Wizara yatenga Sh10 bilioni kushughulikia migogoro ya ndoa

Dodoma. Kutokana na ongezeko la matukio ya kuvunjika kwa ndoa nchini, Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Makundi Maalumu imeandaa mkakati mahsusi wa kukabiliana na changamoto hiyo na kuimarisha ustawi wa familia.

Hayo ni miongoni mwa vipaumbele vya bajeti ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2025/2026, ambapo kati ya maeneo matano ya kipaumbele, moja ni kushughulikia changamoto za ndoa katika jamii.

Wizara hiyo imewasilisha ombi kwa Bunge kuidhinisha Sh76.05 bilioni kwa ajili ya kugharamia utekelezaji wa vipaumbele hivyo, ikiwa ni pamoja na kukabiliana na ongezeko la matukio ya kuvunjika kwa ndoa.

Waziri wa wizara hiyo, Dk Dorothy Gwajima, amesema hayo leo, Mei 27, 2025, bungeni wakati akiwasilisha hotuba ya bajeti ya wizara yake, ambapo aliainisha vipaumbele vitano, ikiwemo huduma ya usuluhishi wa ndoa ambayo imetengewa Sh10.3 bilioni.

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, Dk Dorothy Gwajima akipongezana na Naibu Waziri wa Wizara hiyo, Mwananidi Ali Khamis mara baada ya kuwasilisha bungeni makadirio ya mapato na matumizi ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2025/ 2026.

Aidha, fedha hizo zimepangwa pia kusaidia uratibu na uboreshaji wa utoaji wa huduma za ustawi wa jamii, hususan katika mahabusu za watoto, pamoja na huduma za malezi ya kambo na uasili.

Dk Gwajima amesema tatizo la kuvunjika kwa ndoa limekuwa likitajwa mara kwa mara na linazidi kuchukua nafasi kubwa miongoni mwa matatizo yanayopelekwa mahakamani, huku wengi wakiachana bila kufika mahakamani.

Kwa mujibu wa ripoti ya utafiti ya ufuatiliaji wa kaya (NPS) kwa mwaka 2020/21 iliyotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), ilionyesha asilimia 57 ya Watanzania hawako kwenye ndoa.

Michango mingi ya maswali ya wabunge, imekuwa ikitaja kitendo hicho kama sehemu mojawapo ya kuchangia kuzaliwa kwa kundi la watoto wasio kwenye makazi maalumu (watoto wa mtaani), kwani ndoa nyingi zinapovunjika mzigo wa kulea watoto huachwa kwa mama pekee.

Akizungumzia uamuzi wa wizara kuweka kipaumbele kwenye usuluhishi wa ndoa, Mchungaji mstaafu Jackson Magomba amesema chanzo kikuu cha migogoro ya ndoa ni kupungua kwa hofu ya Mungu miongoni mwa wanandoa.

Aidha, amesema watu wengi wamekuwa wakilaumu upande mmoja kuwa chanzo cha matatizo ya ndoa bila kujitathmini au kutafakari mchango wao katika changamoto hizo.

Mchungaji Magomba amesema katika kipindi cha utumishi wake ndani ya kanisa kwa miaka 29, amekutana na mambo mengi ya kutaka kuvunja ndoa ambayo wakati mwingine yalimweka majaribuni, kwani wasaidizi wake wa karibu wamekuwa wanataka kuvunja ndoa.

“Wakati mwingine nyumba zinaficha mambo mengi, hata hizo mnazosema ni ndoa, wakati mwingine si ndoa kwani watu wanakutana ndani ya nyumba lakini kila mmoja analala chumba chake na wakitoka wanatokea mlango mmoja na kucheka. Ninyi mnaona ni ndoa; fuatilieni, tatizo ni kubwa zaidi,” amesema mchungaji huyo ambaye anaona hata hizo fedha zilizotengwa ni kidogo, kwani hazitasaidia.

Dk Gwajima pia amelieleza Bunge kuwa, mbali na fedha zilizotengwa kwa ajili ya huduma za usuluhishi wa ndoa, kiasi kingine cha fedha kimeelekezwa katika kuongeza ushiriki wa jamii katika kupanga na kutekeleza miradi ya maendeleo inayotokana na vipaumbele vya ngazi ya msingi, ambapo Sh15 bilioni zimetengwa kwa ajili hiyo.

Aidha, kwa upande wa uratibu na uendelezaji wa makundi maalumu, wakiwemo wafanyabiashara wadogo, zimetengwa Sh12 bilioni.

“Eneo la kuboresha mazingira ya kufundisha na kujifunzia katika taasisi na vyuo vya ustawi na maendeleo ya jamii zimetengwa Sh8.5 bilioni. Sh2.5 zitatumika kwenye ufuatiliaji na ushiriki wa mashirika yasiyo ya kiserikali katika maendeleo ya Taifa, wakati ufuatiliaji na tathmini ikitengewa Sh90 milioni.”

