Dar es Salaam. Huduma za Al Barakah zinazotolewa na benki ya CRDB zimeiweka tena Tanzania katika ramani ya huduma bora zinazofuata misingi ya dini ya Kiislam duniani baada ya kutangazwa mshindi wa Tuzo za Euromoney kwa mwaka 2025.
Tuzo hii ya heshima iliyotolewa jijini Dubai hivi karibuni imekuja wakati Benki ya CRDB ikisherehekea miaka 30 tangu kuanzishwa kwake, ikiwa ni miongo mitatu ya uongozi, ubunifu, na ujumuishi wa kifedha kwa Watanzania na nje ya mipaka ya nchi.
Tuzo hii imetolewa kutambua utendaji makini wa Benki ya CRDB na umadhubuti wake katika kutoa huduma za fedha zinazozingatia misingi ya Sharia ambazo zimewawezesha watu binafsi na jamii kupata huduma zinazoendana na imani yao.
Tuzo hiyo imetambua kasi ya CRDB Al Barakah katika kuwafikia wateja ambapo kumeshuhudiwa ongezeko la asilimia 162, ongezeko la amana kwa asilimia 72, na ukuaji wa mapato kwa asilimia 172 kufikia Sh22 bilioni kati ya Desemba 2023 hadi Desemba 2024.
Mafanikio haya yanaonesha kuongezeka kwa imani ya Watanzania katika huduma za fedha za Kiislamu na uongozi wa Benki ya CRDB katika sekta hiyo.
“Tuzo hii ni alama ya kile kinachowezekana pale ambapo misingi ya imani, ubunifu wa kifedha na maendeleo jumuishi vinapoenda sambamba. CRDB Al Barakah imeendelea kuthibitisha kuwa huduma za benki zinazofuata misingi ya Kiislamu si suala la kufuata tu masharti, bali ni suala la athari chanya katika jamii,” amesema
Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri wa Sharia ya CRDB Al Barakah, Abdul Van Mohammed amesema; “Ni kuhusu kuwezesha ustawi na fursa kwa wote. Nawashukuru sana wateja wetu na washirika wetu kwa imani yao na usaidizi. Mafanikio haya ni yao kama yalivyo kwa Benki yetu,” Benki ya CRDB kupitia kitengo chake cha Al Barakah imeanzisha bidhaa bunifu ambazo zimebadilisha taswira ya huduma za benki zinazofuata misingi ya kiislam nchini.
Mifumo hiyo inajumuisha mrabaha kwa ajili ya ununuzi wa mali, Istisna’a kwa ufadhili wa miradi, Ijarah kwa mikopo ya elimu na ibada, pamoja na mkataba wa Qardh unaotekelezwa kwa kushirikiana na Serikali ili kutoa mikopo isiyo na riba kwa wakulima wadogo na wavuvi.
Jitihada za Benki katika kukuza ustawi kwa jamii zimesaidia pia kuanzishwa kwa huduma za bima za Kiislamu zijulikanazo kama Takaful tangu mwaka 2024 ambazo zinatolewa kwa ushirikiano na ZIC Takaful ambapo zaidi ya wateja 300 walinufaika katika mwaka wake wa kwanza pamoja na Akaunti ya Sadaka ambayo ni maalumu kwa ajili ya kutoa michango ya kidini, ni vielelezo vya dhamira ya Benki ya CRDB kuchochea maendeleo ya jamii kwa kuzingatia misingi ya imani.
Akizungumzia tuzo hiyo leo Mei 27, 2025 Mkuu wa Kitengo cha Huduma za Benki za Kiislamu ya CRDB, Rashid Rashid amesema ni matokeo ya imani ambayo wateja wameipatia benki hiyo kwa kutumia huduma zinazofuata misingi ya sharia.
“Tunaposherehekea miaka 30 tangu kuanzishwa kwa Benki yetu ya CRDB, tuzo hii si mwisho wa safari, bali ni alama ya kuendelea kupanua wigo wa huduma, kuleta ubunifu wa kuwajibika, na kujenga mfumo jumuishi wa kifedha,” amesema.
Benki ya CRDB inaendelea kubadilisha maisha kupitia huduma za kipekee kama Mikopo ya Hija na Umra iliyoanzishwa mwaka 2023, ambayo imewezesha maelfu ya Watanzania kutekeleza ibada zao kwa urahisi na heshima.
Katika kipindi cha miaka minne tangu kuanzishwa kwake, Benki ya CRDB imekuwa taasisi ya kwanza ya fedha ya Kitanzania kushinda tuzo za kimataifa katika tasnia ya huduma za benki zinazofuata misingi ya dini ya Kiislamu, zikiwemo tuzo ya huduma bora kwa mwaka 2023 na 2024 kutoka Tuzo za Dunia za Huduma za Benki zinazofauata Misingi ya Kiislamu (GIFA).
Benki ya CRDB inaposherehekea miaka 30 ya kuiwezesha jamii, tuzo hii kutoka Euromoney inaonyesha dhamira yake katika kuendelea kutoa huduma jumuishi na endelevu zinazozingatia imani na maadili ya watu inayowahudumia.