Shinyanga. Vikundi 56 vya kina mama, vijana na watu wenye ulemavu katika Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga vimeaswa kutotoa fedha yoyote kwa mtu yeyote atakayewafuata akidai ‘shukurani’ baada ya kupatiwa mikopo ya asilimia 10.
Badala yake, wametakiwa kutoa taarifa kwa mamlaka husika ili hatua stahiki zichukuliwe dhidi ya wahusika.
Akizungumza leo, Mei 28, 2025, katika shughuli ya utoaji wa mikopo kwa vikundi 56 vilivyokidhi vigezo, Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Julius Mtatiro amesema kuwa kumekuwa na baadhi ya watendaji na watumishi wa Serikali wanaodai fedha kutoka kwa vikundi vinavyopatiwa mikopo, kwa madai kuwa wao walihusika katika kuviunda.
“Mikopo hii si matokeo ya juhudi za watumishi, bali ni haki yenu kama wananchi. Watumishi wanalipwa mshahara kwa ajili ya kuratibu mchakato huu, si kudai fedha kutoka kwa vikundi.
“Msikubali kuwapa hela. Kuna watu wanapita mlango wa nyuma kuomba pesa mkiwaona, toeni taarifa mapema ili hatua zichukuliwe,” amesema Mtatiro.

Kwa upande wake Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Jamii katika Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga, Joseph Ntomela amesema kuwa katika awamu ya pili wamekabidhi hundi yenye thamani ya Sh537.8 milioni yenye lengo la kuwawezesha wanavikundi kujikwamua kiuchumi na kukabiliana na changamoto za umaskini.
Aidha, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga, Dk Kalekwa Kasanga amebainisha kuwa bado kuna changamoto kubwa ya urejeshaji mikopo kwa baadhi ya vikundi.
“Jumla ya Sh865 milioni kutoka kwa vikundi 100 vilivyopata mikopo katika awamu ya kwanza bado haijarejeshwa. Tunawahimiza wanavikundi hao kurejesha mikopo hiyo mapema ili vingine viweze kufaidika na fursa hii,” amesema Kasanga.
Baadhi ya wanavikundi waliopata mikopo wameeleza kuwa baadhi ya watumishi wa Serikali kuomba ‘shukrani’ kutoka kwa wanavikundi hao, lakini pia wameonyesha matumaini kuwa mikopo hiyo itawasaidia kwa kiasi kikubwa kujikwamua kiuchumi.

“Binafsi, hii ni mara yangu ya kwanza kupatiwa mkopo huu. Sijawahi kuona mtumishi yeyote aliyeomba pesa za shukrani, suala hili nalisikia tu sina uhakika kama lipo kweli. Ikiwa halijatokea kwangu, basi kwa wengine limetokea,” amesema Regina Onesmo.
“Ingawa kuna suala la kuombwa pesa, tumepewa namba za viongozi wa juu na tutawajulisha kwa siri tukiwabaini wale waliotekeleza vitendo hivyo, ili kuweka ulinzi binafsi na kuhakikisha haki inatendeka,” amesema Jamaldin Abdallah.