Ukweli daima ni msingi na nguzo ya uongozi bora

Moja ya tabia njema muhimu maishani ni kusema ukweli na kuukubali, hata pale ambapo ladha yake haipendezi au pale ambako kuna sababu za kuuchukia.

Tabia ya kuwa mkweli ni nguzo ya msingi katika uongozi bora, iwe ndani ya familia, darasani, katika jamii, taasisi au hata taifa.

Ndiyo maana ukweli ni msingi wa utawala bora na wa kidemokrasia na si ajabu kuona viongozi wakuu wa nchi yetu, akiwemo Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi, akiahidi kuongoza kwa misingi ya ukweli na uwazi.

Hata hivyo, kwa masikitiko, tabia hii ya ukweli haionekani katika mwenendo wa Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo wa Zanzibar, Tabia Maulid Mwita, hasa katika mchakato wa marekebisho ya sheria zinazohusu sekta ya habari.

Kwa zaidi ya mara kumi katika kipindi cha miaka mitatu, Waziri Tabia amekuwa akieleza kwamba mchakato wa marekebisho ya sheria unaolalamikiwa umefikia hatua za mwisho.

Kauli hizo zimekuwa zikitolewa mara kwa mara kwenye makongamano, vikao mbalimbali, na hata ndani ya Baraza la Wawakilishi (kama kumbukumbu rasmi zinavyoonyesha).

Waziri aliwahi kusema kuwa mchakato umekamilika kwa zaidi ya asilimia 80 na kwamba muda wowote muswada wa marekebisho ungefika Bungeni.

Lakini pamoja na ahadi hizo, na licha ya kuwa Rais Mwinyi aliwahakikishia waandishi wa habari kuwa kilio chao kimesikika na kitashughulikiwa, Waziri Tabia amebadilisha msimamo na sasa anasema wasubiri serikali mpya baada ya uchaguzi wa Oktoba.

Hili ni jambo la kusikitisha, kwani hoja ya mapungufu ya sheria za habari si ya jana wala juzi, ni kilio cha karibu miaka 20, wakati Waziri Tabia bado akiwa shule.

Tabia ya kudanganya waandishi wa habari na jamii kwa ujumla si jambo linalompendeza kiongozi yeyote.

Mbaya zaidi, Waziri anadai kuwa waandishi wenyewe hawaelewani. Kwa kauli ya wazi, hili si la kweli.

Kama wasingeelewana, mchakato usingefikia hatua alizowahi kueleza kama hatua za mwisho. Kauli kama hizi zinaonekana kama jaribio la kuwasambaratisha wanahabari, kuwaonyesha kama watu wasiojitambua au wasiokuwa na msimamo, jambo ambalo si la haki.

Waziri angekuwa mkweli zaidi kama angesema sababu halisi za kucheleweshwa kwa mchakato huu wa marekebisho badala ya kuwabebesha waandishi lawama ambazo si zao. Ningependekeza pia, kwa busara, kwamba awaombe radhi waandishi wa habari, kwa sababu ni ukweli usiopingika kwamba kumekuwa na maelewano mazuri katika vikao vingi vya kutafuta suluhisho. Muungwana akikosea, kuomba radhi ni jambo la kawaida na la heshima.

Kama tunavyosema kwamba maadili yanawataka waandishi wawe wakweli, basi vivyo hivyo, viongozi nao wanapaswa kuwa wakweli.

Udanganyifu, popote pale hauna tija. Katika suala hili la habari, inaonyesha kana kwamba serikali imesahau ahadi yake ya kuendesha nchi kwa misingi ya ukweli na uwazi.

Wataalamu wa malezi wanatuasa kwamba hata kumdanganya mtoto si tabia nzuri, kwani inampotosha aamini udanganyifu ni jambo jema.

Dini zetu pia zinakataza udanganyifu katika familia, ndoa na jamii. Kwa sasa, ikiwa imebaki miezi michache kabla ya uchaguzi, sheria za habari zilizopo si rafiki kwa wanahabari, kwani zimejaa vikwazo vinavyowakosesha uhuru wa kusema ukweli. Taifa haliwezi kutarajia maendeleo kama wanahabari wataanza kuficha ukweli au kudanganya jamii.

Aidha, haiwezekani kuwa na uchaguzi wa wazi, huru na wa haki kama wanahabari wanazuiwa hata kuripoti matokeo ya kura yaliyobandikwa ukutani.

Waandishi wa habari wameeleza mara nyingi mapungufu ya sheria zilizopo, na kulikuwa na matumaini kwamba kilio chao kimesikika.

Lakini ghafla, Waziri Tabia anakuja na kauli mpya, akipuuza ahadi zake kwa wanahabari na taifa.

Wazee walituasa tusidharau wengine tukidhani hawana akili, kwani akili nyingi zikikutana huleta maarifa. Historia itafichua nani alikuwa mkweli kwenye suala hili.

Kilio cha uhuru wa habari na uhuru wa kujieleza ni haki ya msingi ya wananchi. Waswahili wanasema, kila mlango una ufunguo wake, ipo siku ufunguo utapatikana na waandishi wa habari wa Zanzibar watahisi wako huru na kuthaminiwa, badala ya kudharauliwa kwa kudanganywa mara kwa mara.

Kwa sasa, daraja walilotegemea wanahabari ili kulihudumia taifa kwa weledi na kuimarisha uhusiano kati ya jamii na serikali limevunjwa.

Lililopo sasa ni kujifunza kuogelea kuvuka upande wa pili salama, lakini tukumbuke: katika wengi kuna mengi, na miongoni mwa hayo ni watu wanaotoa ahadi za mdomoni, si za moyoni.