Kibaha. Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Mkoa wa Pwani, imeokoa zaidi ya Sh300 milioni mali ya Kijiji cha Msufini, Wilaya ya Mkuranga, zilizokuwa zimechepushwa na kuingizwa kwenye akaunti ya mtu binafsi.
Kiasi hicho cha pesa kilitokana na malipo ya asilimia 10 ya mauzo ya ardhi ya Kijiji hicho iliyouzwa kwa kampuni binafsi.
Hayo yamebainishwa leo Mei 29,2025 na Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Pwani, Domina Mukama wakati akizungumza na waandishi wa habari mjini Kibaha.
Amesema kuwa baada ya mauzo ya ardhi hiyo mwanasheria wa kampuni iliyonunua eneo hilo alitengeneza akaunti ya bandia na kuingiza pesa hizo, huku akijua ni kinyume na taratibu zinazostahili.
“Pesa hizo ni mapato ya asilimia 10 ya mauzo ya ardhi ambapo kwa utaratibu zinatakiwa kutumika na kijiji, lakini huyu mwanasheria alizichepusha na kuingiza kwenye akaunti yake binafsi jambo ambalo ni kinyume na utaratibu”amesema.
Amesema kuwa kutokana na hilo, hivi sasa taasisi hiyo inaendelea kumfanyia uchunguzi ili kuchukua hatua zaidi dhidi yake.
“Pesa zote alizirudisha kwenye akaunti ya kijiji na tayari zinaendelea kutekeleza miradi ya maendeleo na sisi tunaendelea kumfanyia ufuatiliaji kabla ya kuendelea na hatua zingine,” amesema.
Baadhi ya wakazi wa Mkoa wa Pwani wamesema kuwa hatua ya Takukuru kuokoa kiasi hicho cha pesa, inaleta mwelekeo mzuri wa utendaji wa kazi kwa manufaa ya wengi.
“Hii ni hatua nzuri lakini ni vema mtuhumiwa akafikishwa mahakamani ili sheria ishike mkondo wake,” amesema Noel Mwakagenda.
Kwa upande wake Hassani Shabani ametoa wito kwa Takukuru kuongeza wigo wa kutoa elimu kwa wananchi juu ya uelewa wa njia za kupambana na vitendo vya rushwa ili kuwa na utambuzi wa kutosha.