Mwanza. Wizara ya Afya kwa kushirikiana na taasisi ya Baylor Tanzania imepanga kuwapima jumla ya watoto 150,000 wenye umri chini ya miaka mitano viashiria vya selimundu mkoani Mwanza ili kuwagundua mapema na kuwaanzishia matibabu na chanjo, kwa lengo la kukabiliana na ugonjwa huo uliokuwa tishio mkoani humo.
Upimaji huo utafanyika kwa muda wa miaka mitatu kuanzia Juni, 2025 hadi 2027 kupitia mradi wa kupambana na ugonjwa huo (SCALE Care).
Upimaji huo utahusisha watoto katika wilaya za Ukerewe, Nyamagana, Ilemela, Misungwi, Sengerema na Magu kwa kushirikiana na Hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando na Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (Muhas).

Akizungumza baada ya kuuzindua mradi huo leo Mei 29, 2025, Katibu Tawala Mkoa wa Mwanza, Elikana Balandya amesema selimundu imekuwa tatizo sugu katika mikoa ya kanda ya ziwa, kuanzisha mradi huo unaolenga kubadilisha hali kwa kuingiza huduma muhimu kama upimaji, matibabu na huduma kinga ni hatua kubwa ya kupambana na ugonjwa huo.
Amesema watoto 11,000 hadi 14,000 wanazaliwa kila mwaka nchini Tanzania wakiwa na ugonjwa huo, kati ya hao watoto 1,730 wanatoka Mkoa wa Mwanza, idadi ambayo ni kubwa kuliko mikoa yote nchini, jambo ambalo limechochea wizara na Ofisi ya Rais Tamisemi kuanza utekelezaji wa mradi huo mkoani humo.
“Kupitia mradi huu tusiache mtoto yeyote katika mkoa wetu bila kufikiwa na huduma hizi, hivyo, nazitaka mamlaka za Serikali za mitaa ambazo ni halmashauri zitakazofikiwa na mradi huu kutoa ushirikiano, ili huduma zitolewe kikamilifu kuhakikisha hakuna mtot atakayeachwa na kupoteza maisha,” amesema Balandya.

Katibu Tawala Mkoa wa Mwanza, Elikana Balandya akizungumza katika hafla ya kufungua mradi wa kupambana na Selimundu ‘Sickle Cell Access and Life Long Care (SCALE Care). Mradi huo wa miaka mitatu (2025-2027) utatekelezwa katika wilaya za Ilemela, Nyamagana, Sengerema, Ukerewe, Misungwi na Magu ukilenga kupima watoto 150,000 wenye umri chini ya miaka mitano na kuwaanzishia huduma za matibabu. Picha na Damian Masyenene
Katibu huyo amewataka watendaji wa afya kuhakikisha utekelezaji wa mradi huo kuwa sehemu ya majukumu ya kazi yao ya kila siku, ili utakapofika mwisho matokeo yake yaendelee kwa miaka ijayo kwani shughuli ya kupambana na selimundu ni jumuishi.
Naye, mtaalamu wa mradi wa SCALE Care, Dk Lulu Chilande amesema takriban watoto 500,000 duniani huzaliwa wakiwa na selimundu huku robo tatu sawa na asilimia 75 wakitoka kusini mwa Jangwa la Sahara Tanzania ikiwemo.
Dk Lulu ambaye ni daktari bobevu wa magonjwa ya damu na saratani kwa watoto, amesema kupitia mradi huo watafanya upimaji wa selimundu kwa watoto wachanga ili kugundulika mapema na kuwaanzishia matibabu, kwani kufanya hivyo kutasaidia kwa asilimia kubwa kupunguza tatizo hilo.
“Tutafanya upimaji kwenye ngazi ya jamii na vituo vya afya tukishirikisha jamii kupitia uelimishaji, kufanya vipimo, kushirikiana katika huduma za chanjo zinazoendelea, kuwawezesha na kuwajengea uwezo watoa huduma katika vituo vya afya ili watoe huduma kwa ufanisi na kwa ufasaha.”
Mratibu wa mradi huo, Dk Eunice Ketang’enyi amesema wanategemea matokeo mazuri kwani watatumia mfumo unaotumika kwa sasa katika kuwabaini watoto wanaozaliwa na Virusi Vya Ukimwi (VVU) na namna wanavyohudumiwa kupata dawa za kufubaza makali (ARVs).

“Tutafuata hatua zilezile za HIV kwa watoto kwa sababu zimekuwa na mafanikio kwao. Tunataka kufikia watoto 150,000 katika upimaji kwa sababu ukitaka kupata mtoto mmoja mwenye selimundu lazima upime watoto 100, hivyo kwa idadi hiyo ya watoto 150,000 tunategemea huenda tukagundua wagonjwa 15,000 wenye ugonjwa huo,” amesema Dk Eunice.
Mganga Mkuu wa Wilaya ya Ukerewe, Dk Charles Mkombe amesema, “watu wengi wana imani potofu kuhusu ugonjwa huo kuwa labda mtu amerogwa hivyo wanaanzia kwenye mitishamba. Naamini sasa mradi huu unakwenda kufanya mabadiliko na kuongeza uelewa kwa wananchi kuhusu ugonjwa wa selimundu.”