Arusha. Mahakama ya Rufaa imemuachia huru Regina Alex aliyehukumiwa kunyongwa hadi kufa, baada ya kutiwa hatiani kwa mauaji ya mtoto wa jirani yake, Janeth Samson aliyekuwa na umri wa mwaka mmoja na mwezi mmoja kwa kumtumbukiza kwenye kisima cha maji.
Ilielezwa kuwa mama wa mtoto huyo, Happiness John (shahidi wa pili), alimuachia Regina mtoto huyo (ambaye kwa sasa ni marehemu) kisha akaenda kuoga lakini alipomaliza (kuoga) hakumkuta mtoto wake na alipomuuliza Regina, alimweleza kuwa amemuacha nje.
Ilielezwa mahakamani hapo kuwa baada ya kuulizwa tena, mrufani huyo alimjibu Happiness kuwa labda amuangalie kwenye kisima, ambapo alipoenda alikuta mwili wa mtoto wake ukielea juu ya maji, kisha Regina akakamatwa na kushtakiwa kwa kosa la mauaji.
Regina alihukumiwa na Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza, Novemba 3, 2022 adhabu ya kunyongwa hadi kufa baada ya kukutwa na hatia ya mauaji ya mtoto huyo.
Hukumu ya rufaa iliyomwachia huru Regina ilitolewa Mei 27,2025 na jopo la majaji watatu wa Mahakama ya Rufaa walioketi Mwanza ambao ni Zephrine Galeba, Lilian Mashaka na Dk Deo Nangela, na nakala ya hukumu hiyo kuwekwa kwenye mtandao wa Mahakama.
Majaji hao walifikia uamuzi huo baada ya kupitia mwenendo wa kesi na kusikiliza hoja za pande zote mbili na kujiridhisha kuwa ushahidi wa kimazingira wa upande wa mashitaka katika kesi hiyo, uliomtia hatiani Regina ulikuwa dhaifu.
Katika kesi ya msingi, mauaji hayo yalitokea Juni 30, 2019, katika kijiji cha Lobatika, kilichopo Wilaya ya Bukombe, Mkoa wa Geita ambapo upande wa mashitaka ulikuwa na mashahidi wanne.
Ilielezwa kuwa mama wa marehemu (Happiness) na Regina walikuwa majirani na katika makazi yao kulikuwa na kisima walichokuwa wakitumia kuchota maji kwa ajili ya matumizi yao ya kila siku.
Shahidi wa kwanza, Catherine Paschal alieleza kuwa kisima hicho kilikuwa na kifuniko na kila siku jioni kilikuwa kikifungwa na kufunguliwa saa moja asubuhi.
Siku ya tukio mama wa marehemu alimuacha mtoto wake na mrufani huyo, kisha akaenda kuoga katika bafu lililokuwa nyuma ya nyumba kwani ilikuwa ni jioni na giza limeanza kuingia, ila alipomaliza (kuoga) hakumkuta mtoto wake.
Alieleza kuwa baada ya kupata wasiwasi alimuuliza Regina kama alikuwa na binti yake chumbani kwake, akajibu amemuacha nje, na baada ya kuulizwa tena alimweleza amuangalie kwenye kisima, ambapo alipoenda alikuta mwili wa mtoto wake ukielea juu ya maji (akiwa ameshafariki dunia).
Mashahidi wengine walikuwa ni ASP Richard Godbless na F. 6800 Koplo Akwilina.
Katika utetezi wake, Regina alikana kutenda kosa hilo ambapo Mahakama hiyo iliyosikiliza kesi hiyo ilieleza kuwa kesi dhidi yake imethibitishwa bila kuacha shaka na kumuhukumu adhabu hiyo.
Katika rufaa hiyo Regina alikuwa na sababu mbili akiwakilishwa na Wakili Emmanuel John huku Jamhuri ikiwakilishwa na mawakili wawili.
Sababu hizo ni upande wa mashitaka haukuthibitisha kwa ushahidi wa kimazingira kosa la mauaji dhidi ya mrufani , pia haukuthibitisha sababu ya kifo na nani aliyesababisha.
Wakili wa utetezi alieleza kuwa kulingana na rekodi ya rufaa hiyo , ingawa tukio hilo lilitokea wakati shahidi wa pili (mama wa mtoto) na mwenye nyumba wao walipokuwa nyumbani, ila shahidi huyo hakuitwa kutoa ushahidi wake.
