Dar es Salaam. Chama cha ACT Wazalendo kimeitaka Ofisi ya Spika wa Bunge la Tanzania kuwajibika kwa kuwaita na kuwahoji wabunge katika Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge, kufuatia kauli zilizotolewa na baadhi yao kutozingatia maadili ya uongozi, utu wala heshima ya chombo hicho muhimu cha kutunga sheria.
Kwa mujibu wa chama hicho, baadhi ya wabunge walitumia lugha ya kashfa na kejeli, huku wengine wakipongeza hatua zilizochukuliwa na vyombo vya ulinzi dhidi ya wanaharakati wa Kenya, wakisema “wamepewa walichostahili.”
Kauli hiyo imekuja baada ya Mei 28,2025 Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson kuwakanya wabunge wanapochangia bungeni wasivunje kanuni, Katiba na Sheria licha ya kuwepo kwa uhuru wa kujieleza.
Spika alitoa kauli hiyo kutokana na michango ya wabunge katika hotuba ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi na Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu ambapo wabunge wengi waliwashambulia waliotajwa kuwa ni wanaharakati kutoka Kenya.
Akizungumza leo Mei 29, 2025, Mwenyekiti Ngome ya Wanawake wa chama hicho, Janeth Rithe amesema kitendo kilichofanyika ni ukiukwaji wa mikataba ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.
“Tunaitaka Kamati ya Maadili ya Bunge, kupitia Ofisi ya Spika, iwafikishe mbele ya kamati wabunge wote waliotoa kauli za chuki, dharau na dhihaka dhidi ya wanaharakati waliokumbwa na mateso wakiwa nchini Tanzania. Kauli zao si tu zinadhalilisha waathirika, bali pia zinaichafua taswira ya Bunge letu kwa wananchi na kwa jumuiya ya kimataifa,”amedai Rithe.
Amedai jambo la aibu kwamba badala ya kulaani ukiukwaji wa haki za binadamu, baadhi ya wabunge walichagua kucheka na kuponda mateso ya wengine. Huu siyo utu, siyo uongozi, na siyo mfano wa kizalendo.
“Tunasisitiza kwamba, heshima ya Bunge haitatokana na majengo au vyeo, bali na tabia na kauli za wale wanaolihudumia. Tunatarajia kuona Bunge likichukua hatua za wazi, siyo kufumbia macho madhambi ya baadhi ya wabunge wake.”
Miongoni mwa waliodaiwa kunyanyaswa ni viongozi wa chama cha People’s Liberation Party (PLP) cha nchini Kenya akiwemo mwanasheria maarufu, Martha Karua na Jaji mstaafu wa Mahakama ya Juu ya Kenya, Willy Mutunga.
Viongozi hao walidaiwa kuzuiwa kwa muda mrefu katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) na baadaye kurejeshwa nchini kwao bila maelezo rasmi kutolewa.
Aidha, wanaharakati wengine kutoka Uganda na Kenya walidaiwa kukamatwa maeneo ya mipakani, kushikiliwa kwa siku kadhaa, kufanyiwa vitendo vya ukatili kisha kuondoshwa nchini huku wakiwa na majeraha.
Mmoja wa waliotajwa ni Agata Atuhaire kutoka Uganda ambaye inadaiwa alikamatwa karibu na mpaka, kuteswa akiwa kizuizini.
Wakati ACT wanatoa wito huo, Mei 19, 2025 Rais Samia Suluhu Hassan alipokuwa anazindua Sera ya Mambo ya Nje ya Nchi ya Tanzania alijibu kauli za wanaopinga kuzuiwa kwa wanaharakati hao na akaonya tabia ya wanaharakati kutoka nje ya nchi ya Tanzania kutaka kuingilia mambo ya ndani ya nchi yake.
“Tumeanza kuona mtiririko wa wanaharakati ndani ya kanda yetu hii kuanza kuvamia na kuingilia mambo yetu sasa kama kwao wamedhibitiwa, wasije wakatuharibia huku.
“Tusitoe nafasi, walishavuruga kwao. Nchi iliyobaki haijaharibiwa, watu wanaishi kwa amani na usalama ni hapa kwetu,”alisema Rais Samia Mei 19, 2025 alipokuwa anazindua Sera ya Mambo ya Nje ya Nchi ya Tanzania.
Alitumia fursa hiyo kuvitaka vyombo vya Usalama na Wizara ya Mambo ya Nje kutotoa nafasi kwa aliowaita ni waovu wa nidhamu kuja na kutaka kuingilia mambo ya ndani ya Tanzania.
Kauli hiyo iliungwa mkono na Waziri Kiongozi wa Baraza la Mawaziri la Kenya, Musalia Mudavadi ambaye alisema kuna baadhi ya wanaharakati wa nchi hiyo wanatumia vibaya uhuru uliopo nchini humo.
Wakati hayo yakiendelea Rais William Ruto wa Kenya Mei 28, 2025 aliomba radhi mataifa ya Tanzania na Uganda wakati wa ibada maalumu ya kuliombea Taifa hilo iliyofanyika Safari Park nchini humo.
“Majirani zetu Watanzania kama tumewakosea kwa namna yoyote tunaomba mtusamehe na majirani zetu Waganda, mtusamehe, vijana wetu kama kuna kitu wamekosea mtusamehe,” alisema Ruto.
Rais Ruto alieleza hayo wakati kukiwa na majibizano kwenye mitandao ya kijamii ambapo Wakenya wamekuwa wakiwatukana Watanzania na kurusha vijembe na ambapo vijana hao kutoka nchi jirani wameenda mbali zaidi kwa kuwatukana viongozi wa Tanzania.
Mchambuzi wa siasa, Buberwa Kaiza amesema wabunge hawatakiwi kutumia Bunge kama jukwaa la kutoa matusi, kejeli na kauli zisizokuwa na staha, hasa kuhusu watu wanaofika nchi kama ilivyokuwa kwa wanaharakati wa Kenya na Uganda.
“Haina maana kuwa walikuwa ni Wakenya basi hawakupaswa kuwepo nchini, kama watu hao walikuja kwa ajili ya kusikiliza kesi hakuna tatizo. Sheria hairuhusu chuki wala ubaguzi wa namna hiyo,” amesema Kaiza.
Kaiza amesema kutokana na kauli za baadhi ya wabunge kuna haja ya Spika kutumia miongozo na sheria husika ili kuwawajibisha kwani maelezo yao yanaingia kwenye kumbukumbu za Bunge na hiyo ni fedheha kwa upande wao.
Hata hivyo, amesema tabia ya baadhi ya wabunge kutoa kauli za kubeza, kutukana na hata kudhalilisha wengine ndani ya Bunge, inadhihirisha ukosefu wa uelewa na maarifa ya kutosha kuhusu misingi ya haki na utawala wa sheria.
Ametoa wito kwa wabunge kuwa mfano wa kuigwa katika kuonyesha nidhamu, heshima na utii kwa sheria badala ya kutumia jukwaa la Bunge kama mahali pa kuchafua taswira ya watu kwa malengo ya kisiasa au chuki binafsi.