Iringa. Katika kuhakikisha kuwa miundombinu ya usafirishaji inaboreshwa mkoani Iringa, Mkuu wa Wilaya ya Iringa Kheri James amekitaka Chama cha Wasafirishaji mkoani humo kuanza kubuni njia za safari kwenye barabara mpya zinazojengwa, ikiwemo barabara ya mchepuo kutoka Kihesa Kilolo hadi Igumbiro na ile ya Kalenga kuelekea Hifadhi ya Taifa ya Ruaha.
DC Kheri James ametoa agizo hilo leo Mei 31, 2025 katika ukumbi wa mikutano wa Hans Pope uliopo Halmashauri ya Manispaa ya Iringa, alipokuwa akifungua kikao cha mwaka cha Chama cha Wasafirishaji pamoja na kuzindua rasmi ofisi ya kanda ya kati ya chama hicho kanda, itakayokuwa Iringa katika jengo la Hanspoppe.
“Chama cha usafirishaji kisisubiri wananchi waanze kuomba njia mpya, kinapaswa kubuni njia hizo mapema ili kuendana na kasi ya maendeleo ya miundombinu,”amesema James na kuongeza.
“Tunahitaji kuona usafirishaji unakuwa wa kisasa na wenye mpangilio unaoendana na barabara mpya tunazojenga, kama ya Kihesa Kilolo–Igumbiro na Kalenga–Ruaha,”amesema
Kiongozi huyo amepongeza jitihada zinazofanywa na chama hicho lakini akaonya kuwa wasisubiri wananchi waanze kuomba njia hizo mpya ndipo wachukue hatua, badala yake waanze mapema kupanga na kutangaza huduma hizo ili kusaidia maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa wakazi wa maeneo hayo.
Pia ametaka ofisi hiyo ya kanda ya kati mkoani Iringa iwe kichocheo cha maendeleo ya sekta ya usafirishaji kwa mikoa ya nyanda za juu kusini.
Makamu wa Rais wa Chama cha Wasafirishaji Tanzania, Omary Kiponza, amesema chama hicho kimekuwa kikijivunia mafanikio makubwa tangu kuanzishwa kwake mwaka 2015, kikiwa na zaidi ya Wanachama 1,000 wanaojihusisha na shughuli za usafirishaji nchini.
“Tangu mwaka 2015, chama chetu kimefanikiwa kuwafikia zaidi ya wananchi 1,000 wanaojihusisha na usafirishaji nchini,”amesema Kiponza na kuongeza kuwa
“Kituo cha kanda ya kati kitasaidia kurahisisha shughuli za usafirishaji katika mikoa ya Mbeya, Ruvuma, Njombe, Rukwa na Katavi,”
Ameeleza kuwa kituo hicho kipya cha kanda ya kati kitaongeza ufanisi kwa kushughulikia kwa haraka mahitaji ya usafirishaji katika mikoa ya Mbeya, Ruvuma, Njombe, Rukwa, Songwe na Katavi.
Kiponza amesema kuwa kusogeza huduma hiyo karibu na wanachama kutaongeza wepesi wa kutoa huduma stahiki kwa wasafirishaji, hasa katika kuhakikisha kuwa usafirishaji wa mizigo hasa ya mazao ya kilimo unazingatia taratibu maalumu na sheria za usafirishaji wa mazao hayo.
Aidha, Kiponza ameongeza kuwa ofisi hiyo mpya ya chama hicho haitahudumia tu wanachama bali itasaidia pia wananchi wa kawaida kwa kupokea kero na changamoto mbalimbali zinazohusu usafirishaji na kuziwasilisha kwa mamlaka husika ili zipatiwe ufumbuzi kwa haraka.
Wakizungumza na Mwananchi Digital baadhi ya wasafirishaji kutoka mkoani Iringa wameshauri kuwa chama hicho inabidi kianzishe utaratibu wa kutoa elimu kwa wasafirishaji wapya kuhusu sheria na taratibu za sekta hiyo ili kusaidia kupunguza changamoto za mara kwa mara zinazotokana na kutoelewa miongozo ya mamlaka ya usafirishaji.
“Kupatikana kwa ofisi hii Iringa kutapunguza gharama za ufuatiliaji wa vibali na malalamiko; huduma sasa zitakuwa karibu,”amesema Abel Chatanda mmoja wa wasafirishaji kutoka mkoani Iringa.
“Tunapendekeza chama kiweke mfumo wa kidigitali utakaotuwezesha kupata msaada au taarifa kwa haraka kupitia simu au mtandao,”amesema Elia Ngasi msafirishaji kutoka mkoani Iringa.
Pia wasafirishaji hao wamependekeza kuwepo kwa mfumo wa kidigitali unaowawezesha kuwasiliana moja kwa moja na ofisi ya chama kwa njia ya simu au mtandao, ili kurahisisha utatuzi wa matatizo na ufuatiliaji wa taarifa mbalimbali kwa wakati.