Mradi wa maji Sh1 bilioni kuwaokoa wananchi 12,619 kusaka maji usiku na mchana

Nachingwea. Wananchi wa Tarafa ya Naipanga, wameondokana na adha ya kutembea umbali mrefu kutafuta huduma ya maji baada ya Wakala wa maji na usafi wa mazingira vijijini (Ruwasa) kuwajengea tanki la maji lenye ujazo wa lita 300,000.

Wananchi hao walikuwa wanatembea umbali wa kilomita 15 kutafuta maji huku ikiwachukua siku mbili hadi tatu kupata maji hayo.

Wakizungumza leo Alhamisi Mei 29,2025  baada ya kuwekwa  jiwe la msingi, Mkazi  wa Kata ya Rahaleo Tarafa ya Naipanga, Suzan Alex amesema awali walikuwa wanatoka alfajiri kwenda kutafuta maji ambapo umbali wake wanatembea kilomita 15 hadi kufika kwenye visima ambavyo maji yake yalikuwa sio salama.

“Tulikuwa tunatembea umbali mrefu sana kutafuta maji, hukohuko mnakaa foleni siku mbili hadi tatu ndio urudi nyumbani, lakini kumalizika kwa mradi huu tunashukuru sana hata ndoa zetu zitakuwa na amani” Alex.

Onesmo Bakari amesema kuwa ndoa nyingi zilivunjika kwakuwa wanawake wao wakienda kuchota maji wanachelewa kurudi na kuonekana kama wamekwenda kufanya uhuni.

“Tunamshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuweza kuleta fedha kwaajili ya kutujengea kisima cha maji chenye ujazo wa lita 300,000 kwani tumeshaondokana na adha ya maji, na ndoa zitaimarika,” amesema Bakari.

Kwa upande wake Meneja  wa Wakala wa maji na usafi wa Mazingira Vijijini (Ruwasa) Mhandisi Ramadhani Musiba amesema  kuwa mradi huo unatekelezwa na Mhandisi Broadways Engineering Co Ltd chini ya usimamizi wa Ruwasa ambapo amesema  kuwa hadi kukamilika kwake umegharimu zaidi ya Sh1 bilioni na utahudumia Kata nne zenye vijiji 11 na wakazi 12,619.

“Mradi huu umegharimu kiasi cha Sh1 bilioni na utahudumia wakazi 12,619 ambao wanatoka kwenye kata nne zenye vijiji 11,” amesema Mhandisi Musiba.

Amesema pia wananchi hao watatakiwa kulipa Sh50 kwa ndoo moja ya lita 20.

Naye mkimbiza mwenge kitaifa, Ismail Ally Ussi amewataka wananchi hao kutunza miundombinu ili kuweza kutumia kwa muda mrefu.

“Niwaombe wananchi wa Naipanga kutunza miundombinu ya maji ili kuweza kukaa kwa muda mrefu, Rais Samia malengo yake ni kumtua mama ndoo kichwani niwaombe sana kutunza miundombinu hiyo,” amesema Ussi.

Mwenge wa Uhuru umekimbizwa katika Wilaya ya Nachingwea ambapo miradi saba yenye thamani ya Sh2 bilioni imetembelewa, kuwekewa mawe ya msingi na kuzinduliwa.

Related Posts