Diwani mbaroni ‘utekaji’ wa mbunge, DCI aeleza mazito

Moshi/Nairobi. Sarakasi ya kutekwa kwa mbunge mara baada ya kutoka ibadani kisha kutelekezwa shambani akiwa na majeraha imeendelea kuwa kitendawili baada ya diwani kutiwa mbaroni kwa sakata hilo.

Kukamatwa kwa diwani huyo kunafanya idadi ya watu ambao wameshatiwa mbaroni kufikia 10 huku Polisi wakiendelea na utaratibu wa kumfikia mbunge huyo anayedai kulazwa katika Hospitali ya Karen iliyopo Jijini Nairobi.

Tukio la utekaji Mbunge wa Juja, George Koimburi ambalo Polisi wanadai lilitengenezwa, imeshika kasi baada ya Polisi nchini Kenya kumtia mbaroni Diwani wa Kanyenya-Ini, Grace Nduta Wairimu.

Taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), jana imesema uchunguzi unaonyesha wazi Diwani huyo alikuwa na mbunge huyo usiku kucha katika baa ya Ellis Bar and Restaurant siku ambayo mbunge alidai kutekwa.

Diwani wa Kanyenya-Ini, Grace Wairimu

“Taarifa zinazosambaa katika mitandao ya kijamii zikidai mwakilishi wa Kata ya Kanyenya –Ini ametekwa siyo kweli kwani amekamatwa leo Mei 29, 2025 kutokana na uchunguzi unaoendelea wa tukio la kutengenezwa la kutekwa kwa Koimburi,” imeeleza tarifa hiyo.

Taarifa hiyo iliyosainiwa na John Marete kwa niaba ya DCI imeongeza kusema:-“Imethibitishwa kuwa licha ya madai yake kuwa alikuwa Kangema katika ibada na baadaAYe mkutano wa hadhara, ushahidi unaonyesha alikuwa na Koimburi.”

Kulingana na taarifa hiyo, Polisi wanadai Mei 25, 2025 siku mbunge huyo baada ya kudai kutekwa, diwani huyo alikuwa na mbunge huyo katika Baa ya Ellis Bar and Restaurant iliyopo Kiganjo, Gatundu Kusini na walikuwa wote usiku kucha.

Tayari Polisi nchini Kenya (NPS) imeshaweka wazi kuwa tukio la kutekwa kwa Mbunge wa Juja, George Koimburi, lilikuwa ni ‘sinema ya kutengenezwa’ na mbunge huyo na washirika wake na tayari magari yaliyohusika yamekamatwa.

Taarifa iliyotolewa Mei 28, 2025 na Inspekta Jenerali wa NPS, Douglas Kanja Kirocho, imesema watu watatu zaidi ambao walishiriki mwanzo mwisho katika kupanga na kutekeleza tukio hilo wamekamatwa na kuhojiwa kikamilifu.

Kulingana na taarifa hiyo, IGP Kirocho amewataja waliokamatwa kuwa ni pamoja na mwenyekiti wa Juja CDF Peter Kiratu na wengine Cyrus Muhia na Karanja Gatana na kwamba wameeleza mchezo mzima ulivyopangwa na kutekelezwa.

Katika maelezo hayo, Kiratu anadaiwa kueleza kuwa Mei 25,2025, alihudhuria ibada katika Kanisa la Full Gospel huko Mugitha akiwa na mbunge na wakati wanaondoka, ilikuja gari aina ya Subaru Forester na kumchukua mbunge huyo.

Mbunge wa Juja, George Koimburi akiendelea na matibabu.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Kiratu anadaiwa kutaja nambari za gari ambayo baada ya kufika katika lango kuu la Kanisa, watu wawili walishuka na kumuingiza kwa nguvu kwenye gari mbunge huyo.

Ameeleza kuwa alitoa taarifa kituo cha Polisi cha Mugutha na siku iliyofuata na alipokea simu kutoka kwa mbunge akimjulisha kuwa ametupwa katika shamba la kahawa ambapo alikwenda eneo hilo na walimchukua na kumpeleka hospitali.

Kwa upande wake, Muhia ambaye anadaiwa kuwa mshirika wa karibu wa mbunge huyo, anadaiwa kueleza Polisi katika maelezo yake kuwa Mei 24, 2025, alipokea simu kutoka kwa Kiratu akiomba kutumia gari lake ina ya Subaru.

Muhia amewaeleza polisi kuwa sababu ya kutumia gari hilo ni kwamba alitaka kulitumia kwa ajili ya kusafirisha watu zaidi wa usalama kwa ajili ya mbunge, wakati wa ibada katika kanisa lililopo Mugutha, naye alikubali ombi hilo.

Simulizi hiyo inaeleza kuwa Kiratu alimwagiza kwenda nyumbani kwake ambapo alikutana na Gatana akiendesha gari ya Kiratu aina ya Honda CRV yenye namba zinazofanana na Subaru akiwa na watu watatu asiowafahamu.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo ya IGP, wote pamoja walielekea kanisani kwa ajili ya kutazama na kuzoea njia watakayopita kabla ya kurudi nyumbani hapo.

