Dar es Salaam. Baada ya miaka minne ya ukusanyaji wa kodi ya majengo kupitia mfumo wa ununuzi wa umeme kwa kutumia mashine za Luku, inaripotiwa kuwa Serikali ipo katika hatua za mwisho za kubadilisha mfumo huo.
Kuanzia mwaka ujao wa fedha, kodi hiyo inatarajiwa kukusanywa moja kwa moja kupitia halmashauri.
Mchakato wa maandalizi tayari umeanza na halmashauri zimeanza kuhakiki upya taarifa za majengo, zikishirikisha wenyeviti wa Serikali za mitaa, watendaji na hata walimu katika baadhi ya maeneo.
Baadhi ya wenyeviti wa mitaa waliozungumza na Mwananchi kwa sharti la kutotajwa majina yao (kwa kuwa si wasemaji rasmi wa Serikali), wamesema kazi ya uhakiki inaendelea rasmi na mfumo mpya wa malipo kupitia halmashauri utaanza kutumika katika mwaka wa fedha 2025/26.
“Mchakato unaendelea sasa; tunahakiki nyumba moja baada ya nyingine, tunakusanya namba ya mita, namba ya simu, majina ya mmiliki na kitambulisho cha Nida ili kuingizwa kwenye mfumo mpya wa kulipia kodi ya majengo,” amesema mmoja wa wenyeviti wa mtaa mkoani Pwani.
Naye mtendaji mmoja wa kata jijini Dar es Salaam, amesema kuanzia mwaka ujao wa fedha, wananchi hawatalazimika tena kulipa kodi ya majengo kupitia ununuaji wa umeme. “Ile Sh1,500 ambayo ilikuwa inakatwa kila mwezi ukiweka umeme haitakatwa tena; badala yake, kodi ya majengo italipwa moja kwa moja halmashauri,” amefafanua.
Amesema baada ya kukamilika kwa usajili wa majengo unaoendelea sasa, mfumo mpya utaanza Julai, mwaka huu.
“Tumeambiwa wamiliki wa majengo watapewa namba za malipo ya Serikali, ili kulipa kodi ya mwaka mzima kwenye halmashauri husika. Kwa sasa inatajwa kuwa ni Sh18,000 kwa mwaka, ingawa bado hatujapewa maelezo kamili kama italipwa yote kwa mara moja au kama kutakuwa na fursa ya kulipa kwa awamu,” amesema.
Aidha, amesema watendaji waliopo karibu na wananchi ndiyo watakaokuwa mstari wa mbele kuhakikisha wamiliki wanalipa kwa wakati. “Endapo kuna ambaye hatalipa, halmashauri itawatuma watendaji hao kufuatilia na kuchukua hatua stahiki,” amesema.
Mwananchi ilipozungumza na Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Felchesmi Mramba kuhusu Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) kuondolewa kwenye utaratibu wa ukusanyaji kodi ya majengo kupitia Luku, amesema jambo hilo si la Tanesco bali ni la Wizara ya Fedha.
“Mabadiliko kama haya sijui kama yapo, lakini hata kama yapo, basi Waziri wa Fedha ndiye anayeyatangaza wakati wa kuhitimisha bajeti. Kumbuka, utaratibu wa kulipia kodi ya majengo kupitia Luku uliwekwa kupitia hotuba ya Waziri wa Fedha mwaka 2021. Hivyo, kama kutakuwa na mabadiliko, atatoa taarifa rasmi kama alivyofanya mwanzo,” amesema Mramba.
AlipotafutwaWaziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba atolee ufafanuzi suala hilo, simu yake iliita bila kupokewa.
Hata hivyo, Msemaji wa Wizara ya Fedha, Ben Mwaipaja ameiambia Mwananchi kuwamajibu wanayo Wizara ya Tamisemi.
“Kwangu mimi ni mapema mno kuzungumzia kipimo cha bajeti kuu. Mwenye majibu sahihi ni mtu wa Tamisemi,” amesema Mwaipaja.
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti, Oran Njeza amesema mchakato huo upo na kinachoangaliwa ni kuboresha mfumo wa ukusanyaji mapato.
“Uboreshaji wa ukusanyaji mapato unategemea mfumo utakaorahisisha kubaini majengo na kuyakusanya. Urahisi wa kubaini majengo uko Tamisemi, kwa sababu halmashauri ndizo zinayajua majengo yaliyopo katika maeneo yao. Mfumo wa Kitehama utaboreshwa ili kuhakikisha tunakuwa na taarifa sahihi za majengo yote, wapi yapo, yako kwenye hali gani. Zaidi ya hapo, matokeo ya zoezi la sensa ya watu na makazi yatachangia kufanya kazi hii iwe rahisi zaidi,” amesema Njeza.
