Dar es Salaam. Kusainiwa kwa mkataba wa Sh28 bilioni kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha kisasa cha upandikizaji wa figo na mafunzo mjini Dodoma ni hatua inayodhihirisha dhamira ya Tanzania kuwa kinara wa huduma maalumu za afya ukanda wa Kusini mwa Jangwa la Sahara na kuwa mkombozi wa maisha ya maelfu ya watu wanaohitaji huduma hizo.
Mkataba huo wa makubaliano (MoU), umesainiwa Jumatatu, Mei 26, 2025, kati ya Tanzania na Shirika la Matibabu la Tokushukai kutoka Japan. Huu si mradi wa kawaida wa ujenzi wa hospitali.
Usainiwaji huo, ulioshuhudiwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa unawakilisha uwekezaji wa kimkakati katika sekta ya afya unaolenga kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha rufaa kwa matibabu tata, hususan magonjwa ya figo yanayoongezeka barani kote kwa mujibu wa ofisa mwandamizi wa Serikali.
Kituo hicho, kitakachojengwa ndani ya Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH), kitakuwa kikubwa zaidi katika nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara.

Mbali na kutoa huduma za upandikizaji wa figo, pia kitawezesha mafunzo kwa wataalamu wa afya kutoka mataifa mbalimbali ya Afrika.
Kwa Tanzania, huu si mradi wa miundombinu pekee ya afya, bali ni hatua ya kuongoza katika diplomasia ya afya, kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Huduma za Tiba wa Wizara ya Afya, Dk Hamad Nyembea.
Amesema mradi huo utakuza ushirikiano wa huduma za afya kati ya Tanzania na mataifa mengine kama Comoro, Zambia, Malawi, Burundi, DRC na Burkina Faso, kupitia matibabu na kubadilishana utaalamu wa kitabibu.
“Tumezungumza na nchi hizi na tumekubaliana namna bora ya kushirikiana katika kuboresha huduma za afya barani Afrika. Wataalamu wetu pia watatembelea nchi hizo ili kubadilishana uzoefu na kujifunza kutokana na mafanikio yao,” amesema Dk Nyembea.
Kwa sasa, BMH hufanya hadi upandikizaji wa figo kwa wagonjwa saba kwa mwaka, huku Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) kupitia vituo vya Upanga na Mloganzila ikihudumia kati ya tisa hadi kumi kwa mwaka.
“Tunalenga kuongeza huduma maalumu za matibabu kutoka maeneo manane hadi kufikia 17. Wakati huohuo, tunawekeza katika kuboresha huduma za afya kwa asilimia 80 ya Watanzania wanaohitaji matibabu ya kawaida ambayo tunakusudia yaweze kupatikana kwa urahisi kupitia bima ya afya kwa wote,” amesema Dk Nyembea.
Akizungumzia maendeleo hayo, Makamu wa Rais wa Chama cha Madaktari wa Magonjwa ya Figo Tanzania (NESOT), Profesa Paschal Ruggajo, amesema kituo hicho kitakuwa kitovu cha umahiri katika huduma za figo, mafunzo, utafiti na ubunifu kwa ukanda wa Afrika Mashariki, Kati na Kusini (ECSA).
Amesema tangu Tanzania ianze upandikizaji wa figo mwaka 2017, zaidi ya wagonjwa 200 wamepata huduma hiyo nchini, jambo lililookoa hadi asilimia 80 ya gharama zilizokuwa zikitumika kuwatibu nje ya nchi.
“Gharama ya kumtibu mgonjwa mmoja nje ya nchi sasa inaweza kutumika kuwahudumia hadi wagonjwa wanne hapa nchini,” amesema Profesa Ruggajo.
Tanzania kwa sasa ina kati ya wagonjwa 3,200 hadi 3,500 wanaopata huduma ya kusafishwa damu (dialysis) na asilimia 15 hadi 20 wanaweza kufanyiwa upandikizaji.
Akizungumza wakati wa hafla ya usainiwaji wa MoU nchini Japan Jumatatu, Mkurugenzi Mtendaji wa BMH, Profesa Abel Makubi, amesema mradi huo unalenga kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha kikanda cha upandikizaji figo na mafunzo ya kitaalamu.
“MoU hii inaanzisha kituo cha umahiri kwa huduma za upandikizaji wa figo nchini Tanzania na katika ukanda wote wa Kusini mwa Sahara,” amesema Profesa Makubi.
Amesema kituo hicho hakitatoa tu huduma za upandikizaji, bali pia kitaendesha mafunzo ya wataalamu wa afya na kufanya tafiti za kuzuia na kupunguza magonjwa ya figo. Mafunzo hayo yataendeshwa kwa ushirikiano kati ya Hospitali ya Benjamin Mkapa na Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM).