Madhara ya tumbaku kwa wanaoishi na kisukari

Dar es Salaam. Kwa mtu anayeishi na kisukari, kila uamuzi kuhusu mtindo wa maisha una uzito wa kiafya. Mojawapo ya maeneo ya uamuzi  ni matumizi ya tumbaku.

Huenda wengine wakadhani kuwa tumbaku inaathiri mapafu tu, lakini ukweli ni kwamba kwa mtu mwenye kisukari, tumbaku huathiri kila kona ya mwili, kutoka kwenye mishipa ya damu, hadi figo, moyo na hata mfumo wa fahamu.

Mtu mwenye kisukari anayetumia tumbaku anaweza kuongeza mzigo mwingine mwilini; mzigo wenye matokeo mabaya hasa katika udhibiti sukari.

Wataalamu wa afya wanasema kwamba kemikali zilizopo kwenye tumbaku huathiri kiasi kikubwa uwezo wa mwili kutumia insulini, hali inayosababisha sukari kushindwa kudhibitiwa vizuri.

Hii ina maana kwamba hata kama unatumia dawa kwa wakati na kula vyema, matumizi ya tumbaku yanaweza kuvuruga juhudi zote za kudhibiti viwango vya sukari.

 Utafiti uliochapishwa na jarida la Diabetes Care,  unaonesha kuwa matumizi ya tumbaku huongeza hatari ya matatizo ya moyo kwa wagonjwa wa kisukari kwa zaidi ya asilimia 30.

Mbali na hilo, tumbaku hudhoofisha mishipa ya damu na kupunguza uwezo wa damu kufika kwenye maeneo muhimu ya mwili.

Hali hii huchangia vidonda kutopona haraka, miguu kuvimba au hata hatari ya kukatwa viungo.

Watu wenye kisukari ambao pia wana tatizo shinikizo la juu la damu, tumbaku huongeza athari zaidi, hali inayoongeza zaidi hatari ya kupata kiharusi au mshtuko wa moyo.

Kwa hivyo, mtu mwenye kisukari na anatumia tumbaku anakuwa kwenye hatari kubwa zaidi ya kupata matatizo mengine ya kiafya.

Kwa watu wasiokuwa kisukari, utafiti uliochapishwa na Shirika la Afya Duniani (WHO)  mwaka 2023 kuhusiana na uhusiano kati ya matumizi ya tumbaku na kisukari,  unaonesha kuwa uvutaji wa tumbaku au sigara huongeza hatari ya mtu kupata kisukari cha aina ya pili.

Kwa walio tayari na kisukari, tumbaku huongeza uwezekano wa kupata matatizo ya moyo kwa asilimia 30 hadi 40 zaidi ya wale wasiovuta.

Tumbaku pia huathiri mzunguko wa damu na huchangia kupungua kwa mzunguko wa hewa safi katika mapafu, hali inayoweza kusababisha miguu kukosa damu ya kutosha na hata kusababisha kukatwa kwa viungo.

Kwa wanawake wanaoishi na kisukari na wanatumia tumbaku wapo katika hatari kubwa zaidi ya kupata kiharusi au matatizo ya uzazi. Kwa wanaume yanaweza kuathiri nguvu za kiume, hasa endapo ugonjwa wa kisukari haujadhibitiwa vyema.

Uamuzi wa kuacha kutumia tumbaku huleta mabadiliko makubwa na chanya kama vile kupunguza viwango vya juu vya shinikizo la damu, mzunguko wa damu kuimarika, na  hatari ya kupata magonjwa ya moyo hupungua.

Related Posts