Uhaba wa watalaamu, miundombinu hafifu kikwazo sekta ya afya

Unguja. Licha ya mafanikio yaliyopatikana katika sekta ya afya kwa mwaka wa fedha 2025/26, Waziri wa Afya wa Zanzibar, Nassor Ahmed Mazrui amesema wizara bado inakabiliwa na changamoto 12 ikiwamo ya msongamano wa wagonjwa katika hospitali za wilaya na mikoa, hasa katika wodi za wazazi.

Pia, Mazrui amesema kutofikiwa kwa viwango vya ubora vya kitaifa na kimataifa katika utoaji wa huduma kwenye vituo vya afya kumeendelea kuwa changamoto nyingine, jambo linalokwamisha utekelezaji wa mfumo wa rufaa kwa ufanisi.

Waziri Mazrui amesema hayo leo Jumanne Mei 27, 2025, wakati akisoma hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Afya kwa mwaka wa fedha 2025/26 huku akianisha vipaumbele vya wizara katika kukabiliana na changamoto hizo, alipoliomba Baraza la Wawakilishi kuidhinisha Sh368.150 bilioni.

Pia, ametaja uhaba wa wataalamu wenye sifa katika utoaji wa huduma za kibingwa na bobezi kama vile madaktari bingwa, wataalamu wa ganzi na usingizi, wataalamu wa ICU, wahandisi vifaa tiba, wauguzi wenye shahada ya kwanza, wakaguzi wa kemikali kuwa ni kikwazo kingine.

“Miundombinu hafifu ya uendeshaji wa mfumo wa ukusanyaji wa taarifa za wagonjwa (EMR), katika vituo vya afya vya msingi ikiwamo ukosefu wa huduma za intaneti na vifaa vya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama),” amesema.

Akiendelea kuwasilisha bajeti hiyo, Waziri Mazrui amesema upatikanaji wa fedha usioridhisha kwa ajili ya uendeshaji wa wizara na utekelezaji wa miradi ya maendeleo pia ni changamoto inayoikabili wizara hiyo.

Pia, amesema changamoto nyingine ni kuongezeka kwa maradhi yasiyoambukiza yakiwamo ya shinikizo la damu na kisukari.

“Katika kuimarisha huduma za kinga na elimu ya afya dhidi ya magonjwa ya kuambukiza na yasiyoambukiza Sh103.983 bilioni zimetengwa sawa na asilimia 28 ya bajeti ya wizara mwaka 2025/26 kukabiliana na changamoto hiyo,” amesema.

Kikwazo kingine katika utoaji wa huduma kwa mujibu wa Mazrui ni uchakavu wa miundombinu ya vituo vya afya ikiwamo majengo, mashine na vifaa tiba, kuongezeka kwa matumizi ya dawa za asili kutokana na uuzaji holela wa dawa hizo katika maeneo mbalimbali.

“Lishe duni ya mama na mtoto inayosababisha maradhi na vifo vinavyotokana na uzazi kwa mama na watoto na kutopatikana kwa taarifa za afya kwa ukamilifu na kwa wakati kutoka katika vituo vya afya vya binafsi,” amesema.

Kutokana na changamoto zilizojitokeza katika utekelezaji wa majukumu ya wizara, amesema mwaka wa fedha 2025/26, wizara imejipanga kuongeza kasi ya kukamilisha ujenzi wa vituo vya afya na zahanati katika maeneo yanayochangia idadi kubwa ya wagonjwa.

Amesema katika mwaka ujao wa fedha, wizara itaimarisha miundombinu na huduma katika baadhi ya vituo vya afya kila wilaya ili viweze kutoa huduma saa 24 kwa siku, ikijumuisha siku za mapumziko na mwisho wa wiki.

Waziri amesema wizara imejipanga kuongeza idadi ya watumishi wa sekta ya afya kwa kuajiri wataalamu wenye ujuzi kupitia Serikali pamoja na kampuni binafsi zinazoendesha hospitali za wilaya na mikoa.

Amesema wizara itaendelea kuboresha miundombinu na kufunga vifaa vya  Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) kwa ajili ya kuimarisha huduma za mtandao na kuongeza kasi ya intaneti katika vituo vya afya.

Pia, amesema wizara imejipanga kuongeza wafanyakazi wa afya kwa kuajiri wataalamu wenye ujuzi kupitia Serikali na kampuni binafsi zinazoendesha hospitali za wilaya na mkoa na kuweka miundombinu na kufunga vifaa vya mtandao ili kuongeza kasi ya intaneti.

Katika kulifanikisha hilo, amesema tayari wizara imeingia mkataba na Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) kupeleka mkonga kwenye vituo vya afya 142.

Amesema Shirika la Kimataifa la Kuhudumia watoto (Unicef) limeingia mkataba na wizara kwa ajili ya kuimarisha mifumo ya Tehama ikiwamo mfumo wa ukusanyaji wa taarifa za wagonjwa (ZanEMR).

Mpango mwingine wa wizara ni kuwatumia wahudumu wa afya ngazi ya jamii kwa ajili ya kusajili, kuchunguza na kuhamasisha wajawazito kuhudhuria kliniki mapema na kujifungulia katika vituo vya afya.

Vilevile, wizara itashirikiana na wamiliki wa vituo vya afya na hospitali binafsi ili kuhakikisha taarifa za wagonjwa zinaingizwa kwenye mfumo rasmi wa taarifa kwa kutumia fomu maalumu zilizotolewa na wizara.

Akiwasilisha maoni ya kamati ya ustawi wa jamii, mwenyekiti wa kamati hiyo, Sabiha Filfil Thani amesema licha ya kazi kubwa iliyofanywa na wizara hiyo, kamati imebaini kulikua na upatikanaji mdogo wa fedha za matumizi.

Amesema kwa mwaka wa fedha 2024/25 zilikadiriwa kutumika Sh282.756 bilioni lakini hadi kufika Machi 2025, Sh136.047 bilioni sawa na asilimia 48 zilitumika, jambo ambalo limesababisha kuzorota kwa baadhi ya shughuli za wizara kutekelezwa kwa wakati uliopangwa.

“Pia, Kamati inaishauri Wizara kuongeza madaktari na wataalamu wengine kama wauguzi ili waweze kusaidia kukabiliana na changamoto hizo hususani katika wodi za mama na mtoto,” amesema.

Related Posts