Unguja. Korea Kusini imeeleza kuridhishwa na utekelezaji wa miradi inayofanywa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) kupitia ufadhili na mikopo ya masharti nafuu kutoka taifa hilo, na imeahidi kuendelea kuiunga mkono katika sekta nyingine za uchumi wa buluu.
Maeneo ambayo Korea Kusini imekuwa ikisaidia Zanzibar ni katika sekta ya elimu, ambapo mbali na kujenga maabara na kuipatia vifaa, pia imejikita katika kujenga uwezo wa walimu na wanafunzi kupitia Shirika la Maendeleo (KOICA).
Mwingine ni mradi wa ujenzi wa miundombinu ya umwagiliaji, uliogharimu Dola za Marekani milioni 68 (sawa na Sh183.396 bilioni), ambao pia unalenga kuwajengea uwezo wakulima ili watumie mbinu za kisasa badala ya kutegemea mvua.
Hayo yamebainika jana Mei, 2025 baada ya balozi wa Korea Kusini, Ahn Eunju kutembelea Zanzibar kwa mara ya kwanza na kufanya mazungumzo na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango, Dk Saada Mkuya.
Amesema ataangalia maeneo mengine ambayo Korea itaendelea kuisaidia Zanzibar katika harakati zake za maendeleo.
Balozi Eunju amesema wamefurahishwa na namna ambavyo miradi hiyo imetekelezwa na kwa sasa wanaangalia namna ya kuendelea kuisaidia Zanzibar ujenzi wa hospitali ya rufaa ya Binguni na kuwajengea uwezo katika uchumi wa buluu.
“Tunaridhika namna miradi inavyotekelezwa, yapo maeneo ambayo tumevutiwa kushirikiana, ikiwemo uchumi wa buluu, miundombinu na kwa hiyo tutaendelea kuisaidia Zanzibar ili kukuza uwezo wa watu wake,” amesema.
Naye Dk Mkuya amesema Zanzibar inashirikiana na Korea katika miradi mbalimbali ukiwemo wa umwagiliaji.
Kwa mujibu wa Waziri wa Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo, Shamata Shaame Khamis, wakati akiwasilisha bajeti ya wizara hiyo hivi karibuni barazani, alisema kuwa kupitia mradi wa umwagiliaji wa miaka mitano, uzalishaji wa mpunga umeongezeka ikilinganishwa na hali ya awali ambapo wakulima walitegemea mvua pekee, kabla ya kuwekwa kwa mifumo ya umwagiliaji.
Alisema wakulima walikuwa wanazalisha tani tano za mpunga kwa hekta moja lakini sasa wanazalisha tani 11 kwa hekta moja, na wanatarajia kufika uzalishaji wa tani 19 kwa hekta moja.
Akitaja miradi mingine ambayo inasaidiwa na Korea, Dk Mkuya amesema wamesaini ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Binguni ambayo itagharimu Dola za Marekani 160 milioni sawa na Sh431.52 bilioni.
“Pia tunashirikiana na Korea katika mradi wa ujenzi wa bandari ya Wete, barabara za Unguja na Pemba kilometa 246,” amesema Dk Mkuya.
Katika mpango wa kubadilisha sekta ya utalii Zanzibar, Korea Kusini imepanga kusaidia katika mradi mwingine wa ujenzi wa ukumbi mkubwa wa mikutano, ambao utajumuisha pia hospitali ya kisasa na viwanja vya michezo.
Kwa sasa, tayari kuna mpango kabambe wa utekelezaji wa mradi huo, na kinachosubiriwa ni upatikanaji wa fedha kwa ajili ya kuanza upembuzi yakinifu. Ujenzi wa miundombinu hiyo umepangwa kufanyika katika eneo la Fumba.