Ndejembi aja kivingine kumaliza migogoro ya ardhi nchini

Dodoma. Bunge limepitisha bajeti ya Sh164.1 bilioni kwa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa mwaka 2025/26, fedha ambazo zitaelekezwa kwenye maeneo saba ya vipaumbele, yakiwamo mapambano dhidi ya migogoro ya ardhi nchini.

Waziri wa wizara hiyo, Deo Ndejembi, leo Alhamisi Mei 29, 2025, amewasilisha bajeti hiyo bungeni jijini Dodoma. Awali, ilipangwa kujadiliwa kwa siku mbili, lakini mjadala wake umedumu kwa saa mbili na nusu tu kabla ya kuhitimishwa.

Naibu Spika, Mussa Zungu aliyeongoza kikao hicho hakufafanua sababu za kuharakisha mjadala huo, lakini inafahamika kuwa wabunge wengi walihitajika kuhudhuria Mkutano Mkuu Maalum wa CCM ambao ni wajumbe.

Waziri Ndejembi ametaja maeneo ambayo bajeti hiyo itaelekezwa kuwa ni kuongeza kasi ya upangaji, upimaji, umilikishaji na usajili wa ardhi mijini, vijijini na maeneo ya kimkakati, sambamba na kuimarisha mifumo ya Tehama kwa ajili ya ukusanyaji wa maduhuli na upatikanaji wa taarifa za ardhi na uthamini.

Maeneo mengine ni kuimarisha mifumo ya utatuzi wa migogoro ya ardhi kwa njia ya kiutawala na kwenye mabaraza ya rrdhi na nyumba ya wilaya, kuhakikisha upatikanaji wa nyumba bora na kuendeleza sekta ya milki na makazi kwa maendeleo ya kiuchumi na kijamii.

Aidha, bajeti hiyo itaelekezwa kwenye kuimarisha mipaka ya kimataifa na miji ya mipakani, upatikanaji wa ramani kwa ajili ya mipango ya kitaifa na matumizi mengine, pamoja na kuimarisha mifumo ya usimamizi na ufuatiliaji wa utekelezaji wa vipaumbele vya sekta hiyo.

Katika mwaka wa fedha 2024/25, wizara iliahidi kuendelea kushughulikia migogoro ya ardhi kwa njia ya kiutawala kupitia mifumo ya kielektroniki, kwa kushirikiana na wadau, kupanga matumizi ya ardhi na kutoa elimu kwa umma kuhusu haki ya umiliki na madhara ya migogoro.

“Hadi kufikia Mei 15, 2025, jumla ya migogoro 5,801 ilitatuliwa kwa njia ya kiutawala, ikilinganishwa na lengo la awali la kutatua migogoro 3,000. Kwa mwaka 2025/26, tumepanga kushughulikia migogoro mingine 3, 000,” amesema.

Katika bajeti ya 2025/26, Wizara imepanga kuidhinisha jumla ya taarifa za uthamini 54,000, ambapo 20,000 ni za uthamini wa kawaida na 34,000 ni zenye wafidiwa.

Kwa lengo la kuharakisha utatuzi wa migogoro, Ndejembi amesema wizara ilianzisha mabaraza 18 mapya katika mwaka 2024/25, na kufanya jumla ya mabaraza ya ardhi na nyumba kufikia 115, hatua iliyopunguza mzigo wa malalamiko.

Kwa mwaka wa fedha 2025/26, Wizara imepanga kuanzisha mabaraza mengine 24, hatua itakayofanikisha kuwa na mabaraza ya ardhi na nyumba katika wilaya zote 139 nchini, na kusaidia kushughulikia mashauri 11,725 yaliyosalia pamoja na yale yatakayofunguliwa.

Kasi ya ongezeko la idadi ya watu mijini imetajwa kuchangia kwa kiasi kikubwa ukuaji wa makazi yasiyopangwa ambayo kwa mujibu wa Sensa ya Majengo ya mwaka 2022, yamefikia asilimia 67.1.

Sera ya Taifa ya Ardhi ya mwaka 1995, toleo la mwaka 2023, imehimiza uboreshaji wa maeneo chakavu na yasiyopangwa katika maeneo ya miji.

“Kwa kuzingatia takwa hilo la kisera, Wizara inaandaa Programu Maalumu ya Uendelezaji Upya wa Maeneo Chakavu katika miji mbalimbali nchini ambapo jumla ya maeneo 111 yenye ukubwa wa hekta 24,309.3 yameainishwa katika mikoa 24, kwa ajili ya kupangwa na kuendelezwa upya ili kuyafanya kuwa na tija kiuchumi na kijamii,” amesema Ndejembi.

Miongoni mwa maeneo ambayo yametajwa kuwa yanahitaji kuendelezwa ni Makangira lililopo Msasani, Dar es Salaam, kama eneo la mfano.

Kwa upande wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Serikali ilitoa kibali kwa shirika hilo kukopa Sh174 bilioni kwa ajili ya kuendelea na utekelezaji wa miradi hiyo.

Fedha hizo zimetekeleza Mradi wa Morocco Square wenye thamani ya Sh137 bilioni, ambao umekamilika, nyumba zote 100 zimeuzwa na maeneo mengine ya biashara na ofisi yamepangishwa.

Ujenzi mwingine ni Mradi wa Kawe 711 uliopewa Sh169 bilioni ambao hadi sasa uko asilimia 70 na unatarajiwa kukamilika katika mwaka wa fedha 2025/26.

