Dar es Salaam. Wakati Chadema, wakitoa msimamo wa kutojibu barua ya msajili wa vyama vya siasa, msajili huyo ameeleza hatua atakazochukua baada ya chama hicho kukaidi maelekezo yake.
Maelekezo aliyotoa msajili kwa Chadema ni kutaka liitishwe Baraza Kuu la chama hicho ili wapate wajumbe wa Kamati Kuu na Sekretarieti, hata hivyo, Chadema kupitia Kamati Kuu kiliazimia kutokujibu kwa kile walichodai ofisi ya msajili haina mamlaka ya kuwapangia viongozi.
Mzizi wa yote hayo ni barua ya malalamiko iliyowasilishwa na aliyekuwa mwenyekiti wa Chadema Wilaya ya Mwanga mkoani Kilimanjaro, Lembrus Mchome akisema chama hicho kimekiuka katiba yake katika mchakato wa uthibitishwaji wa wajumbe hao.
Hadi Mchome anafikisha barua hiyo kwa Msajili alikiandikia chama chake na kabla ya kujibiwa aliwasilisha malalamiko hayo katika Ofisi ya Msajili.
Mchome alikuwa akilalamikia kwamba akidi ya Baraza Kuu haikutimia wakati wa kuwathibitisha viongozi hao. Alisema kikao hicho, kilipaswa kuwa na wajumbe 309, badala ya 85 waliokuwepo ambao ni sawa asilimia 20.6. Kutokana na hilo, Mchome aliiomba Ofisi ya Msajili kuingilia kati ili waliothibitishwa kinyume cha utaratibu watangazwe kuwa batili, wasitumikie nafasi zao hadi uthibitishaji halali utakapofanyika.
Kutokana na msimamo huo wa Chadema, Ofisi ya Msajili leo Jumanne Mei 27,2025 imetoa taarifa kwa umma ikitaja hatua ilizozichukua ambazo ni kutowatambua viongozi wanane waliopitishwa na Baraza Kuu lililoketi Januari 22,2025.
Viongozi wanaolalamikiwa na msajili na kuamua kuwaweka kando hadi Baraza kuu jingine litakapoitishwa ni Katibu Mkuu, John Mnyika, Amani Golugwa (Naibu Katibu Mkuu – Bara) na Ally Ibrahim Juma (Naibu Katibu Mkuu – Zanzibar).
Wengine ni wajumbe wa kamati huu Godbless Lema, Rose Mayemba, Salma Kasanzu, Hafidh Ally Saleh pamoja na Dk Rugemeleza Nshala, ambaye aliteuliwa kuwa mwanasheria mkuu wa chama hicho.
Hatua nyingine kwa mujibu wa barua ya Msajili ni kuwasimamisha wanaojifanya kuwa ni viongozi kufanya shughuli za kisiasa kwa mujibu wa kifungu cha 21E cha sheria ya vyama vya siasa.
“Ofisi ya Msajili wa vyama vya siasa inawasihi wananchi, wadau mamlaka na taasisi zote za Serikali na binafsi, kutowapa ushirikiano na huduma wanachama walioorodheshwa hapo juu.
“Endapo watahitaji kuzipata kama viongozi wa Chadema, kwa mujibu wa kifungu cha 4(5),(a)(b),8B 10(f) vya Sheria ya Vyama vya siasa sura ya 258 na kanuni ya 31 ya kanuni za usajili na ufuatiliaji wa vyama vya siasa za mwaka 2019,”imeeleza sehemu ya taarifa hiyo.
Mbali na hilo imeamua kusitisha kuwapa ruzuku hadi watakapotekeleza maelekezo ya Msajili wa Vyama vya Siasa, kwa sababu chama hicho hakina viongozi wanaoweza kusimamia mapato, matumizi na mrejesho wa fedha hizo za umma.
Mkurugenzi wa Sheria wa Chadema, Dk Nshala Rugemeleza amesema wameona taarifa ya Msajili, hivyo watakwenda kupambana naye kisheria.
“Nimesoma taarifa ya msajili wa vyama vya siasa, ina upotoshaji mkubwa na madaraka ambayo amesema anayatumia ni kutaka kuiua Chadema kwa makusudi . Sasa majibu atakayopambana nayo yatakuwa ya kisheria yeye si mtu mwisho wa kutafsiri sheria.”
“Tutapambana naye kisheria dhidi ya hatua zake alizozichukua, maana amekiuka sheria ni ajenda ya siri ya kutaka Chadema ife,”amesema Dk Rugemeleza.