Arusha/Moshi. Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimewataka Watanzania kuendeleza mapambano ya kudai Katiba Mpya na kuondolewa kwa kasoro zote zinazofanya chaguzi zisiwe huru na haki.
Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika amesema hayo Leo Mei 30, 2025 wakati akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika viwanja vya Mbulu Mjini, katika operesheni ya chama hicho ya ‘No reforms, no election’ inayoendelea katika kanda ya Kaskazini.
Mnyika amesema Katiba Mpya ni muhimu kwani ya sasa ndiyo inampa Rais ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) mamlaka ya kumteua Mwenyekiti na wajumbe wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC).
Vilevile, amesema katiba ya sasa ndiyo inatoa fursa kwa watendaji na viongozi wa halmashauri kuwa wasimamizi wa uchaguzi, jambo aliloeleza kuwa linachagia uchaguzi usiwe huru wala za haki, na kumpata mamlaka Rais ambaye ni mgombea wa CCM, kuteua wasimamizi wa uchaguzi.
Mnyika amewataka Watanzania wote, wakiwemo wana CCM, kufanya suala la kudai Katiba Mpya kuwa kipaumbele chao cha kwanza, badala ya changamoto zinazowakabli ikiwemo ukosefu wa ajira na masuala mengine.
Akizungumzia uchaguzi, Mnyika amesema lazima kwa sasa waache kujadili matatizo mengine na kuweka msisitizo kwenye kudai uchaguzi huru na wa haki.
“Tunataka Katiba ya sasa ibadilishwe sehemu mbalimbali, ikiwemo ibara ya 74(1), inayompa mamlaka Rais kuteua mwenyekiti, mkurugenzi wa Tume na watendaji wa Tume. Ibara hiyo irekebishwe watu waombe (nafasi) wapatikane watu huru wa kusimamia uchaguzi,” amesema Mnyika.
Katibu mkuu huyo ametaja ibara nyingine kuwa ni 74 (5) inayompa Rais mamlaka ya kuondoa Tume wakati wowote na nyingine za 74(10), 74(12) pamoja na 41 (7) inayoweka kinga ya matokeo ya urais yakishatangazwa yasihojiwe mahakamani.
“Ni lazima Watanzania tuendeleze mapambano kupata Katiba Mpya ili tupunguze madaraka ya Rais na tupeleke mamlaka kwenu (wananchi). Nafahamu mngetamani tuzungumzie matatizo yenu wananchi wa Mbulu yanayochangiwa na Serikali ya CCM.
“Najua wakulima wa mbaazi mngetamani tuzungumzie utaratibu mbovu wa masoko, kwani masoko ya sasa si huru, mfumo wa stakabadhi ghalani, wengine mngetamani tuzungumzie kukithiri kwa mageti na kutozwa ushuru wa mazao,” amesema.
“Wafanyabiashara wakubwa na wa kati, hapa mngetamani nizungumzie TRA inavyobambika kodi, vijana msiokuwa na ajira mngetamani tuzungumzie masuala hayo, lakini yote hayo yote ni matatizo ya kimfumo, kisera huku chimbuko lake likiwa ni uongozi mbovu. Suluhisho lake ni kuondoa CCM madarakani na kuingiza Chadema madarakani.
“Haya matatizo ya kiuongozi ambayo suluhisho lake ni kubadili uongozi, tunashindwa kutumia hili suluhisho kwa sababu ya kukosa nyenzo inayotuwezesha kuchagua viongozi, ambayo ni uwepo wa uchaguzi huru na haki,”ameongeza
Katibu mkuu wa zamani wa chama hicho, Dk Willibrod Slaa amesema Chadema hawasusii uchaguzi mkuu wa mwaka huu, bali wanataka marekebisho yafanyike ili uchaguzi uwe huru na wa haki na wananchi wachague viongozi wanaowataka.
“Niwaombe tuungane pamoja, tushirikiane na Chadema ili kusukuma ajenda hii uchaguzi usiwepo. Kuhusu Katiba, sote tutambue Katiba haijaandikwa na Mungu na hata tukitaka kuifanyia marekebisho inawezekana ndani ya muda mfupi, tunataka Katiba mpya na sheria mpya.
