifa Serengeti, kuelekea Ziwa Victoria kwa ajili ya malisho na maji.

Akitoa taarifa ya utendaji kazi wa miezi mitatu iliyopita mjini Musoma leo Jumatatu Mei 27,2025 Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Mara, Mohamed Shariff amesema kiasi hicho cha Sh49.2 milioni kilitarajiwa kulipa makaburi hewa 123.

“Baada ya kufanya uchunguzi tulibaini uwepo wa makaburi hewa yaani yasiyokuwa na miili ambapo kila kaburi lilitakiwa kulipwa Sh400,000 tukazuia malipo hayo,  kwani hayakuwa na sifa ya kulipwa fidia,” amesema

Amesema makaburi hayo hewa yaliingizwa kwenye mfumo wa malipo wakati wa mchakato wa ufanyaji wa tathmini huku akisema kuwa walibaini kuwa wahusika walionyesha maeneo  matupu au matuta kuwa ni makaburi, jambo ambalo halikuwa na ukweli kwani uchunguzi ulibaini kuwa hapakuwa na mabaki ya miili ya binadamu katika makaburi hayo.

Katika hatua nyingine Shariff amesema taasisi hiyo pia imeokoa zaidi ya Sh21 milioni ambazo  zilikuwa zimetengwa kwa ajili ya ununuzi wa vifaa vya ujenzi wa Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Bunda kwa awamu ya pili, huku vifaa vilivyopangwa kununuliwa vikiwa tayari vimehanunuliwa katika ujenzi wa awamu ya kwanza.

“Tulifanya uchunguzi na kubaini vifaa vilivyopangwa  kununuliwa vilikuwa vimeshanunuliwa na vingine vilikuwa tayari vimefungwa kwenye majengo husika wakati wa utekelezaji wa mradi kwa awamu ya kwanza,” amesema.

Amesema baada ya uchunguzi walishauri mamlaka husika zisilipe fedha hizo hivyo kuweza kuokoa kiasi hicho cha fedha.

Katika hatua nyingine Shariff amesema ofisi yake imepokea taarifa mbalimbali zikihusisha baadhi ya wanasiasa kujihusisha  na vitendo vya rushwa kuelekea uchaguzi mkuu, ambapo hatua kadhaa zimechukuliwa ikiwa ni pamoja kuanza kufanya uchunguzi juu ya tuhuma hizo huku baadhi ya wahusika wakipewa onyo.

Hata hivyo hakuwa tayari kuzungumzia kwa undani juu ya tuhuma hizo ikiwepo takwimu za watuhumiwa na uchunguzi upo katika hatua gani.

Kuhusu utekelezaji wa miradi, mkuu huyo wa Takukuru amesema katika kipindi cha miezi mitatu ofisi yake imefuatilia miradi 28 yenye thamani ya zaidi ya Sh9.2 bilioni katika sekta za afya, elimu barabara na maji.

“Kati ya miradi hiyo tulibaini kasoro na dosari kwenye miradi 12 yenye thamani ya Sh3.9 bilioni na kutoa ushauri ili marekebisho yafanyike kabla miradi hiyo haijakamilika,” amefafanua.

Baadhi ya wakazi wa Musoma mkoani Mara wameshauri hatua kali zichukuliwe dhidi ya wale wote wanaobainika kuwa na lengo la kuisababishia hasara Serikali.

“Hapo unasema watu walitaka kupiga Sh70 milioni lakini hakuna hatua zimechukuliwa baada ya fedha hizo kuokolewa, ilitakiwa zikishaokolewa nao wachukuliwe hatua ili wasije wakarudia tena,” amesema Fazel Janja.

Joyce Martin amesema kitendo cha kutokuwachukulia  hatua wahusika kinatoa mwanya wa kuendelea na majaribio ya aina hiyo.

“Watakuwa wanaendelea kufanya hivyohivyo wakifanikiwa inakuwa furaha kwao wakishtukiwa kabla fedha zinarudishwa, mimi nadhani kudhibiti kuende sambamba na kuwachukulia hatua,” amesema.

Related Posts