Dar es Salaam. Ikiwa imepita mwezi mmoja tangu Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu (TEC), Padri Kitima ashambuliwe, Jeshi la Polisi limeeleza hatua ilipofikia katika kufuatilia uchunguzi wa tukio hilo.
Padri Kitima alishambuliwa Aprili 30, 2025, majira ya saa nne usiku, katika makazi na Makao Makuu ya Baraza hilo yaliyopo Kurasini Wilaya ya Temeke jijini Dar es Salaam.
Katika tukio hilo, Padri Kitima inadaiwa alishambuliwa kwa kupigwa na kitu butu kichwani na tayari watu wawili wameshakamatwa wakidaiwa kuhusika na tukio hilo akiwemo.
Kati ya waliokamatwa yupo Edward Cosseny (51) mkazi wa Dodoma, kutokana na chapisho lake la vitisho dhidi ya Padri Charles Kitima ambalo kwa mujibu wa ufuatiliaji alilitoa na kulichapisha mitandaoni siku chache kabla ya kutokea kwa tukio liliomuhusisha Padri Kitima.
Kukamatwa kwa Cosseny, kulitokana na agizo lililotolewa na Waziri wa Mambo ya Ndani, Innocent Bashungwa.
Akizungumza leo Jumamosi Mei 31, 2025 na waandishi wa habari, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro amesema ni jukumu la kisheria kuhakikisha wanapata maelezo ya Padri kitima ya kimaandishi.
Kamanda Muliro amesema wakati ule tukio lilipotokea ilikuwa vigumu mtu akiwa anaumwa ukaanza kutumia njia ya kutaka kupata maelezo kutoka kwake.
“Atakapotulia tutaweza kupata maelezo ya kina ya kimaandishi ambayo yataingia kwenye mafaili na kwenda kwenye mfumo wa mashtaka kwani huu ndio msingi wa kisheria.
“Kama serikali inapofanya kazi katika mfumo wa kimaandishi mafaili sasa yataweza kutoka sehemu moja kwenda nyingine kwa kuwa sasa unamuona Father (Padri) katika maandishi yake,” amesema Kamanda Muliro.
Hata hivyo ameeleza kuwa licha ya kuwa kesi hiyo imefunguliwa na Jamhuri lakini shahidi mkuu ni Padri Kitima.
“Kwa hiyo ni busara za kisheria atakapokuwa ametulia kupata taarifa za kimaandishi kutoka kwake,” ameeleza.
Kamanda Muliro amesema hiyo ni hatua nyingine ukiacha taarifa za awali ambazo wameshazipata ambazo wameshazifanyia kazi katika yale ambayo yalitakiwa kufanywa.
Aidha Kamanda huyo amewahakikishia wananchi kuwa bado jeshi hilo linafanya kazi ili kuhakikisha usalama unaimarika katika Jiji la Dar es Salaam.
Katika hatua nyingine Jeshi hilo la Polisi limesema kuanzia Januari 2023 hadi Mei 2025 ilipeleleza na kuwakamata watuhumiwa mbalimbali ambao baadhi yao walifikishwa kwenye mahakama tofauti zilizopo jijini kwa tuhuma mbalimbali.
Baadhi ya mashauri yao yamefika mwisho kusikilizwa na wamepatikana na hatia na kati ya hayo zipo kesi kumi za ubakaji na kesi nane za ulawiti na kesi tisa za unyang’anyi wa kutumia silaha.
Kwa upande wa hali ya usalama barabarani, Kamanda Muliro amesema kuanzia Aprili Mosi hadi Mei 31, 2025, Jeshi hilo lilidhibiti makosa hatarishi ya madereva walevi pamoja na wanaotumia barabara za mabasi yaendayo haraka (Mwendo kasi) na kuchukuliwa hatua kali kama.
Katika muda huo amesema madereva 289,waliokamatwa kwa kutumia barabara za mwendo kasi kinyume na sheria kati yao 61 ni wa pikipiki (bodaboda), 65 wa bajaji 35 wa magari ya Serikali 35, na 123 walikuwa magari binafsi 123 ambapo kati yao wapo waliochukuliwa hatua kali za kisheria na wengine 41 walionywa.
“Aidha Kwa kutumia kifungu cha 45 na 46A vya Sheria ya Usalama barabarani sura ya 168 iliyorekebishwa mwaka 2002 kinachokataza dereva kutumia kilevi na kuendesha chombo cha moto, ufuatiliaji Maalum usiku na mchana ulifanywa na kuwapima ulevi madereva kwa dharura.
Katika ufuatiliaji huo madereva 19 walikamatwa wakiwa walevi kwa kuzidisha kiwango cha kisheria ambacho ni 0.8mls ambapo Mkoa wa Kinondoni walikuwa 18 na Ilala 1“
Pia kati ya madereva waliobainika kuwa walevi, madereva wa magari, binafsi walikuwa 16 ambao kwa mujibu wa sheria ya Usalama barabarani sura 168 iliyorekebishwa mwaka 2002 kifungu cha 49 inaelekeza kuwa kiwango cha ukomo wa ulevi kuwa ni 0.8mg,” amesema Kamanda Muliro.
Vilevile madereva wa magari ya abiria walikuwa 3 ambao kwa mujibu wa kanuni zinazosimamia usafiri wa umma hairuhusiwi kwa dereva kutumia kiwango chochote cha ulevi na kuendesha gari la abiria.
Kati ya hao, amesema madereva 14 wamefikishwa mahakamani, madereva 3 wamefungiwa leseni na madereva 2 waliandikiwa faini.
“Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam linatoa rai kwa watumiaji wote wa barabara kuzingatia Sheria, Kanuni, na matumizi sahihi ya barabara muda wote wanapoendesha vyombo vya moto.
“Pia Jeshi linaendelea kuwashukuru wananchi na vyombo vingine vya dola na sheria kwa ushirikiano wa kuhakikisha Dar es Salaam inaendelea kuwa salama,” amesema Kamanda Muliro na kuongeza kuwa mwaka huu Jeshi hilo limejipanga, na halitamuonea aibu mtu yoyote atakayejihusisha na vitendo vya uhalifu.