Arusha. Licha ya Sheria ya Udhibiti wa Tumbaku ya mwaka 2003 kukataza uvutaji wa sigara hadharani, sheria hiyo imeendelea kukiukwa kutokana na uwepo wa watu wanaovuta sigara katika maeneo ya umma.
Mbali na uvutaji huo wa sigara hadharani uchunguzi uliofanywa na Mwananchi umebaini kuwa katika maeneo mengi hakuna mabango ya kuzuia.
Sheria hiyo imezuia matangazo ya tumbaku na bidhaa zitokanazo na tumbaku kwenye maeneo ya umma, ikiwemo vyombo vya habari, mabango na kwenye matamasha mbalimbali.
Kifungu cha 12 cha Sheria ya Udhibiti wa Bidhaa za Tumbaku kimetafsiri maeneo ya umma ni mahali ambapo inatolewa huduma ya afya, maktaba, mahali pa ibada, majengo au maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya mikutano ya kitamaduni na kijamii, shughuli za michezo au burudani.

Mengine ni sehemu za huduma ya chakula, majengo ya ofisi, vyombo vya usafiri wa anga, ardhi au maji, mabanda ya maonesho, masoko, maduka makubwa na maeneo mengine yanayotumiwa na umma.
Katika maeneo hayo sheria imekataza uvutaji wa aina yoyote ile wa bidhaa za tumbaku na kuelekeza kuwekwa bango lenye maneno yanayosomeka ‘No smoking au Hairuhusiwi kuvuta sigara’ kwa herufi kubwa.
Aidha, kifungu cha 13 cha sheria hiyo kimeruhusu uvutaji kwenye baadhi ya maeneo ikiwemo hoteli, baa, migahawa na maeneo ya burudani yanayopaswa kutenganisha vyumba au maeneo maalum ya kuvutia na kutovutia.
Aprili 30, 2024 akijibu swali la Mbunge wa Tumbe, Amour Khamis Mbarouk aliyeuliza, ni lini Serikali italeta sheria ya kuzuia uvutaji wa sigara na mazao mengine hadharani, Naibu Waziri wa Afya, Dk Godwin Mollel alisema tayari Bunge limepitisha sheria hiyo ambayo inakataza uvutaji sigara hadharani.
Alisema sheria hiyo imezuia matangazo ya tumbaku na bidhaa zitokanazo na tumbaku kwenye maeneo ya umma ikiwemo vyombo vya habari, mabango na kwenye matamasha mbalimbali.
Hatahivyo, bado sheria hiyo haifuatwi katika maeneo mbalimbali nchini, ambapo watumiaji wa sigara wanavuta maeneo ya umma na hakuna mabango ya kuzuia au kuonya kutovuta sigara.
Mkazi wa Butimba jijini Mwanza, Kwezi Sudi anasema stendi ya daladala ya Igombe ni miongoni mwa maeneo jijini hapo ambapo sigara zinavutwa ovyo na hakuna bango linalokataza uvutaji sigara.
“Baadhi ya makondakta na wapiga debe wanavuta hadharani huku wakiendelea kupakia abiria kwenye magari, pamoja na kuwa moshi huo unakera sana hasa kwa sisi ambao hatuvuti lakini nasikia pia unaathari kwenye afya zetu,” anasema Sudi.
Mkazi wa Nyegezi jijini Mwanza, Benard Josephat anahauri kuwa kama lilivyo bango la kuzuia watu kuvuta sigara lililowekwa stendi kuu ya mabasi Nyegezi, basi mabango kama hayo yawekwe hata stendi za daladala jijini humo kuwaepusha abiria na watumiaji wengine na kero ya moshi pamoja na athari za kiafya.
Mama lishe wa eneo la soko kuu la Arusha, Neema Maliki anaasema licha ya kutokutambua kuhusu uwepo wa sheria ila yeye ni miongoni mwa watu wanaogombana na wavuta sigara wanaovuta katika eneo lake la biashara.
“Mimi binafsi kila mara hapa nagombana na watu wanaovuta sigara karibu na eneo langu la biashara kwani mimi binafsi inaniumiza kifua…tunaomba Serikali itazame suala hili kwa kutoa elimu kwa jamii ili tusije kupata maradhi kutokana na moshi wa sigara,”anasema
Mkazi wa Wilaya ya Moshi, James Jerome anasema imekuwa ni tatizo kubwa kwa baadhi ya watu kuwa na desturi ya kuvuta sigara kwenye mkusanyiko mkubwa wa watu kitu ambacho wasiovuta hawakifurahii kwa sababu ni kero kwao.
“Uvutaji wa sigara holela ni changamoto huku mtaani unaweza kwenda zako dukani unakuta mtu anapuliza moshi wa sigara utadhani yupo mwenyewe, hii imekuwa ni kero kubwa kwetu na wakati mwingine ule moshi unatuliza na kujisikia vibaya,” anaasema Jerome
Mwenyekiti wa Kamati ya Maendeleo ya Jamii Jiji la Arusha, Isaya Doita anasema ni muhimu viongozi kwa kushirikiana na wataalam wa afya kuelimisha jamii kuhusu madhara ya moshi wa tumbaku hasa katika maeneo ya kijamii (masoko na stendi) pamoja na maeneo ya starehe ambako wavutaji na wasiovuta hukutana.
Doita anasema wanafahamu kuna sheria inayozuia uvutaji wa sigara hadharani hivyo ni muhimu jambo hilo likazingatiwa, ili kuepusha madhara kwa watu wengine kwani inatishia afya ya vizazi vijavyo.
“Jiji hatuna sheria ndogo kuhusu suala hilo, naamini ni wakati sasa wa kujadiliana na kuweka sheria ndogo kwa kuwashirikisha wadau ili mtu ajue akikutwa eneo la umma anavuta sigara anatozwa faini,
“Pia hakuna elimu inayotolewa katika maeneo jumuishi mfano sasa hivi ukienda baa, kwenye masoko au stendi unakuta watu wanavuta shisha na sigara. Ni wakati sasa vyombo vya dola vikasimamia maelekezo ya sheria wakati sisi tukiendelea kutoa elimu kwa kushirikiana na wadau,” anasema Doita.
Athari za uvutaji wa sigara
Katika ripoti ya Shirika la Afya Duniani kuhusu magonjwa yasiyoambukiza ya mwaka 2023, Tanzania imetajwa kufanya vizuri katika ukusanyaji wa kodi za sigara, lakini ilionekana kufanya vibaya katika kudhibiti matumizi ya tumbaku hadharani.