Maeneo mengine yanayopewa kipaumbele ni kutambua, kuratibu maendeleo na ustawi wa makundi maalumu wakiwemo watoto, wazee na wafanyabiashara ndogondogo; kuboresha mazingira ya kufundisha na kujifunzia katika taasisi na vyuo vya ustawi na maendeleo ya jamii; lakini pia kuimarisha mazingira ya ushiriki na mchango wa mashirika yasiyo ya kiserikali katika maendeleo ya Taifa.

Wakichangia mjadala wa bajeti ya wizara hiyo, Mbunge wa Kuteuliwa, Profesa Shukrani Manya, amesema maadili kwa Watanzania yameporomoka kwa kiasi kikubwa, ndiyo maana wanaume wanawatelekeza watoto wao.

Profesa Manya amesema katika maeneo mengi nchini kumeshuhudiwa watu wakizitelekeza familia zao, hasa watoto waliowazaa, na ndipo inaibuka wimbi la watoto wa mitaani, lakini akaitaka Serikali kutafuta namna bora ya kupeleka elimu kwa watu.

“Kimsingi, hakuna mimba za mitaani na hivyo hakuna watoto wa mitaani, lakini tukubaliane kwamba kuna mahali maadili yamesahaulika au uwajibikaji umekuwa mdogo. Kuzaa mtoto na kumtelekeza ni dhambi kubwa,” amesema Profesa Manya.

Mbunge wa Viti Maalumu, Munde Tambwe, amelalamikia taasisi na mashirika yasiyo ya kiserikali kwamba yamekuwa kichaka cha kujificha na kuwatapeli watu kwa mgongo wa imani za kidini, jambo alilosema halikubaliki.

Munde amesema ndani ya Taifa kuna asasi ambazo zinajulikana zinaendelea kufundisha mmomonyoko wa maadili na mambo yasiyofaa kwa watoto, lakini ni kama Serikali imefumba macho na haiwachukulii hatua zinazostahili wahusika wote.

Naye Mbunge wa Kinondoni, Tarimba Abbas (CCM), ameitaka Serikali kuondoa usiri na badala yake iwe inawatangaza hadharani watu wenye kesi za ubakaji, na hata inapofika wamehukumiwa majina yao yaanikwe hadharani ili wawe kwenye orodha ya aibu (blacklist).

“Mashauri ya ukatili yanamalizwa nyumbani, hii siyo sawa kabisa. Haya mambo yasiwe na mapatano, bali wanaofanya mambo hayo waanze kutangazwa mapema wakati kesi zikiendelea, na utakapofika mwisho basi wawe kwenye orodha. Lakini kwenye vyombo vya maamuzi hebu watusaidie kesi zisichukue muda mrefu,” amesema Tarimba.

Mbunge wa Viti Maalumu, Dk Teya Ntala, amegusia suala la misuko kwa wanaume na uvaaji mavazi yasiyo na staha, ikiwemo kwa wasanii, lakini akasema inashangaza kuona Serikali ikiendelea kuwashangilia.

Dk Ntala ametaja sheria ya ndoa ya mwaka 1992 kwamba imekuwa tatizo badala ya suluhisho, hasa watu wanapojificha kwenye kivuli cha balehe.

“Lakini yote kwa yote, naona hawa Polisi wapo hapa. Nataka kuhoji kwa nini isije sheria tupitishe humu ili mtu akibainika kwa kosa la ubakaji, adhabu yake ahasiwe kabisa.

“Nawaomba Polisi mshughulike na wanaume wa aina hiyo. Hakikisheni mnamwachia sehemu ndogo kwa ajili ya kupatia haja ndogo tu,” amesema Dk Ntala.

Kuhusu ukatili wa ubakaji, amesema ni tishio, huku akitaja Sheria ya Ndoa ya mwaka 1972 kwamba inatumika kuwakandamiza watoto wa kike.

Kamati ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii wamesema miradi mingi ya maendeleo imetekelezeka kwa kasi isiyoridhisha na mingine kutotekelezeka kutokana na ucheleweshwaji wa fedha za maendeleo.

Mwenyekiti wa kamati hiyo, Fatuma Toufiq, ameitaka Serikali ijielekeze zaidi kwenye kutumia vyanzo vya ndani vya mapato katika kutekeleza miradi ya maendeleo kutokana na uzoefu kuwa upatikanaji wa fedha za nje umekuwa wa kusuasua.

Kingine alichogusia ni mwenendo usioridhisha wa utoaji wa mikopo kwa wafanyabiashara wadogowadogo. Kwa mwaka wa fedha 2024/25, Wizara ilipokea Sh8 bilioni kwa ajili ya kuwawezesha wafanyabiashara hao kupata mikopo.

Hata hivyo, hadi kufikia Machi 2025, Wizara kupitia Benki ya NMB ilikuwa imekopesha Sh197.5 milioni pekee kwa wafanyabiashara 119, huku idadi ya waombaji ikiwa ni 1,389 waliokuwa wameomba jumla ya Sh2.96 bilioni.

Related Posts