Awali Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Kaskazini, Samwel Welwel amesema kampeni hiyo inalenga kuhakikisha uchaguzi unaofanyika ni huru na wa haki na wananchi wanachagua viongozi
wanaowataka.
“Mimi ni wakili, mwaka 2019 niligombea uenyekiti wa kijiji change, nikaambiwa sijui kusoma na kuandika, wakati nasimamia kesi hadi za wana CCM mahakamani. Kwa utaratibu huu lazima tudai mabadiliko kwanza.
“Wako wana CCM wachache ambao bado wanaamini baada ya miaka 64 tangu tupate uhuru, tutapata maendeleo chini ya Serikali inayoongozwa na chama hicho, niwaombe wana CCM muungane na Chadema tupiganie haki,” amesema mwenyekiti huyo.
Katika hatua nyingine, makamu Mwenyekiti wa Chadema – Bara, John Heche amefika nyumbani kwa mmoja wa waasisi wa chama hicho, marehemu Phillemon Ndesamburo, mjini Moshi mkoani Kilimanjaro na kuieleza familia kuwa kamati kuu ya chama hicho, imepitisha azimio la kuwaenzi waasisi wa chama hicho.
Heche ambaye ameongozana na viongozi mbalimbali wa chama hicho, amefika kwa Ndesamburo leo Mei 30, 2025 kabla ya kuanza kampeni yao ‘No Refoms No Election’, na kuweka shada la maua kwenye kaburi la marehemu.
Ndesamburo ambaye alikuwa Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Kilimanjaro, tangu mwaka 1992 hadi anakutwa na mauti Mei 31, 2017, aliku mbunge Jimbo la Moshi Mjini kwa vipindi vitatu mfululizo, hadi alipoamua kung’atuka mwaka 2015 na kukiacha kijiti kwa Jafari Michael wa chama hicho.
Akizungumza baada ya kufika nyumbani kwa Ndesamburo, Heche amesema Ndesamburo ni miongoni mwa waasisi wa chama hicho ambao walisimama kukitetea na kukiletea heshima kubwa.
Amesema Ndesamburo alishirikiana na Freeman Mbowe, Edwin Mtei na Bob Makani kukijenga chama hicho na kwamba wataendelea kuwaenzi kutokana na mchango wao katika kukijenga chama hicho.
“Tukiwa kwenye ziara Kanda ya Kaskazini tumefika kwenye familia ya mzee wetu Philemon Ndesamburo ambaye ni miongoni mwa waasisi wa chama chetu ambao walifanya kazi nzuri katika kuanzisha chama hiki, mwishoe chama hiki kimekuwa baraka kubwa kwa nchi yetu kwa sababu ni chama ambacho kinapigania mageuzi ya kiuchumi, kisiasa na kijamii katika nchi yetu,” amesema Heche.
Ameongeza kuwa, “tumefurahi kumuona mama hasa tukikumbuka kwamba mzee alifariki Mei 31 siku kama ya kesho, tukio hili tumelifurahia na tumemuona mama yuko imara, Mungu ameendelea kumbariki tunamuombea afya njema”.
Amesema “tumekuja kutembelea familia yake kuwaambia chama chetu kiko pamoja nao na kumwambia mama kuwa tulipitisha azimio la kamati kuu la kuenzi waasisi wa chama chetu.
“Kwa hiyo atakaposikia kuna jengo la Chadema limepewa jina la Ndesamburo House akubali kuwa ni katika harakati za chama chetu kuenzi hawa wazee, ili majina yao yaishi milele kwa sababu ni watu ambao wamefanya kazi kubwa.”
Baada ya tukio hilo, Heche na tumu yake wameendelea na kampeni ya kudai mabadiliko ya sheria za uchaguzi kabla ya kufanyika kwa uchaguzi mkuu mwaka huu kupitia kampeni yao maarufu ya ‘No Refoms No Election’ katika Wilaya ya Moshi.