Dodoma. Msisitizo kwenye ukusanyaji wa mapato ya ndani ya nchi umetajwa kuwa njia pekee ya kupunguza Deni la Taifa ambalo mpaka mwaka huu wa 2025 limefikia Sh97 trilioni, kwa mu-jibu wa ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali (CAG).
Wadau wa maendeleo ya Taifa wamebainisha hayo leo Mei 30, 2025 jijini Dodoma wakati wa kongamano lililowakutanisha kujadili deni la Taifa ambalo mwenendo wake unaonyesha lime-kuwa likiongezeka mwaka hadi mwaka.
Wamesema endapo Serikali itaweka msisitizo wa kukusanya mapato ya ndani kwa ajili ya shughuli za maendeleo, deni hilo linaweza kupungua badala ya sasa ambapo linaongezeka kila mwaka.
Akizungumza kwenye kongamano hilo, Mkurugenzi wa Mtandao wa Madeni na Maendeleo Tanzania (TCDD), Hebron Mwakagenda amesema kuna haja ya Tanzania kuimarisha mapato yake ya ndani ili iondokane na madeni ambayo hayana ulazima.
Amesema kama nchi itaweka utaratibu mzuri wa kukusanya kodi ambayo itatumika kwenye uwekezaji wa shughuli za maendeleo za ndani, deni la Taifa litapungua tofauti na sasa linavyozidi kuongezeka kila mwaka.
“Mikataba ya ukopaji iwekwe hadharani ili kila mwananchi ajue tunakopa kwa sababu gani na siyo kutangaziwa kuwa deni la Taifa limefika Sh97 trilioni bila kujua tulikopa kwa sababu gani na ndiyo maana kila siku huwa tunashauri Bunge lipewe mamlaka ya kumhoji Waziri wa Fedha ambaye ndiye mwenye dhamana ya kukopa kwa niaba ya Serikali kila anapotaka kukopa na lir-idhie, kama mkopo hauna maslahi kwa Watanzania likataliwe,” amesema Mwakagenda.
Amesema mikopo yote ambayo Serikali inaingia ni lazima ipate kibali kutoka kwenye kamati ya Bunge ambapo Waziri wa Fedha ataenda kueleza ni kwa nini anakopa, kama Bunge litaridhia, atakopa na kama litakataa basi asikope kwa kuwa ndiyo chombo kinachowakilisha wananchi.

Baadhi ya washiriki kwenye kongamano la Kitaifa kuhusu deni la Taifa lililoandaliwa na Mtandao wa Madeni na Maendeleo Tanzania (TCDD) Jijini Dodoma leo Mei 30, 2025. Picha na Rachel Chibwete
Mwakagenda ameshauri kuwe na hotuba ya Waziri wa Fedha kuhusu mikopo peke yake ili wananchi waelewe nchi ilikopa kwa sababu gani na kama fedha hizo zimefanya kazi ili-yokusudiwa, tofauti na sasa ambapo Serikali inakopa lakini miradi inayotekelezwa inaonekana fedha zimetolewa na Rais.
“Ifike mahali Serikali itamke na iwaambie wananchi kuwa inakopa fedha kwa ajili ya miradi ya maendeleo kama vile barabara, afya, maji na huduma nyingine za kijamii badala ya kuonekana zimejengwa kwa fedha za mtu binafsi na siyo Serikali,” amesema Mwakagenda.
Akifafanua kuhusu deni hilo, Abeid Mzee kutoka Wizara ya Fedha, amesema pamoja na wadau na wananchi kulalamikia kuongezeka kwa deni la Taifa, deni hilo ni himilivu kwa vigezo vya Shi-rika la Fedha duniani (IMF) na Benki ya Dunia (WB) kwa kipindi cha miaka 20 ijayo.
Amesema Serikali huwa inakopa fedha kwa ajili ya kuendeshea miradi ya kimakakati ambayo ikikamilika inaliingizia Taifa mapato makubwa ambayo yatasaidia kulipa deni hilo kama vile ujenzi wa reli ya kisasa (SGR) na ujenzi wa bwala la kufua umeme la Julius Nyerere (JNHPP).
“Ikumbukwe kuwa kila mwaka Serikali huwa inatenga kiasi cha fedha kwa ajili ya kulipia deni la Taifa na endapo deni hilo lisingekuwa himilivu, basi tusingeruhusiwa kukopa kwenye taasisi za kimataifa,” amesema Mzee.
Amesema deni la Taifa huwa linaongezeka kutokana na miradi mikubwa inayotekelezwa nchini lakini ukusanyaji wa mapato unakuwa haukidhi utekelezaji wa miradi hiyo, hivyo ili kuitekeleza Serikali ni lazima iingie kwenye madeni ambayo ina uwezo wa kuyalipa.
Amesema kama mapato ya ndani ya nchi yatazidi miradi inayotekelezwa Serikali itaondokana na madeni kwa sababu itakuwa na uwezo wa kugharamia miradi yote inayotekelezwa ndani ya nchi kwa mapato yake ya ndani.
Kwa upande wake, mjumbe wa bodi ya TCDD, Boniface Buliga ameitaka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (Takukuru) kuisimamia kwa ukaribu miradi yote ambayo fedha zake zimepatikana kwa njia ya mkopo ili zitumike kwa lengo lililokusudiwa.
Amesema wakati mwingine Serikali inakuwa na nia njema ya kukopa kwa ajili ya kuendeshea miradi mbalimbali ya kimkakati lakini wakandarasi na wasimamizi wanaosimamia miradi hiyo wanakuwa siyo waadilifu na hivyo kusababisha fedha hizo kutofanya kazi iliyokusudiwa.
Naye Mkurugenzi wa Taasisi ya Amka Mtanzania, Tobia Msihi amesema kuongezeka kwa deni la Taifa kunaathiri uchumi wa nchi kwa sababu makusanyo yote yanayopatikana ndani ya nchi yanakwenda kulipia madeni, hivyo kuwabebesha wananchi mzigo mzito wa kodi.