Miradi mingine ni Golden Premier Residence wenye thamani ya Sh71 bilioni uliopo Kawe, ambapo mazungumzo kati ya mkandarasi na Shirika kuhusu kuwezesha kuendelea na ujenzi yanaendelea na yanatarajiwa kukamilika ifikapo Juni, 2025.

Kupitia taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii iliyosomwa na Makamu Mwenyekiti, Najma Giga, Serikali imetakiwa kurejesha utaratibu wa kodi ya pango la ardhi kukusanywa na wizara yenyewe kwa kuwa ndiyo ina nyenzo za kisheria na mifumo ya ukusanyaji wake.

Kamati imetaka Serikali itengeneze mipango na mbinu za kufuatilia wadaiwa wa pango la ardhi ili kuongeza mapato ya wizara, ikiwa ni pamoja na kupima, kupanga na kumilikisha ardhi (KKK).

Imependekeza Serikali iongeze kasi ya upangaji na upimaji wa ardhi ili kufikia lengo la viwanja 100,000 hadi Juni, 2025 na ihakikishe wizara inashirikiana na Tamisemi kuhimiza wakurugenzi wa halmashauri zenye uhitaji kufanya hivyo.

Mbunge wa Viti Maalumu, Halima Mdee ‘amewaka’ bungeni akitaka Serikali ieleze hatima ya wananchi wa mitaa saba katika majimbo ya Kawe na Kibamba jijini Dar es Salaam.

Waziri Ndejembi amekiri kuwepo kwa migogoro hiyo, lakini akasema tayari walishakaa na wahusika katika eneo hilo ambalo lina nyumba zaidi ya 200,000 na mipango mizuri inaendelea.

Katika mchango wake, Mdee amezungumzia usumbufu na adha wanazopata wananchi wa mitaa ya Mabwepande, Mbopo na Madale katika jimbo la Kawe, na wale wa Tegeta A, Msumi A, Msumi B na Kulangwa katika Jimbo la Kibamba, akisema wapo kihalali lakini wanaonewa.

Amesema Ndejembi ni waziri wa tatu kushughulikia mgogoro huo ambapo mara ya kwanza ulikuwa chini ya Angelina Mabula, kisha Jelly Silaa na wote hawakufanikisha utatuzi, hivyo akamwomba Ndejembi ajitahidi kuumaliza ili wananchi wapate haki yao.

Kwa mujibu wa Mdee, Shirika la DDC lilichukua ardhi hiyo mwaka 1980 wakati eneo hilo bado ni kijiji, lakini halikufuata utaratibu uliotakiwa na baadaye likapatiwa hati ya umiliki.

“Walisema wanataka kufanya shughuli za kilimo na ufugaji lakini hawajawahi kulima mchicha wala kufuga hata kuku, badala yake wanawasumbua wananchi zaidi ya 250,000 walioko kwenye mitaa hiyo, wakiwemo wa asili na waliouziwa maeneo,” amesema Mdee.

Ametaja matangazo ya Serikali la Februari 10, 2024 lililotoka kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kinondoni kuhusu kuuza viwanja katika eneo hilo, na tangazo la Mei 9, 2025 lililotolewa na mtu aliyemtaja kwa jina la Shedrack Maxmiliani lenye maudhui kama hayo.

Mbunge wa Kibamba (CCM), Issa Mtemvu, ametoa taarifa kwa Mdee akisema kumekuwa na hatua nzuri za utatuzi wa mgogoro huo na kwamba viwanja vinavyotangazwa ni vile ambavyo bado viko wazi, huku kila kimoja kikitajwa kuuzwa kwa Sh15,000 kwa mita ya mraba, wakati waliojenga wanauziwa kwa Sh3,000 kwa mita ya mraba.

Hata hivyo, taarifa hiyo ilikataliwa na Mdee aliyewahi kuwa Mbunge wa Kawe, akisema jambo analolizungumza ana ushahidi nalo kwani amekuwa mbunge kwa miaka 20, hivyo hawezi kusema maneno ya uongo bila vielelezo.

Kwa upande wake, Mbunge wa Korogwe Vijijini (CCM), Timotheo Mzava, ameitaka Serikali kuja na mkakati wa kupunguza gharama za kodi kwa nyumba za NHC, kwa kuwa sera ya nyumba si rafiki.

Mzava amesema gharama za manunuzi au kodi ya pango kwa nyumba za Shirika la Nyumba hazina tofauti na zile za mtaani, hivyo inakuwa ngumu kuona unafuu. Amesema kuwa kinachosababisha hali hiyo ni sera ya manunuzi ya Serikali.

Naye Mbunge wa Mvumi, Livingston Lusinde, amesema ndani ya Wizara ya Ardhi kuna watu wanaojiita madalali ambao bado wanawaumiza wananchi, akisema mbinu nyingine inayoonekana kukithiri ni kufunguliwa kesi kwa watu wasiokuwa wahusika, halafu hukumu ikitolewa wanagawana ardhi husika au fedha kutoka kwenye mauzo.

“Lakini kuna watumishi wanakuwa chanzo cha haya yote, tunaomba waziri umulike, maana watu wa chini wanaumizwa sana, na kingine pimeni ardhi ili muitenge kwa matumizi hasa vijijini, mkawatambue wafugaji,” amesema Lusinde.

Related Posts