Utouh: Fedha za umma hazina itikadi za kisiasa

Dodoma. Aliyekuwa Mdhibiti na Mkaguzi mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Ludovick Utouh amesema fedha za umma hazina itikadi za kisiasa na badala yake zinapaswa kuleta maendeleo kwa wananchi ambao ndiyo wamiliki wa rasilimali.

Ametoa kauli hiyo leo Mei 28, 2025 jijini Dodoma katika ufunguzi wa mafunzo kuelekea utekelezaji mradi wa ‘Raia Makini’. Mradi huo unatarajiwa kugharimu Euro 1.1 milioni (Sawa na Sh3.3 bilioni) huku ukitekelezwa kwa miezi 30 katika mikoa mbalimbali Tanzania Bara na Zanzibar.

Katika utekelezaji wake utahusisha makundi mbalimbali ikiwemo waandishi wa habari, wawakilishi kutoka serikalini na mashirika yasiyokuwa ya kiserikali (NGO’s). Utekelezaji wake unasimamiwa na Wajibu Institute, Policy Forum ukifadhiliwa na Umoja wa Ulaya.

Utouh ambaye pia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Wajibu Institute, amesema mradi huo unakuja ili kuchochea uwajibikaji bora katika usimamizi wa fedha za umma kwenye utekelezaji wa shughuli mbalimbali.

“Lazima kuwa wenye taarifa na uelewa mpana wa maswala ya uwajibikaji ambao wataweza kushirikiana na Serikali katika kusimamia fedha za umma, kudai uwajibikaji pamoja na kupinga rushwa,” amesema Utouh.

Kauli ya Utouh inakuja ikiwa ni siku chache tangu CAG, Charles Kichere kuwasilisha ripoti yake ya mwaka 2023/2024 ambayo ilionyesha kuwapo kwa ubadhilifu wa fedha za umma katika maeneo mbalimbali ikiwemo mashirika ya umma.

Hali hiyo ilifanya kuwapo kwa maoni mbalimbali ya wadau wakishinikiza wote waliotajwa kufanya ubadhilifu au kuisababishia Serikali hasara kuchukuliwa hatua na iwekewe wazi ili iwe fundisho kwa wengine. 

Amesema katika utekelezaji wake wanatarajia kuwapo kwa mageuzi ya kifikra miongoni mwa wananchi ndiyo maana waliona ulazima wa kuwapo ushirikiano wa wadau mbalimbali, ikiwemo Serikali yenyewe na Azaki za kiraia.

“Ndiyo maana tunasema mradi shirikishi, tunalenga kuhamasisha ushiriki wa wananchi katika usimamizi wa fedha za umma kwenye  makusanyo na matumizi, kwani fedha hizo hazina itikadi za kisiasa. Itikadi ya kisiasa ni moja tu kuwaletea wananchi maendeleo, hivyo kuna umuhimu mkubwa wa kuhakikisha fedha zinazokusanywa zitumike kama zilivyoainishwa na Bunge,” amesema Utouh.

Amesema mradi huo pia unalenga kumjenga Mtanzania anayejielewa na anayeshiriki kwenye mfumo wa bajeti katika kufuatilia utekelezaji wa miradi ya Serikali.

Katika utekelezaji tunalenga kuzalisha na kusambaza taarifa kwa lugha rahisi kuhusu usimamizi wa fedha za umma, kwa ajili ya kuwawezesha wananchi na wadau wasio wa Serikali kushiriki kwenye mijadala ya umma na midahalo ya sera, na kushawishi mageuzi ya sheria na kuimarisha mifumo,” amesema Utouh.

Amesema pia wataimarisha uwezo wa wadau wa uwajibikaji kuhusu usimamizi wa fedha za umma ili waweze kushiriki kikamilifu na kwa ufanisi katika kudai uwazi na uwajibikaji kutoka kwa wenye mamlaka katika ngazi ya kitaifa na za wilaya.

Mkurugenzi wa ukaguzi wa mifumo ya Tehama Ofisi ya CAG Zanzibar, Juma Mohammed Juma amesema kuwapo kwa mradi huo kutasaidia kuimarisha utawala bora nchini.

Related Posts