Hai. Mwenyekiti wa Kanda ya Pwani wa Chadema, Boniphace Jacob, maarufu Boni Yai amesema kazi iliyofanywa na Mwenyekiti mstaafu wa chama hicho, Freeman Mbowe kwa miaka 21 wanaithamini na kumtaka asikae pembeni kwa kuwa bado wanamuhitaji na wataendelea kumlinda.
Bon Yai ameyasema hayo leo Alhamisi Mei 29, 2025 wakati akizungumza na wananchi kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika viwanja vya Half London vilivyopo Bomang’ombe, Wilaya ya Hai ikiwa ni mwendelezo wa kampeni ya kudai mabadiliko ya sheria za uchaguzi kabla ya kufanyika kwa uchaguzi mkuu mwaka huu, kupitia kampeni yao maarufu ya ‘No reforms, no election’.
Amesema mchango wa Mbowe kwenye chama hicho ni mkubwa na wana kila sababu ya kujivunia utumishi wake hivyo hapaswi kuwa mnyonge.
“Sisi wazee wetu wakishashuka wanakaa pembeni wamemaliza dhumuni lao, wajibu wetu kama chama ni kuwatumia kama washauri, wasuluhishi kwenye migogoro ya chama lakini la tatu ni wajibu wetu kuwalinda na kuwaheshimu wazee waliomaliza utumishi wao”.
Ameongeza kuwa, “kwa kusema hivyo tuna kila sababu ya kujivunia utumishi wa Freeman Mbowe ndani ya chama chetu na tunamwambia asiwe mnyonge sisi vijana wake tuko naye kazi yake tunaithamini na asikae pembeni, bado tunamuhitaji.”
Amesema “Mimi namuombea Mwenyezi Mungu pepo ambalo wanalitengeneza la kutufarakanisha na mzee wetu, lishindwe katika jina la Yesu…. leo kumnyemelea mzee yule ambaye yuko bize na maisha yake binafsi ya biashara, kumuhusisha husisha na mambo ya kijinga pepo hilo nalo lishindwe katika jina la Yesu”
“Pepo la kumtenganisha mwenyekiti wetu Freeman na chama chake anachokipenda, alichokipigania na kuumia kwa chama hiki na pepo hilo lishindwe kwa jina la Yesu,”amesema.
Katika hatua nyingine amesema kwa sasa wana kazi kubwa ya kuwalinda makamanda wao wapya ambao ni Mwenyekiti wa sasa wa chama hicho Tundu Lissu na Makamu wake bara, John Heche kwa sababu ndio wamebeba dhumuni la chama hicho.
“Nimesimama hapa nikiashiria kwamba sisi Chadema ni chama kimoja na wanaosubiri ife ni sawa na fisi anayefuatilia mkono wa binadamu akijua utaanguka.”
Amesema, “Kusimama mimi hapa ni kuonyesha Chadema haifi na haitokufa, mambo yetu ya ndani tuliyamaliza tumesimama kama chama kwa sababu tofauti, maudhi machache na sisi wenyewe tofauti zetu si za muhimu kama nchi yetu ya Tanzania ama shida za Watanzania. Ukiziacha kuzitanguliza mbele na kutanguliza matumbo yetu…hata nyie mtatuombea tulaaniwe, kweli au si kweli ..nyie mngetamani siku moja tuamke tunagawana gari za chama au tunauza jengo la Mikocheni leo tunapeana hela kila mtu aende nyumbani,”ameuliza Bon Yai.
“Mmeanzisha chama kimeenea kwenye mioyo yenu mmekielewa, mmekithamini, mnakipenda, na ndiyo maana pamoja na Hai tunafanyaga mikutano uwanjani kule barabarani leo tuko hapa mita 500, mmetoka kukifuata chama chenu kwa sababu mnakiamini.”
Akizungumza katika mkutano huo wa hadhara, Makamu Mwenyekiti wa Chadema , John Heche amesema endapo chama hicho kitashika dola, kitahakikisha kila Mtanzania mwenye umri wa miaka 60 anapewa mafao ya kiinua mgongo na Serikali.
Amesema kila Mtanzania katika nchi hii amelitumikia Taifa kwa namna yake, hivyo anao wajibu wa kupewa mafao yake na inawezekana.
“Fundi ujenzi ndiye anayetujengea nyumba tunakaa, inakuwaje watumishi wa Serikali ndio walipwe tu mshahara kwa miaka 60 wewe uliyejenga nyumba wakati ulilitumikia Taifa usipate chochote, sisi tumesema kila mtu atalipwa mafao kwa sababu amelitumikia Taifa, tunataka tubadilishe nchi hii, inawezekana.”
Pamoja na mambo mengine, Heche amesema Tanzania sio nchi ya watu waliofikisha umri wa miaka 60 kupewa Tasaf (mpango wa kunusuru kaya Maskini) kutokana na rasilimali zilizopo nchini.
“Tuna uwezo wa kuibadilisha nchi hii, hii sio nchi ya watu kupewa Tasaf Sh30,000, akina mama wenye miaka 60 wanaenda kuchimba mitaro ya barabara na kulima,”amesema Heche.
Mwenyekiti wa Baraza la wanawake Taifa (Bawacha), Sharifa Suleiman amesema wataendelea kuhubiri uchaguzi wa huru na haki ili kuleta maendeleo katika Taifa.
“Tunataka uchaguzi wa huru na haki ili kusudi tuweze kuwaletea maendeleo endelevu ya Watanzania na si vinginevyo, kina mama wenzangu tunapozungumzia masuala ya changamoto zozote zinazohusu nchi hii basi tunaathirika moja kwa moja,”amesema Sharifa