Dodoma. Macho na masikio ya Watanzania kesho ni katika mkutano mkuu maalumu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), utakaoweka wazi Ilani yake ya Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba, 2025.
Mkutano huo umetanguliwa na vikao vya Kamati Kuu na Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya chama hicho vilivyofanyika jijini Dodoma kuanzia Mei 26 mwaka huu na kuhitimishwa leo Jumatano Mei 28, 2025.
Mambo mengine yanayotarajiwa ni kupendekezwa na kupitishwa kwa jina la Katibu Mkuu wa chama hicho baada ya aliyepo sasa, Dk Emmanuel Nchimbi kuteuliwa kuwa mgombea mwenza wa Samia Suluhu Hassan anayekwenda kupeperusha bendera ya chama hicho katika Uchaguzi Mkuu mwaka huu.
Vikao vya Halmashauri Kuu ya CCM vilivyofanyika kati ya Januari 18 na 19, 2025 jijini Dodoma, ndivyo vilivyopendekeza na kupitisha majina ya wagombea wa nafasi za urais na mgombea mwenza.
Katika vikao hivyo, Mwenyekiti wa chama hicho Rais Samia atagombea urais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania huku Dk Hassan Mwinyi akiteuliwa kuwa mgombea urais Zanzibar.
Aidha, katika mkutano huo maalumu ambao utafanyika kesho Mei 29, 2025 na Mei 30, katika ukumbi wa Jakaya Kikwete Convention Center jijini Dodoma, kutakuwa na mabadiliko madogo ya katiba ya chama hicho.
Machi 12, 2025 Katibu wa Halmashuri Kuu (NEC) Idara ya Oganazesheni Issa Haji Ussi alisema uamuzi uliofanywa na NEC, ni kuweka ukomo wa vipindi viwili vya miaka mitano kwa nafasi za ubunge, uwakilishi na udiwani wa viti maalumu.
Utaratibu wa ukomo wa nafasi za uongozi kwenye chama hicho, unafanyika hivyo kwa upande wa Rais wa Tanzania na Rais wa Zanzibar kwa kipindi kirefu ambapo ni vipindi viwili kama ilivyopitishwa na NEC.
Kwa mujibu wa Katibu wa NEC wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Amos Makala ajenda nyingine ni utekelezaji wa Ilani za uchaguzi ya mwaka 2020 hadi 2025 wa Serikali zote mbili ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ).
Mkutano huo unategemewa kuhudhuriwa na a watu 2700, huku 2,000 wakiwa ni wajumbe na waliobakia ni wageni waalikwa.
Wajumbe waelezea matarajio yao
Mjumbe wa mkutano mkuu huo, Anthony Mavunde amesema anatarajia kuona CCM ikitoa Ilani itakayokwenda kugusa na kubadilisha maisha ya Watanzania na kukifanya chama hicho kuwa sehemu ya utatuzi wa kero za wananchi.
“Tunatarajia katika Ilani itakayozinduliwa kesho, itakwenda kutoa majawabu katika masuala mengi yanayoigusa jamii yetu,” amesema Mavunde.
“Watanzania wakae mkao wa kula, watege masikio na macho kushuhudia na kusikiliza nyaraka (Ilani) itakayokwenda kubeba matumaini na kuwa sehemu ya kuboresha maisha ya Watanzania na utatuzi wa kero zao zinazowakabili,”amesema Mavunde ambaye ni mbunge wa Dodoma Mjini.
Mjumbe miwngine, Mashimba Ndaki amesema ana matarajio makubwa hasa ya kupitishwa kwa Ilani ya uchaguzi ya CCM ya mwaka 2025/30.
“Watanzani na wajumbe wa mkutano mkuu tuna matumaini makubwa kuwa kilichomo ndani ya Ilani matamanio ya Watanzania kuwa nchi yetu inapiga hatua,”amesema.
Ndaki ambaye ni mbunge wa Maswa Magharibi, mkoani Simiyu, amesema anatamani kuona maboresho makubwa katika Katiba ya CCM ili kutoa uhakika wa kukiendesha chama hicho kwa uwazi.
“Huu ndio utakuwa mkutano mkuu wa mwisho kwa Bunge hili la 12, nadhani tutatiwa moyo hasa wabunge kwamba kazi iliyofanywa na Bunge hili ilikuwa nzuri na ilisaidia kukipeleka chama kwa wananchi.
“Lakini lilihakikisha Serikali inasimamiwa vizuri na lengo lilikuwa kukamilisha mahitaji ya Watanzania,” amesema Ndaki aliyewahi kuwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi.
Naye Neema Lugangira, mjumbe kutoka mkoani Kagera, amesema anatarajia Ilani yao ya uchaguzi itatoa majawabu ya kuongeza kasi ya maendeleo ya Taifa.
“Ninachoamini mimi ni kwamba, hata kama mtu hazipendi rangi zetu, lazima ataipenda Ilani ya CCM,” amesema Lugangira.