Mawakili wa Serikali waitwa kunolewa utekeleza Dira ya Taifa

Dar es Salaam. Mawakili wa Serikali wameitwa kwa ajili ya mafunzo ya kuwajengea uwezo katika kutekeleza majukumu yao katika sekta mbalimbali, pamoja na mambo mengine kuwapa ujuzi wa utekelezaji Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 na majadiliano ya kumaliza kesi nje ya vyombo vya kisheria.

Mafunzo hayo ya siku tatu yatakayofanyika jijini Arusha katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa (AICC) kuanzia Juni 2 mpaka 4, 2025 yameandaliwa na Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jijini Dar es Salaam, Wakili Mkuu wa Serikali (Solicitor General – SG), Dk Ally Possi amesema kuwa mafunzo hayo yatawahusisha mawakili wote wa Serikali nchini.

Dk Possi amefafanua kuwa mawakili hao wa Serikali watakaohusika katika mafunzo hayo ni kutoka wizara, Taasisi, mashirika ya umma na Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) Bara na Zanzibar.

“Dhima kuu ya  kuwawezesha mawakili wa Serikali kutimiza wajibu wao wa kila siku,” amesema Dk Possi.

Amesema kuwa mafunzo hayo yatakuwa na kaulimbiu ya ” Ubobezi wa Kisheria kwa Ajili ya Kesho: Teknolojia, Mikakati na Mizania Binafsi kwa Mawakili wa Serikali katika Kutekeleza Dira ya Taifa ya Maendeleo, 2050.”

Kwa mujibu wa Dk Possi, wamechagua kaulimbiu hiyo kwa kuwa wao ni sehamu muhimu na mtambuka katika utekelezaji wa  Dira ya Taifa 2025 mpaka 2050.

Maelekezo wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 ni kuwa na Taifa lenye ustawi, haki na linalojitegemea.

Dk Possi  amesema kuwa katika kutimiza majukumu yao kama wanasheria, kuna mambo muhimu ambayo wao lazima waendane nayo kulingana na wakati.

“Mafunzo yamezingatia nafasi ya tasnia ya Sheria na majukumu ya mawakili wa Serikali katika nguzo mbalimbali za maendeleo ya Taifa ikiwemo uchumi Jumuishi na shindani”, amesema Dk Possi na kuongeza:

“Kwa hiyo na sisi mawakili wa Serikali hatuna budi kujiimarisha kwa kutoa mafunzo mbalimbali yatakayoendana na wakati. Hatuna budi kutoa mafunzo ya kimkakati kutuwezesha kuwa na utaalamu utakaoendana na mabadiliko ya sasa ya Teknolojia.”

Amesema kuwa kupitia mafunzo hayo mawakili wa Serikali watapata nafasi kujifunza kwa wataalamu wabobezi wa ndani na nje katika sekta ya sheria, teknolokia, uongozi.

Dk Possi amesema kuwa zitatolewa mada zinazohusiana na  wakati uliopo, ambazo ni pamoja na namna bora ya majadiliano ya kufikia suluhu nje ya vyombo vya kisheria, eneo ambalo amesema linahitaji ufahamu na uelewa mpana ili nchi iweze kufaidika na  uingiaji na majadiliano hayo.

Nyingine amezitaja kuwa ni kupata uelewa mpana wa sheria za uwekezaji kwa kuwa nchi yetu inatapata wawekezaji wengi, hivyo hawana bundi kuwawezesha mawakili wa Serikali  kupata uelewa katika eneo hilo.

Vilevile amesema kutakuwa na mada ya uelewa wa masoko ya mitaji, ambalo amesema ni eneo jipya pamoja na namna bora ya usimamizi mikataba ya miradi ya ujenzi sekta ambayo Serikali pia imewekeza, kwa kuwa nayo na ubobezi wake.

“Ni imani yetu kuwa mawakili tutajifunza mbinu za kisasa kutumia teknolojia na maarifa kutoa huduma za kisheria kwa weledi na kuiitetea Nchi katika vyombo vya kisheria kuendana na mabadiliko ya ya teknolojia katika karne ya 21,” amesema Dk Possi.

Akizungumzia mafunzo hayo, Wakili wa Serikali Stanley Kalokola ambaye alishiriki mafunzo hayo mwaka 2024, amesema kuwa ni muhimu na yana yana tija kubwa kwa mawakili wa Serikali.

Wakili Kalokola amesema kuwa taaluma ya sheria moja ya taaluma ambazo zinahitaji kujiendeleza kila siku na kwamba mafunzo hayo yaliyoandaliwa na Ofisi ya SG ni jukwaa muhimu la kumjenga Wakili wa Serikali.

“Kila mara yanatokea marekebisho ya Sheria. Kwa hiyo mafunzo haya no jukwaa la kuwawezesha mawakili kujua mabadiliko mbalimbali yanayotokea katika Sheria na sekta nyingine,” amesema Wakili Kalokola na kuongeza:

“Mawakili wa Serikali wako katika wizara, taasisi, mashirika ya umma wakala na Ofisi za Serikali za Mitaa. Kwa hiyo mafunzo hayo pia mi jukwaa la kubadilishana uzoefu katika kuboresha utendaji kazi wa mawakili wa Serikali.”

Mbali na mafunzo hayo ya mawakili yatakayofunguliwa rasmi na Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Damasi Ndumbalo, Jumi 3, 2025, pia Dk Possi amesema kuwa katika siku ya kilele watazindua Mfumo wa Usimamizi wa Mashauri.

Mfumo huo amebainisha kuwa utakuwa unasajili na kuhifadhi taarifa mashauri yatakayoendeshwa.

Related Posts