Viongozi wa dini watoa neno suluhu ya mashauri ya ndoa

Dar es Salaam. Wakati Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu ikija na mkakati wa kushughulikia mashauri ya ndoa kwa kutenga fungu kwa ajili hiyo, viongozi wa dini wameshauri nguvu ielekezwe kwenye kukabiliana na kiini cha changamoto hiyo.

Mei 27,2025 akiwasilisha bajeti bungeni jana, Waziri Dk Dorothy Gwajima alisema wizara hiyo imeandaa mkakati wa kukabiliana na changamoto hiyo na Sh10.3 bilioni imetengwa kwa ajili ya huduma ya usuluhishi wa ndoa.

Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na wizara hiyo, hadi kufikia Aprili 2025, mashauri 97,234 ya ndoa yameshughulikiwa kupitia vitengo vya ustawi wa jamii kuanzia ngazi ya halmashauri hadi Taifa, idadi hiyo ikiwa ni ongezeko la mashauri 31,380 yaliyowasilishwa kipindi kama hicho mwaka 2023/24.

Kati ya mashauri hayo, 81,820 yalipatiwa ufumbuzi huku mashauri 15,414 yakipelekwa mahakamani kwa hatua zaidi.

Akizungumza na Mwananchi leo Jumatano Mei 28, 2025, Askofu mstaafu wa Kanisa Katoliki, Methodius Kilaini amesema licha ya Serikali kuwa na nia njema kwa kutenga fedha kwa ajili ya utatuzi wa migogoro ya ndoa ni vyema nguvu kubwa ikawekwa kwenye kutibu kiini cha migogoro hiyo.

Katika hilo askofu Kilaini ameshauri uwekezaji mkubwa ungefanyika kutoa elimu na kutengenezwa kwa programu maalumu kwa vijana kabla ya kuingia kwenye ndoa ili wajue thamani ya taasisi hiyo.

Amesema programu hizo zinapaswa kuhusisha viongozi wa dini, wanasaikolojia, madaktari na wataalamu wengine wanaohusika katika ujenzi wa taasisi ya familia.

“Siku hizi ndoa zinapata matatizo kwa sababu watu wanaingia wakiwa hawajajiandaa na hawajui maana ya taasisi hiyo, matokeo ya hili ndiyo tunasikia ndani ya muda mfupi wanandoa wametengana.

“Athari yake haiishii kwao, taasisi ya ndoa ikiandamwa na misukosuko jamii nzima inaandamwa, watoto hawawezi kukua katika misingi bora, hili ni jambo linalopaswa kuangaliwa kwa umakini zaidi,” amesema Askofu Kilaini.

Hilo limeelezwa pia na Askofu wa Kanisa la Anglican dayosisi ya Dar es Salaam, Jackson Sosteness ambaye amesema kinachotakiwa kuwekewa nguvu kwa sasa ni kuzuia tatizo na sio kusubiri hadi litokee.

“Tukiri huenda tunaopaswa kufundisha maadili hatujafanya kazi yetu sawa, taasisi ya familia nayo imeshindwa kuwandaa vijana katika misingi ya kwenda kudumu kwenye ndoa. Kutokana na ukweli huu basi tunapaswa kuweka nguvu kubwa kwenye kizazi kijacho ili kuzuia tatizo hili lisiendelee.

“Uwekezaji usifanyike zaidi kwenye kutengeneza ajira kwa watu ambao wakati mwingine hawana hiyo shauku au inawezekana na wao hawaamini katika taasisi ya ndoa, ndiyo maana nasema tuwekeze kwenye kiini cha tatizo tukianzia kwa hawa watoto, elimu itolewe kuanzia ngazi ya familia,” amesema Askofu Sosteness.

Mwenyekiti wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya Baraza la Waislam Tanzania (Bakwata), Sheikh Khamis Mataka amesema ni muhimu kwa wanajamii kurudi katika misingi ya dini na kuzingatia inachoelekeza kuhusu ndoa.

“Ukisimamia misingi ya dini huwezi kupata shida,tukija kwenye suala la ndoa turudi katika dini tuangalie inatuelekeza kufanya nini. Tukiyajua na kuzingatia maelekezo basi kila kitu kitakwenda sawia.

“Mwanamume atajua wajibu wake na mwanamke atafahamu vitu gani azingatie kama mke ndani na nje ya nyumba. Dini inazuia masuala ya kutoka nje ya ndoa sasa kama unazingatia mafundisho hayo suala la michepuko halitakuwa na nafasi kwako, amani, upendo na utulivu vitatawala kwenye ndoa yenu,”amesema Sheikh Mataka.

Amesema wanandoa ni zao la jamii, kuna mmomonyoko mkubwa wa maadili kwenye jamii ambayo haiishi kidini, uongo umekuwa sehemu ya maisha, kukosa uaminifu inaonekana ndio ujanja.

Amesema katika hali kama hiyo,  ndoa haiwezi kudumu.

