Dar es Salaam. Wajumbe wa mkutano mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) wameridhia kwa kauli moja marekebisho matatu madogo ya katiba yake ya 1977, toleo la Januari 2025 ya kufanya mikutano ya kidijitali ili kuendana na kasi ya mabadiliko ya teknolojia.
Mbali na marekebisho hayo, kuongezwa kwa namba ya wadhamini wa chama hicho kutoka wanane hadi tisa ili kukidhi sheria ya vyama vya siasa na rekebisho jingine ni kamati za siasa za mikoa na wilaya kukasimiwa miradi kwa maandishi kutoka kwa wadhamini wa chama hicho.
Mabadiliko hayo madogo ya katiba yamewasilishwa mbele ya wajumbe wa mkutano mkuu leo Alhamisi, Mei 29, 2025 jijini Dodoma na Mwenyekiti wa chama hicho, Rais Samia Suluhu Hassan.
Rais Samia amesema mabadiliko hayo yanayolenga kuongeza utendaji kazi yalipendekezwa na oganaizesheni ya chama hicho.
“Tumefunga mitambo ya kuweza kuwasiliana mikoa kwa mikoa au wilaya kwa wilaya ili kurahisisha utendaji wa kazi iliyopendekezwa na idara ya oganaizesheni, kikao cha kwanza ni sekretarieti ya wilaya, kamati ya siasa ya wilaya, sekretarieti ya mkoa, kamati ya siasa ya mkoa.
“Sekretarieti maalumu ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, Sekretarieti ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, Kamati Maalumu ya Halmashauri Kuu ya Taifa, Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM na mkutano mkuu wa Taifa,” amesema.
Amesema mikutano hiyo wameiweka jinsi wanavyoendelea huko mbele watakuwa wanaenda na teknolojia na katiba yao kwani inawapa fursa ya kutunga kanuni za vikao hivyo.
“Kwa sasa tumeanza mikutano na halmashauri kuu za siasa za mikoa au wilaya lakini mikutano ile haimo katika maelekezo ya katiba yetu,” amesema.
Amesema kupitia mabadiliko hayo wameamua kuiingiza mikutano hiyo kwenye katiba ili isikiuke katiba ya chama na isiwe kinyume.
Amesema vikao hivyo vitafanyika endapo kuna ulazima au dharura ambapo vikao kwa ngazi ya mkoa na wilaya vitakuwa vinafanyika kwa idhini ya katibu mkuu wa chama hicho.
“Watamjulisha katibu mkuu kwa nini wanafanya vikao hivyo, kwa nini wanafanya vikao kwa njia mtandao ili kuepuka kutumika vibaya mitandao hii,” amesema Rais Samia.
Jambo la pili lililoridhiwa na wajumbe wa mkutano huo ni mabadiliko kwenye wajumbe wa baraza la wadhamini la chama hicho kwa kumuongeza mjumbe mmoja na kufikia tisa.
Wamefanya mabadiliko hayo ili kuendana na sheria ya vyama vya siasa namba 258 rejeo la mwaka 2019, inayoitaka wajumbe wa baraza la wadhamini wa vyama vya siasa wawe na idadi ambayo namba yake haigawanyiki kwa mbili.
“Iwe tatu, tano, tisa, 11, sasa baraza letu lina watu wanane, kwa hiyo tunapasa kumuongeza mmoja ili wawe tisa na hii inakwenda kwa mujibu wa katiba yetu na tunaileta ilikuwa na namba inayohitajika kwenye baraza la wadhamini,” amesema.
Kulingana na Rais Samia sehemu ya pili katika kuimarisha jitihada zake za kuinua uchumi wa kisiasa wanatazamia kutumia ushauri wa kitaalamu, katika shughuli zake za uwekezaji ili kuongeza tija.
“Chama chetu kwa sasa tunazipa nguvu kampuni zetu za chama ili ziweze kuzalisha kwa manufaa ya chama, ni muhimu wadhamini kujielekeza katika kuhakiki miradi lakini katika kutekeleza hilo, baraza la la wadhamini litatoa idhini kwa maandishi Katiba inavyosomeka sasa itakasimu madaraka hayo kwa kamati za siasa,”amesema.
Amesema kulingana na mabadiliko hayo kamati za siasa za mikoa na wilaya zitalazimika kuomba ridhaa kutoka kwa baraza la wadhamini.