Alidai kuwa kutokuwepo kwake sio sawa kwani ndiye aliyeshiriki kumtafuta marehemu na kusaidia kuupeleka mwili wa marehemu hospitalini na kuhitimisha kuwa shahidi huyo angesaidia kujua nani aliyefungua kisima hicho, kwa sababu ndiye hukifungua asubuhi na kukifunga jioni.
Ili kuunga mkono maoni hayo, aliegemea kesi ya Katona Rashid dhidi ya Jamhuri katika rufaa ya jinai ya mwaka 2016 iliyotolewa Mei 15, 2019.
Kuhusu sababu ya kwanza, wakili huyo alisema kwa kuwa kesi hiyo ilitokana na ushahidi wa kimazingira, ushahidi ulipaswa bila shaka uelekeze hatia ya mrufani kuliko wengine wote na kueleza kuwa huenda Janeth (marehemu kwa sasa), alienda kisimani peke yake na kuzama.
Kwa mujibu wake, bila kujali tuhuma hizo zilikuwa na nguvu kiasi gani, madai tu kwamba mrufani ndiye aliyekuwa mtu wa mwisho kuwa na marehemu hayatoshi, kama ilivyoamuliwa katika kesi ya Peter Mabara dhidi ya Jamhuri ,iliyotolewa uamuzi Desemba 14, 2017.
Kwa upande wao mawakili wa Jamhuri walipinga rufaa hiyo na kueleza kuwa kesi hiyo iliyokuwa ikitegemea ushahidi wa kimazingira, ilithibitishwa bila kuacha shaka dhidi ya mrufani huyo.
Walieleza kuwa katika ukurasa wa 23 hadi 25 wa rekodi ya rufaa, shahidi wa pili alimuachia mrufani mtoto wake kabla hajaenda kuoga na kuhitimisha kuwa siyo tu alikuwa mtu wa mwisho kuonekana na marehemu, bali alipewa jukumu la kumuangalia na mama yake aliyekwenda kuoga.
Wakili huyo aliieleza mahakama kwenye kesi ya Mathayo Mwalimu na mwingine dhidi ya Jamhuri katika rufaa ya jinai namna inayoelezea mtu wa mwisho kuonekana na marehemu katika kesi za mauaji.
Baada ya kusikiliza za pande zote mbili majaji hao walianza na sababu ya kwanza ambayo ni iwapo ushahidi wa kimazingira ulitosha kuthibitisha kesi bila kuacha shaka.
Jaji Nangela amesema kimsingi, kwa kuwa hakuna shahidi aliyemwona mrufani akimzamisha mtoto (marehemu) kisimani, ushahidi uliotumika kuunga mkono shitaka la mauaji dhidi ya mrufani ulikuwa wa mazingira.
Amesema ili ushahidi wa kimazingira utegemewe lazima utoe hitimisho moja tu, yaani, mtu anayedaiwa kutenda kosa alihusika, kwa namna fulani, katika utendaji wake na hakuna mtu mwingine.
“Tumezingatia hoja za mawakili wote wawili waliojifunza kulingana na mfumo uliotajwa hapo juu. Kwa maoni yetu, ingawa wakili wa Jamhuri alijaribu kuleta mchanganyiko kati ya mrufani na mazingira ya mara moja ambapo kosa lilifanyika.
“Ila kama tutakavyoonyesha hapa chini, alishindwa kuzingatia kwa kina na kuchambua kwa kina mwingiliano kati ya mrufani na mazingira ambayo uhalifu ulifanyika, kwa njia ambayo iliondoa uwezekano mwingine wote wa uhalifu kwa mtu mwingine.
Jaji huyo amesema katika ukurasa wa 22 wa rekodi ya rufaa, shahidi wa pili hawakuwa na mgogoro wowote na mrufani hivyo hakukuwa na sababu au nia mbaya ya kumfanya mrufani kumuua binti wa jirani yake.
Amesema ni wazi, kwa kuangalia mazingira ambapo uhalifu ulifanyika pamoja na mambo mengine muhimu yanayohusiana na hayo, kosa lilifanyika usiku, hakuna ushahidi kwamba kulikuwa na mwanga wowote.
Baada ya kutathmini ushahidi uliopo kwenye rekodi na, kwa kuzingatia mambo yote muhimu, ikiwa ni pamoja na maswali mengi ambayo walijiuliza wakati wa uchambuzi wao walifikia hitimisho kuwa ushahidi wa mashitaka ulikuwa dhaifu kumuunganisha mrufani na kosa hilo.
Jaji huyo amesema kwa sababu hiyo ya kwanza ya rufaa inatosha kuondoa rufaa hiyo na kufuta hukumu na adhabu dhidi ya Regina na kuamuru aachiwe huru.