Mbeya. Pamoja na kutabiriwa ushindi, lakini baadhi ya wananchi, wadau na wachambuzi wa siasa jijini Mbeya, wamesema uamuzi wa Dk Tulia Ackson kugombea jimbo la Uyole haikuwa kazi nyepesi, huku wakitaja maeneo yanayomsubiri iwapo atapenya.
Hivi karibuni Dk Tulia alitangaza nia ya kugombea jimbo jipya la Uyole baada ya kuliongoza jimbo la Mbeya Mjini kwa miaka 10, ikiwamo mitano ya kuchaguliwa.
Hiyo ilikuwa ni baada ya Tume huru ya Taifa ya uchaguzi (INEC) kutangaza kuligawa jimbo la Mbeya Mjini baada ya kukidhi vigezo ikiwamo idadi ya watu, japokuwa baadhi ya wananchi walionesha kutokubaliana na kigezo hicho.
Kwa mujibu wa INEC kigezo cha kuligawa jimbo kuwe na idadi ya watu wasiopungua wastani wa 600,000 kwa eneo la mjini na wastani wa watu 400,000 kwa eneo la majimbo ya vijijini.
Takwimu za Jimbo la Mbeya mjini zinaonesha kuwa na zaidi ya watu 682,264 kwa wanaoingia na kutoka kutokana na shughuli mbalimbali, huku takwimu za sensa ya mwaka 2022 zikionesha jimbo hilo kuwa na watu 541,603.
Baada ya kugawanywa jimbo hilo, inafanya Mbeya Mjini kuwa na watu 254,748, ikiwa na Kata 23 huku Jimbo jipya la Uyole likiwa na wakazi 286,857 na Kata 13.
Wakati Dk Tulia akifikia uamuzi huo, wananchi, wadau na wachambuzi wamesema kigogo huyo asitarajie mteremko kutokana na mambo yanayomsubiri ikiwamo upinzani na miundombinu.
Ikumbukwe uchaguzi mkuu wa madiwani, wabunge na Rais, unatarajia kufanyika Oktoba mwaka huu, huku Chama Cha Mapinduzi (CCM) kikitangaza Juni 28 makada kuanza kuchukua na kurejesha fomu.

Hadi sasa hakuna kada wa CCM aliyetangaza wala kutajwa kutaka kutia nia ya kugombea Jimbo la Uyole zaidi ya Dk Tulia, ambaye kama hali itabaki hivihivi, atapambana na wagombea wa vyama vingine vya siasa.
Mkazi wa Mtaa wa Uyole, Tifah Mwankemwa amesema kilio cha wengi katika jimbo hilo jipya la Uyole ni barabara na maji.
Amesema mbunge yeyote atakayefanikiwa kupenya katika uchaguzi mkuu, ajue ataenda kupimwa na vilio hivyo.
“Maeneo mengi barabara ni mbovu, huduma ya maji hakuna na baadhi ya wananchi hawana umeme, kwa mantiki hiyo, awe Dk Tulia au mwingine tunahitaji atupe uhakika wa huduma hizi,” amesema Tifah.
Naye Odilo Benson amesema hali ya uchumi kwa wakazi wa Uyole siyo nzuri sana, hivyo kiongozi ajaye atapaswa kupambania mazingira rafiki kwenye eneo la uchumi.
“Ikiwezekana wajasiriamali wapewe mikopo isiyo na riba au yenye masharti nafuu ili kujikwamua kiuchumi, bado kuna sehemu shule na vituo vya afya vipo mbali” amesema Benson.
Mdau wa siasa jijini Mbeya, Charles Mwasote amesema pamoja na Dk Tulia kutangaza nia yake mapema, wana Uyole wasiweke mawazo kwa Tulia pekee, wapo wapinzani pia wanalitazama jimbo hili.
Boniface Mwabukusi ambaye ni rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) ndiye anatajwa kugombea jimbo hilo jipya kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).
Hata hivyo, alipotafutwa na Mwananchi kuzungumzia tetesi hizo amesema: “Mimi sijui kama wananitaja ila nilishaeleza msimamo wangu kuwa safari hii sitagombea na msimamo wangu uko vizuri tu pale kwenye akaunti yangu ya X. Ninawashukuru wanaoniona ninafaa na wanaoniamini ila safari hii (uchaguzi mkuu 2025) nimeshasema sitagombea. Nina mambo ya kuyafanya kwa sasa”

Akizungumza na wafuasi wa CCM wakati wa kutangaza nia ya kung’atuka Jimbo la Mbeya Mjini, Dk Tulia alisema anafahamu wapo watakaojitokeza kwenye jimbo hilo.
Alisema pamoja na yote, anawakaribisha wote sehemu yoyote, huku akitahadharisha wanaoenda Jimbo la Uyole wajipange.
“Mbeya Mjini tumefanya mengi, japo bado kulikuwa na mahitaji lakini acha niwape nafasi wengine, nikabadilishe huko kwingine, wapo watakaokuja hapa ninapoondoka na kule niendako, ila wajipange,” alisema Dk Tulia.
Alisema anatoa rai kwa wana Mbeya Mjini wachague kiongozi na mtumishi kwa sababu kuna miradi mkubwa inaendelea kutekelezwa jimboni humo inahitaji usimamizi makini.