Wananchi wasimulia kilimo mseto kilivyowanusuru na utegemezi

Songwe. Wanawake wa Kijiji cha Nyimbili  Kata ya Nyimbili,  Wilaya ya Mbozi Mkoa wa Songwe wamesema uwepo wa ujira kupitia mashamba ya kilimo mseto na viwanda vya kuongeza thamani zao la kahawa vimekuwa kimbilio na kuwaondoa kwenye  changamoto ya mfumo dume na utegemezi.

Hatua hiyo imetajwa ni baada ya Diwani wa Kata hiyo, Tinson Nzunda kufanya uwekezaji kupitia kiwanda cha kuongeza thamani zao la kahawa na mashamba ya kilimo mseto kwenye eneo lenye ukubwa wa hekari zaidi ya 50 kijijini hapo.

Mbali na uwekezaji huo, Pia ametoa ajira kwa wananchi 300 kati ya hao wanawake 200, kwa lengo la kuondoa tatizo la ajira, mfumo dume na kupunguza vitendo vya uharifu.

Wakizungumza na Mwananchi Digital  Mei 26, 2025, wamesema miaka  kadhaa iliyopita kabla ya uwekezaji huo  kulikithiri vitendo cha ukatili ,mfumo dume kutokana na dhana ya wanawake kukaa ndani au kutumikishwa kwenye kilimo.

 “Wanawake tulikuwa hatuna sauti  hatutakiwa kufanya shughuli yoyote ya kiuchumi kujiingiza kipato, muda mwingi tulikuwa  tukikaa ndani au tumikishiwa kwenye kilimo na mifugo,”amesema Edimatha Msongole.

Amesema uwepo wa uwekezaji wa kilimo mseto na viwanda vya kuchakata zao la kahawa imekuwa kimbilio kubwa kwao kwani wana uwezo wa kumudu  kutunza familia na kutoa fursa ya kupata elimu.

“Kwa sasa ukimkuta mwanamke amekaa nyumbani amependa yeye kwani ujira wa mashambani na viwanda vya kuchakata zao la kahawa uko nje nje ni juhudi yako namna ya kupambana,” amesema.

Edimatha ambaye ni mama wa watoto watatu amesema kupitia ujira huo, kwa wiki analipwa Sh58,000 huku kwa mwezi ni zaidi ya Sh230,000 jambo ambalo linawapa msukumo wa kujituma.

“Kwanza tuna kila sababu ya kuishukuru serikali kwa kuruhusu uwepo wa uwekezaji huu ambao umekuwa suruhisho la kutuondoa katika dhana ya mfumo dume na kuondokana na utegemezi kwa waume zao,” amesema.

Naye Maria Mdolo amesema hiyo ni fursa pekee kwa wanawake kuchangamkia ili kuweza kumudu kuendesha maisha ya kila siku na kuachana na utegemezi katika ndoa ambao uchangia vitendo vya unyanyasaji na ukatili wa kijinsia.

“Miaka ya sasa wanawake tumeshtuma maana tulikuwa usingizini kwa kuruhusu kutumikishwa kwenye kilimo, kuchunga mifugo na kutunza familia kama sehemu ya maisha ya kila siku,” amesema.

Amesema kitendo cha Diwani wa Kata hiyo, Tinson Nzunda kuja na uwekezaji huo amekuwa mkombozi kwao kiuchumi jambo ambalo  limewasaidia  kuanzisha miradi ya kimkakati kama kilimo, mifugo na mingineyo ya kujiingizia kipato.

“Kwa sasa nimeweza kuzalisha mazao yangu binafsi kupitia mshahara ninaopata, nasomesha watoto na kutokuwa tegemezi tena,” amesema.

Akizungumza na Mwananchi Digital Jumatatu Mei 26, 2025, Diwani Kata ya Nyimbili, Tinson Nzunda amesema awali alibaini kuwepo kwa changamoto ya  mfumo dume kwa wanawake na hata vijana kujihusisha na uharifu.

“Unajua kwenye jamii kama hakuna ajira ni changamoto kubwa, lakini mimi kama kiongozi niliona hilo na kulazimika kuishirikisha jamii yenye uwezo kupata ajira, jambo ambalo lilileta hamasa kubwa hususani kwa wanawake,”amesema.

Nzunda amesema awali alianza na watu 50, lakini idadi imeongezeka mpaka  kufikia 300, huku mikakati ni kutoa ujira kwa  wananchi 500.

Nzunda amesema kufuatia uwekezaji huo ameweza  kubadili mifumo ya maisha ya wananchi na kupunguza vitendo vya uharifu kwa vijana wasio na ajira.

Kuhusu ujira wa kuchakata kahawa

Amesema wastani kwa siku wakiingia asubuhi uchakata tani 50 mpaka 60, kulingana na wingi wa kahawa sambamba na kupatiwa huduma zote yakiwepo maziwa na chakula nje ya malipo yao.

“Nilibaini changamoto nikatafuta suruhisho la  kugusa wananchi wanao nizunguka lengo ni kuunga mkono jitihada za serikali kuondoa changamoto ya ajira kwa vijana nchini,”amesema.

Wakati huohuo, Nzunda amesema amezalisha vitalu vya miche  ya  kahawa milioni  moja  kupitia Taasisi ya Utafiti wa  Kahawa (TaCRI), kituo cha Mbimba Mkoa wa Songwe ambayo itatolewa kwa wananchi.

“Miche hiyo inamudu  kukabiliana na magonjwa ya majani maarufu kama” kutu,” na wadudu waharibifu wakiwepo konokono zao ,”amesema.

Amesema ameweka mikakati ya kutoa elimu kwa wananchi kuhusiana na uzalishaji wa mazao mseto kwa lengo la kuwaondoa na dhana ya kilimo cha mazoea.

“Unajua wakulima wamezoea mazao ya kutegemea mvua, lakini wakigeukia kilimo mseto kila mwaka watazalisha mazao ya chakula na biashara na  kujikwamia kiuchumi,” amesema.

Related Posts