Baadaye Kiratu alimpigia simu na kumwagiza kuiendesha Subaru Forester ikiwa na watu wawili kuelekea kanisani na baada ya kufika, watu hao wawili walishuka haraka na ndipo alisikia kelele za mbunge wakati akiingizwa kwenye gari.

Baada ya kufanya hivyo, waliondoka kuelekea Jakaranda Coffee Research kupitia Barabara ya Kambogo ambapo mbunge anadaiwa kuwapa amri ya kusimama jirani na gari ile aina ya Honda CRV namba KBP 096W ambayo ni mali ya Kiratu.

Mahia aliachwa hapo na akiwa na watu wawili waliomuonya asije kutoa taarifa yoyote kwa Polisi. Polisi wamefanikiwa kuyapata magari hayo mawili ambayo ni Honda CRV mali ya Kiratu na Subaru mali ya Mahia.

Aliyemtupa mbunge afunguka

IGP ameeleza kuwa Karanja ametiwa nguvuni na Polisi na amekiri kuwa yeye ndiye aliyekwenda kumwacha mbunge huyo katika hoteli moja ambako walipata vinywaji pamoja na kupata malazi hapo pamoja na ‘watekaji’ wale wawili.

Mtuhumiwa huyo amewaeleza polisi kuwa Mei 26, 2025, akiwa anatumia gari la Kiratu, alimchukua mbunge kutoka katika hoteli hiyo na kumpeleka hadi eneo ambalo mbunge baadaye alieleza kuwa ndipo alipotupwa na watekaji wake.

“Kabla ya kutoka kwenye gari, alimsaidia mbunge huyo kurarua nguo zake kama njia ya kutengeneza ushahidi wa uwongo wa kuteswa na ‘watekaji’ wake.

IGP amewaomba umma wa wakenya kuendelea kutoa ushirikiano kwa NPS zitakazosaidi katika uchunguzi wa suala hilo wakati Jeshi hilo likiendelea na jitihada za kumfikia Mbunge huyo ili naye aweze kuhojiwa kuhusiana na tukio hilo.

Taarifa za kutekwa zilivyosambaa

Mbunge huyo ambaye ni mshirika wa karibu wa aliyekuwa Makamu wa Rais wa Kenya, Rigathi Gachagua, alidaiwa kutekwa mara ibada ilipomalizika katika kanisa la Full Gospel lililopo Mugutha na alipopatikana alipelekwa hospitali ya Karen.

Tukio la kutekwa nyara kwa mbunge huyo lilianza kusambaa katika mitandao ya kijamii muda mfupi tu baada ya kutekwa ambapo video iliyosambaa mitandaoni ilionyesha gari hilo likiondoka kwa mwendo kasi kutoka nje ya kanisa hilo.

Baada ya tukio hilo, mke wa mbunge huyo, Ann Koimburi alinukuliwa akisema watu waliomteka mumewe walijifanya kama sehemu ya waumini na ndipo baadaye walimchukua kwa nguvu na kumwingiza kwenye gari bila kujitambulisha.

“Tulikuwa ndio tumetoka tu kanisani na ni utaratibu wa kawaida kwa mheshimiwa (mumewe) kusalimiana na watu, lakini ghafla watu wawili walimgeuka na kumlazimisha kuingia kwenye gari na kuondoka naye kwa mwendo wa kasi,”alidai.

Seneta wa Kiambu, Karungo wa Thang’wa alinukuliwa akidai kuwa watu wanaoaminika kuwa maofisa wa usalama ndio waliomteka nyara mbunge huyo akidai huo ulikuwa mpango wa kumkamata uliokuwa umepangwa wiki iliyopita.

Kulingana na taarifa hizo, dereva wa pikipiki maarufu kama bodaboda ndiye aliyembaini mbunge huyo na katika mahojiano ya awali amelalamika kupigwa na watekaji hao na polisi wamejiweka kando na tukio hilo wakisema wanachunguza.

Taarifa zilizomkariri Ofisa wa Polisi ambaye hakutaka kutajwa kwa kuwa si msemaji, alisema polisi hivi sasa wanachunguza ni namna gani wasamaria wema waliompata mbunge huyo katika shamba hilo, walitambua kuwa yupo hapo.

“Simu yake ya kiganjani ilikuwa haipatikani tangu Ijumaa Mei 23,2025 wakati polisi walipotaka kumkamata na operesheni hiyo ilisitishwa. Polisi walijaribu kumakamata alipokuwa anaondoka Juja alitoroka na Bodaboda,” ameeleza.

Hata hivyo, kulingana na taarifa hiyo, dereva wake alikamatwa na kupelekwa makao makuu ya Ofisi ya Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) na alipohojiwa amesema bosi wake ndiye alimwambia amshushe katikati ya barabara.

Hii ni baada ya kubaini kuwa alikuwa akifuatiliwa na polisi kwa lengo la kumkamata, ambapo alishuka haraka na kupanda bodaboda na tangu siku hiyo simu zake zilikuwa hazipatikani hadi polisi walipoona taarifa kuwa ametekwa.

Kwa mujibu wa vyanzo mbalimbali, polisi walifika eneo ambalo inadaiwa utekaji ulifanyika pamoja na eneo ambalo alipatikana ametupwa ambapo maelezo ya mashuhuda mbalimbali yalirekodiwa na Polisi na hakuonyeshi kulikuwa na purukushani.

Related Posts