Tabora. Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Mkoa wa Tabora imekamata jumla ya mabelo ya magunia ya kufungia Tumbaku maarufu kama Majafafa yenye thamani ya Sh1.4 bilioni.
Akitoa taarifa ya utendaji kazi wa taasisi hiyo kwa kipindi cha Januari hadi Machi mwaka huu Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Tabora, Azza Mtaita amesema magunia hayo yamekamatwa kwa wafanyabiashara waliokuwa wakiyauza kinyume na utaratibu kufuatia opeshereni maalumu inayoendeshwa na vyombo vya dola mkoani ambapo wameyakamata.
“Tunaposema tunafanya operesheni hatutanii na tutawakamata kweli kweli hakuna atakaefanikiwa kutafuna jasho la mkulima wa Tabora,” amesema.
Amesema watuhumiwa waliokamatwa katika Sakata hilo wamekiri makosa hayo hivyo kufanya makubaliano ya kulipa faini ya Sh2 milioni na kurejesha magunia hayo yenye thamani ya Sh1.4 bilioni kwa wakulima kwa ajili ya kuendelea kuhifadhia Tumbaku.
Mkuu huyo wa Takukuru Mkoa wa Tabora, amesema watuhumiwa hao wamechukua magunia hayo kutoka katika vyama vya msingi vya Mulokhu, Mkombozi, Bukemba, Ikobelo na Kasisi na hivyo kuyarejesha katika vyama hivyo kwa mujibu wa utaratibu.
“Wakulima hawa wanakua shambani kipindi cha mwaka mzima hakuna mapumziko kabisa alafu watu wachache kwa faida zao binafsi wanasumbua wakulima hawa hatuwezi kukubali tuko kazini muda wote,” amesisitiza.
Amewahimiza wafanyabiashara wa Tumbaku mkoani Tabora wanaokwenda kinyume na taratibu za mauzo ya zao hilo kuacha tabia hiyo kwani sheria kali zitaendelea kuchukuliwa dhidi yao kwani hatua hiyo ni kinyume cha sheria na taratibu za biashara hiyo.
Katika hatua nyingine sekta sita mkoani Tabora zimelalamikiwa zaidi na wananchi juu ya utoaji wa huduma zake ikiwemo sekta ya afya, miundombinu ya barabara, ulinzi na usalama, kilimo, nishati na elimu ambapo jumla ya kero 215 ziliibuliwa na kwamba kero 194 sawa na asilimia 79 zimetatuliwa.
Hata hivyo katika uchunguzi na mashtaka yalipokelewa malalamiko 116 ambapo malalamiko 92 yalihusu rushwa, taarifa 4 zilihamishwa na watoa taarifa 20 wamepewa ushauri wa namna ya kutatua malalamiko yao, taarifa 12 uchunguzi wake ulifungwa kutokana na kujkosa ushahidi.
Kwa upande wa mashtaka kesi mpya 4 zilifunguliwa, kesi 3 ziliamriwa ambapo jamhuri imeshinda kesi 1imeshindwa kesi 1 na kesi 1 imeondolewa huku kukiwa na kesi 15 ambazo zinaendelea kusikilizwa katika mahakama mbali mbali za wilaya za Mkoa wa Tabora.
Mbali na hayo taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa Takukuru Mkoa wa Tabora imewataka wananchi kutoruhusu mianya ya rushwa hasa katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu, huku wakisisitizwa kutoa taarifa za viashiria vya rushwa au rushwa katika maeneo yao.