Washington. Rais wa Marekani, Donald Trump ametoa onyo kwa Rais Vladimir Putin wa Russia kitendo cha kukwamisha jitihada za kumaliza vita yake na Ukraine ni sawa na kusema kuwa ‘anacheza na moto’.
Matamshi hayo ya Trump yamekuja baada ya kumkosa kiongozi hiyo wa Russia baada ya Putin kuamuru utekelezwaji wa mashambulizi mapya ya anga nchini Ukraine.
Baada ya kutekeleza mashambulizi hayo ya Russia na kusababisha vifo vya watu zaidi ya 12 na majeruhi nchini Ukraine, Trump alitangaza kuwa Marekani itaiwekea Russia vikwazo wakati wowote.
“Kile ambacho Vladimir Putin hakitambui ni kwamba kama si mimi, mambo mengi mabaya sana yangekuwa tayari yameikumba Russia na ninamaanisha mambo mabaya sana,” amesema Trump kupitia chapisho lake kwenye mtandao wa Truth Social huku akisisitiza kuwa Putin ‘anacheza na moto!’
Trump hakufafanua kwa kina mambo ambayo yangempata Rais Putin. Gazeti la Wall Street Journal na CNN viliripoti kuwa Trump sasa anaangalia uwezekano wa kuiwekea Russia vikwazo vipya vya kiuchumi.
Akizungumza na waandishi wa habari Jumapili, Trump alisema kuwa ana uhakika kwa asilimia 100 kuwa ataiwekea vikwazo vipya Russia endapo haitobadili msimamo wake kuhusiana na mzozo wa Ukraine.
“Vita hivi ni kosa la Joe Biden na Rais Trump ameweka wazi kuwa anataka kuona makubaliano ya amani kwa njia ya mazungumzo. Rais Trump pia kwa busara ameweka uelekeo wa maamuzi yake,” amesema Msemaji wa Ikulu, Karoline Leavitt.
Hata hivyo, shutuma za hivi karibuni kutoka kwa Trump zinaashiria mabadiliko makubwa ya mtazamo wake wa awali kuhusu Putin, ambaye hapo awali alikuwa akimsifu na mara nyingi huku akikwepa kumkosoa hadharani.
Mbali na hilo, Rais Trump ameelezea kukatishwa tamaa na mwenendo na msimamo wa Russia juu ya mapigano hayo ya Ukraine yaliyodumu kwa zaidi ya minne.
Russia nayo imekuwa ikiishutumu Ukraine kwa kuvuruga mipango ya amani ambayo imekuwa ikipangwa na wawakilishi wa pande mbili za mgogoro huo sambamba na wapatanishi hususan ni Marekani.
Wakati huo, wabunge wa Marekani wameongeza presha kwa Trump kuiwekea Russia vikwazo ambapo Seneta mkongwe wa Chama cha Republican, Chuck Grassley ameomba hatua kali zichukuliwe dhidi ya Russia ili kumkumbusha Putin kuwa Marekani haimchekei tena.
Mbali na Grassley, maseneta wengine wawili wa chama cha Republican, Lindsey Graham na chama cha Democrat, Richard Blumenthal nao walitoa wito wa vikwazo vizito dhidi ya nchi zinazonunua mafuta, gesi na malighafi kutoka Russia.
Wakati maseneta wakiibua pendekezo hilo, Ofisa Usalama Mwandamizi wa Russia, Dmitry Medvedev amemuonya Trump juu ya hatari ya kuibuka kwa vita ya tatu ya dunia kwa kumwambia Putin kuwa anacheza na moto.
Medvedev amesema Vita ya tatu ya dunia ndiyo jambo bay asana ambalo linapswa kuogopwa na kila mtu duniani.
“Kuhusu kauli ya Trump kwamba Putin ‘anacheza na moto’ na ‘mambo mabaya’ kuikumba Russia. Ninajua jambo moja tu baya sana vita ya tatu ya dunia. Naamini Trump analielewa hili!,” ameandika Medvedev kwenye akaunti yake ya mtandao wa X.
Imeandikwa na Mgongo Kaitira kwa msaada wa mashirika ya habari.