Alipoulizwa mchakato huo umefikia wapi, amesema kwa sasa Tamisemi inaendelea na kazi hiyo.
Katibu Mkuu wa Tamisemi, Adolf Ndunguru alipoulizwa kuhusu hatua hiyo, amesema:“Utaratibu wa kulipa kodi unatolewa bungeni. Umesikia Waziri wa Fedha amesema? Kama hajasema, basi tusubiri tamko rasmi kutoka kwake.”
Hata hivyo, tayari baadhi ya wamiliki wa majengo wameanza kupokea ujumbe mfupi wa maandishi (SMS) kutoka Tamisemi, ukiwataka kulipia kodi ya majengo Sh18,000.
Mchakato wa kulipia kodi za majengo kupitia Luku ulianza Juni 10, 2021, wakati akiwakilisha bungeni bajeti kuu Serikali kwa mwaka wa fedha 2021/22.
Waziri Mwigulu alisema watafanya marekebisho kwenye Sheria ya Kodi ya Majengo sura 289 ili ukusanyaji wa kodi ya majengo ufanyike kwa kutumia mfumo wa ununuzi na utumiaji wa umeme kupitia mashine za Luku.
Alisema kila mita ya umeme ina uhusiano na mmiliki wa jengo au mtumiaji wa mita, na kwa kuwa sheria ya kodi ya majengo inataka kodi hiyo ikusanywe kwa mmiliki au mtumiaji wa jengo, hivyo anapendekeza kodi ya majengo ya kiwango cha Sh1,000 kwa mwezi kwenye nyumba za kawaida zenye mita moja itakatwa kwenye ununuzi wa umeme (Luku).
“Napendekeza kiwango cha Sh5,000 kwa mwezi kwa kila ghorofa au apartment zenye mita moja na itakatwa kwenye ununuzi wa umeme. Serikali itaweka utaratibu kwenye nyumba za kawaida na za ghorofa zinazochangia mita moja na zinazotumia mita zaidi ya moja,” alisema ingawa baadae kiwango hicho kilipanda hadi Sh1,500 kwa nyumba za kawaida.
Awali, mpango huo ulipoanza uliibua lawama kwa wapangaji ambao walidai kulazimika kulipa kodi hiyo ilhali si wamiliki wa nyumba.
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ililitolea ufafanuzi mwaka 2012 ikieleza anayepaswa kulipa kodi hiyo na mmiliki na si mpangaji.
Pia, nyumba zilizokuwa na mita zaidi ya moja zilitozwa kodi hiyo kulingana na idadi ya mita zilizokuwepo si jengo.
Baadhi ya wananchi ambao tayari wamesajiliwa kuingia kwenye mfumo huo mpya wamesema ni utaratibu mzuri endapo halmashauri zitakusanya kodi hizo na kufanya kazi za maendeleo kwenye maeneo yao.
“Kama zitasaidia kuboresha barabara, kuleta maji, umeme na mambo mengine ya maendeleo ni sawa, lakini sio tunalipa tu, tukitaka maji tunaleta wenyewe, hivyo hivyo umeme, tukija kwenye barabara ndio usiseme hata kuleta greda likwangue ni shida,” amesema Rajabu Kondo wa Kibaha.
Mery Simwanza wa Temeke, amesema hofu yake ni pale itakapotakiwa pesa hiyo ilipwe kwa mkupuo yote Sh18,000.
“Tulipokuwa tunaandikishwa tumeambiwa control number tutakayopewa ni ya mwaka mzima, isije kuletwa unatakiwa ulipe deni lote papo hapo, wengi tutakwama, bora walete utaratibu wa kulipia kidogo kidogo hadi mwaka unakwisha na wewe unamaliza deni maana vipato haviligani,” amesema.
Kauli sawa na iliyotolewa na Meshack Aden wa Kigamboni Dar es Salaam ambaye amesema control number iwe ya mwaka mmoja, lakini itoe mwanya kwa atakayependa kulipa pesa yote kwa mkupuo alipe na atakayelipa kidogo kidogo naye alipe.
“Kikubwa tusibambikiane madeni, kama unavyolipa maji, wasije kuanza mara mfumo haujasoma umelipa halafu unadaiwa tena, kingine wachukue sawa kodi za majengo na wao watuboreshee huduma huku mitaani.”