Wakati Serikali ikiweka mkakati huo, ripoti ya tathmini ya miaka mitatu ya Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia kilicho chini ya Mahakama ya Tanzania, inaonesha kutengana kwa wanandoa na uzinzi ndiyo sababu zinazoongoza ndoa nyingi kufikia hatua ya kutolewa talaka.

Uchunguzi huo uliohusisha mashauri 1,348 ya ndoa  uliolenga kubaini maelezo sahihi na kutathmini hali halisi ya migogoro ya ndoa, ili kufikia suluhu bora kwa pande zote ulibaini kwamba wanandoa wengi wanaofikia kutalikiana huanza kwa kutengana.

Tathmini hiyo inaonesha kuwa, katika kipindi cha miaka mitatu jumla ya mashauri 4,843 ya ndoa yalifunguliwa huku mwaka 2023 ukiweka rekodi ya kuwa na mashauri mengi zaidi ya ndoa na kesi 2,425 zilifunguliwa.

Mwaka 2021 mashauri 672 ya ndoa yalirekodiwa katika Ofisi ya Usuluhishi wa Migogoro ya Ndoa (OSJC) wakati mwaka 2022 yakirekodiwa mashauri 1,746, ikiwa ni ongezeko la asilimia 62 kutoka mwaka wa kwanza.

Ripoti hiyo inazitaja sababu sababu tano kuu zinazochangia kuongezeka kwa mashauri yanayolenga kuvunja ndoa ni pamoja na kutengana, ambayo inaongoza kwa asilimia 25 ya kesi zote, ikifuatiwa na uzinzi inayochangia asilimia 16.

Talaka ya Kiislamu inafuata kwa asilimia 15, ikifuatiwa na ukatili asilimia 14 na migogoro ya kifamilia na kutokuelewana kwa wanandoa inachangia asilimia 12.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo wanandoa wengi wanakutana na changamoto za kutokuelewana na hivyo hutafuta suluhu ya kutengana.

Kwa nini wanandoa hutengana

Mwanasaikolojia Christian Bwaya amesema wengi wo hufikia hatua ya kutengana kutokana na kukosa elimu sahihi kuhusu taasisi hiyo, hivyo wengi huingia wakiwa na matarajio tofauti msingi mkuu ambao ni upendo.

Amesema inapotokea pale matarajio yao yanaposhindwa kutimia, kutengana inakuwa njia rahisi kuikwepa taasisi ya ndoa na kupambania matamanio binafsi.

“Kinachotokea ni kwamba vijana wengi siku hizi hawaingii kwenye ndoa kwa sababu ya upendo, wanakuwa na matarajio yao kichwani na linaloonekana zaidi ni ngono, muonekano wa nje na kipato.

“Sasa inapotokea ameshaingia kwenye ndoa halafu anakutana na vitu tofauti na matarajio yake ndipo visa vinaanza, usaliti unatokea na migogoro ikishika kasi ndiyo wanatengana,” amesema Bwaya.

Amesema kutengana inatumika kama njia ya kukwepa kuwepo kwenye ndoa na migogoro ya aina hiyo isipotafutiwa ufumbuzi, kinachofuata ni kwa wanandoa kupeana talaka.

Bwaya ametaja sababu nyingine inayochangia ndoa nyingi za sasa kusambaratika ni matokeo ya kuingia kwenye uhusiano bila kushirikisha familia.

“Tofauti na ilivyokuwa zamani, kijana hadi kufikia hatua ya kufunga ndoa ni lazima familia ina ufahamu wa kina kuhusu mwenza wake na familia yake. Hii iliweza kupunguza migogoro kwa namna moja au nyingine.

“Siku hizi vijana wanakutana wanaanzisha uhusiano ghafla wanafunga ndoa hawajipi muda wa kufahamiana, hawatoi nafasi kwa familia zao kujuana vizuri na kusikiliza mawazo yao,” amesema.

Akizungumzia hilo, Askofu Mkuu mstaafu wa Kanisa la Anglikana Tanzania, Valentino Mokiwa amesema vijana wengi wanaoingia kwenye ndoa hawapati mafunzo ya kiroho kutoka kwa viongozi wao wa dini na kuwawezesha kufahamu uhalisia wa ndoa.

Amesema kutokana na hilo, wengi wanaingia kwenye ndoa bila kufahamu wanaenda kufanya nini na wanapaswa kusimamia vipi viapo vyao wanavyotoa wakati wanaoana.

“Siku hizi watu wanaingia kwenye ndoa hawajapata mafundisho ya kutosha ikitokea wamepata basi ni kwa siku moja au wiki. Siku moja haiwezi kumfanya mtu ajifunze na kuelewa undani wa ndoa, faida na hasara zake hapa viongozi wa dini tunapaswa kujitathmini.

“Tukiwafundisha hawa vijana tutawasaidia waishi kwa upendo, kumtanguliza Mungu katika kila jambo na ndoa zao zitadumu, tofauti na ilivyo sasa wanaingia wakiwa hawafahamu wanaenda kufanya nini, wanakwenda wakiwa na picha tofauti kuhusu ndoa yaani wanaiga kwa sababu fulani kaoa au kaolewa,”amesema Mokiwa.

Related Posts