Kwa mujibu wa WHO inakadiriwa kuna kemikali zipatazo 7,000 katika moshi wa sigara ambapo 250 kati ya hizo ni sumu na 70 zinasababisha saratani.
Pafu moja la sigara limetajwa kuwa na mamia ya kemikali, ambapo moshi wake huathiri karibu kila kiungo mwilini kuanzia seli hadi mfumo wa kulinda mwili.
Pindi moshi unapovutwa, mifumo ya kusafisha makohozi na uchafu kutoka kwenye mapafu hudhoofishwa, hivyo kuruhusu sumu iliyomo kwenye tumbaku kuingia kwenye mapafu kwa urahisi.
WHO inasema kila mwaka watu milioni nane hufariki dunia kutokana na tumbaku, huku mamilioni wengine wakipata magonjwa sugu kama saratani, kifua kikuu, pumu au magonjwa sugu ya njia ya hewa yanayosababishwa na matumizi ya tumbaku.
Shirika hilo linasema matumizi ya tumbaku hayajaacha watoto salama kwani zaidi ya watoto 60,000 wenye umri wa chini ya miaka 5 hufariki dunia kutokana na kuvuta moshi kutoka kwa mvutaji wa kwanza, wanaoishi hadi kufikia utu uzima wako kwenye nafasi kubwa zaidi ya kupata magonjwa sugu ya njia ya hewa.
Mtaalam wa afya kutoka Hospitali ya Jafarry Charitable services, Teddy Khumbelle anasema kumekuwepo na madhara makubwa kwa wanaovuta sigara hasa kwa upande wa mwanamke na mwanaume lakini madhara makubwa zaidi anayapata anayevuta moshi kutoka kwa mtu anayevuta sigara.
“Moshi wa sigara una madhara makubwa kwa mtu ambaye sio mvutaji na hii imeonekana kwenye tafiti mbalimbali zilizofanyika hapa nchini,” anasema Khumbelle.
Kuhusu athari za uvutaji wa sigara kwa wanaume, anasema huathiri mbegu za kiume na matokeo yake watoto huzaliwa na tatizo la saratani.
Kwa upande wa wanawake, anasema kuna athari kubwa ya kupata saratani ya kizazi na wakati mwingine kusababisha mimba kuharibika au kuzaa mtoto aliyekufa.

Meneja Programu wa Shirika la Blue Cross Society of Tanzania linalojishughulisha na utoaji wa elimu juu ya madhara ya matumizi ya dawa za kulevya, ukatili wa kijinsia pamoja na kuwezesha wanawake na vijana, Gloria Vincent anasema wavutaji hupuuza na kuvuta sigara ovyo bila kujali kuna watoto au watu wengine wasiotumia.
Anasema licha ya kuwa na programu maalumu ya kusaidia jamii kuongeza uelewa kuhusu athari za matumizi ya dawa za kulevya, uvutaji sigara na ukatili wa kijinsia kwa kushirikiana na Serikali, viongozi wa kidini na kimila lakini wanakutana na changamoto ya jamii kutokuwa tayari kukemea masuala ya pombe, dawa za kulevya na uvutaji sigara holela.
“Wengi wanapuuzia hili jambo na imekuwa kawaida kumuona mtu hata barabarani akitembea huku anavuta sigara bila kujali wapo watoto au watu wengine ambao hawatumii,” anasema.
Imeandikwa na Janeth Mushi, Janeth Joseph na Saada Amir.