Dodoma. Mbunge wa Viti Maalum, Halima Mdee ‘amewaka’ bungeni akitaka Serikali ieleze hatima ya wananchi wa mitaa saba katika majimbo ya Kawe na Kibamba jijini Dar es Salaam.
Mdee ametoa kauli hiyo bungeni jijini Dodoma leo Alhamisi Mei 29, 2025 wakati akichangia hotuba ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa mwaka 2025/26.
Hata hivyo, Waziri wa Wizara hiyo, Deo Ndejembi amekiri kuwepo kwa migogoro hiyo lakini akasema tayari walishakaa na wahusika katika eneo hilo ambalo lina nyumba zaidi ya 200,000 na tayari mipango mizuri inaendelea.
Katika mchango wake, Mdee amezungumzia usumbufu na adha wanayokutana nayo wananchi wa mitaa ya Mabwepande, Mbopo na Madale katika jimbo la Kawe na wale wa Tegeta A, Msumi A, Msumi B na Kulangwa ambayo jimbo la Kibamba akisema wapo kihalali lakini wanaonewa.
Amesema Ndejembi ni waziri wa tatu kutaka kusikiliza mgogoro huo ambao mara ya kwanza alikuwepo Waziri Angelina Mabula kisha Jelly Silaa lakini wote hawakufikia mwisho ndiyo akamuomba ajitahidi kuumaliza ili wananchi wapate haki yao.
Kwa mujibu wa Mdee, Shirika la DDC lilichukua ardhi hiyo mwaka 1980 kikiwa ni kijiji lakini hawakufuata utaratibu uliotakiwa na kisha wakapatiwa hati ya umiliki.
“Walisema wanataka kufanya shughuli za kilimo na ufugaji lakini hawajawahi kulima mchicha wala kufuga hata kuku badala yake wanawasumbua wananchi zaidi ya 250,000 walioko kwenye mitaa hiyo ambao wapo wa asili na wale waliouziwa maeneo,” amesema Mdee.
Ameyataja matangazo ya Serikali la Februari 10, 2024 lililotoka kwa Mkurugenzi wa wilaya ya Kinondoni akitaka kuuza viwanja katika eneo hilo na tangazo la Mei 9, 2025 lililotolewa na mtu aliyemtaja kwa jina la Shedrack Maxmiliani lenye maudhui kama hayo.
Mbunge wa Kibanda (CCM), Issa Mtemvu ametoa taarifa kwa Mdee akisema kumekuwa na hatua nzuri za utatuzi wa mgogoro huo na kwamba viwanja vinavyotangazwa ni vile ambavyo bado viko wazi na kila kimoja kinauzwa Sh15,000 kwa mita za mraba wakati waliojenga wanauziwa Sh3000 kwa mita za mraba.
Hata hivyo, taarifa hiyo ilikataliwa na Mdee aliyewahi kuwa mbunge wa Kawe akisema jambo analolizungumza ana ushahidi nalo kwani amekuwa mbunge kwa miaka 20 sasa hivyo hawezi kusema maneno ya uongo ambayo hana vielelezo.