Dar es Salaam. Mkurugenzi wa Mkondo wa Juu wa Petroli (Pura), Charles Sangweni amesema wameongeza kasi ya utafiti wa kina katika maeneo ambayo wanaamini kuwapo kwa viashiria vya mafuta nchini, ikiwemo Eyasi-Wembele na Ziwa Tanganyika.
Wakati hilo likifanyika, pia, Pura imeita wawekezaji wenye nia ya kuwekeza katika sekta ya gesi na mafuta kuchangamkia fursa iliyopo katika vitalu 26 inayovinadi sasa. Wito huo umetolewa katika mkutano wa kimataifa uliowakutanisha Jumuiya ya Wahandisi wa Petroli (SPE).
Wahandisi hao waliotoka maeneo mbalimbali duniani, wanatarajia kufanya mkutano wa siku mbili unaolenga kuangalia suala la teknolojia katika nchi za Afrika. Mkutano huo unafanyika Tanzania kwa mara ya tano sasa baada ya kufanyika katika nchi za Misri, Afrika Kusini, Nigeria na Ghana.
Sangweni amesema wanatangaza fursa za uwekezaji katika ugunduzi wa gesi na mafuta ili nchi iweze kufaidika na rasilimali ilizonazo kabla ya dunia haijahamia katika nishati jadidifu.
“Kupitia TPDC kuna maeneo ambayo tunaamini kuna viashiria vya mafuta kama Eyas Wembele na Lake Tanganyika ambayo tunaamini baadaye tunaweza kupata mafuta.
“Tafiti zinaendelea na tunaongeza kasi kwa sababu dunia inahama kutoka katika matumizi ya mafuta na mazao yake kwenda kwenye nishati jadidifu, lazima twende kwa kasi ili kuitumia rasilimali tuliyonayo,” amesema Sangweni.
Amesema wanatumia jukwaa kama hilo kunadi fursa za uwekezaji zilizopo kwani wanaamini kati ya washiriki wapo watu watakaokuwa na uwezo wa kuwekeza.
Kwa mara ya mwisho, Tanzania ilinadi vitalu vyake 26 mwaka 2013 lakini havikupata mwekezaji kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo mabadiliko ya bei za mafuta duniani, lakini sasa ipo katika maandalizi ya duru ya tano ya kuvinadi upya.
“Tunafanya hivi ili gesi iweze kutumika katika maeneo mengi zaidi, na kuokoa fedha za kigeni ambazo zingetumika katika kuagiza mafuta nje ya nchi,” amesema.
Tanzania inakadiriwa kuwa na mita za ujazo trilioni 230 za gesi asilia, ingawa zilizothibitishwa mpaka sasa ni futi trilioni 57.5, hivyo kuiweka kwenye ramani ya dunia ikishika nafasi ya 82.
Gesi hiyo tayari imeanza kuchimbwa katika visiwa vya Songosongo, Wilaya ya Kilwa mkoani Pwani na eneo la Msimbati mkoani Mtwara, ikitumika kuzalisha umeme na kuendesha mitambo ya baadhi ya viwanda nchini.
Akizungumzia mkutano huo, Sangweni amesema unasaidia kuandaa vijana ili waweze kuendana na mabadiliko ya teknolojia yanayotokea duniani kupitia ubadilishanaji wa uzoefu kati ya nchi.
“Kuna wenzetu ambao wameendelea au wako nyuma hivyo tunabadilishana uzoefu na kuelezana mwelekeo wa tasnia hii duniani,” amesema.
Mwenyekiti wa SPE Tanzania, Alex Stephano amesema katika mkutano wa sasa wanatazamia zaidi suala la teknolojia upande wa Afrika huku akiamini kuwa kama wafanyakazi watabadilishana uzoefu.
“Tumepiga hatua katika masuala ya petroli kwani kuna maeneo ambayo yanazalisha gesi na kuna shughuli za utafiti na uendelezaji wa gesi zinazoendelea nchini, imekuwa ni fursa ambayo imewavutia wageni na kuona Tanzania ni sehemu ambayo wanaweza kuwekeza,” amesema.
Mwenyekiti wa SPE Afrika, Dk Riverson Oppong amesema wamepata nafasi ya kusikia fursa za uwekezaji zilizopo katika vitalu zaidi ya 20 ambavyo vinaweza kufanyiwa uwekezaji na watu waliopo ndani ya sekta.