Dar es Salaam. Wizara ya Afya imetaja sababu ya ongezeko la magonjwa ya mfumo wa upumuaji, huku wataalamu wa afya wakiebainisha hatua sahihi za kuchukua kwa wagonjwa.
Kauli hiyo imekuja, wakati kukiwa na ongezeko la wagonjwa wa mafua, kifua na kikohozi nchini, hususani katika Jiji la Dar es Salaam, Arusha na Dodoma na baadhi ya mikoa nchini.
Akizungumza na Mwananchi leo Jumamosi, Mei 31, 2025 Mkurugenzi wa huduma za dharura na maafa, Dk Erasto Silvanus amesema licha ya ongezeko la wagonjwa wanaobainika na Uviko19, maambukizi ya virusi vingine tofauti vinavyosababisha athari kwenye mfumo wa upumuaji na mafua, pia yameongezeka.
Kukiwa na hali hiyo nchini, Shirika la Afya Duniani, WHO juzi liliripoti kuwa mpaka kufikia Mei 11, 2025 sampuli zilizopimwa katika nchi 73, asilimia 11 zilionyesha maambukizi ya Uviko19 na kwamba virusi aina ya SARS-CoV-2 ndivyo vinavyoonekana.
Kwa mujibu wa WHO, Kiwango hiki kinakaribia kilele kilichoshuhudiwa Julai 2024 cha asilimia 12 kutoka nchi 99, na kinaonyesha ongezeko kutoka asilimia 2 iliyoripotiwa na nchi 110 katikati ya Februari, 2025.
Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa nchini Mei 20, 2025 na Ofisi ya Mganga Mkuu wa Serikali, Dk Grace Magembe kupitia taarifa kwa umma, wizara ilikuwa imebaini kuna ongezeko la wagonjwa wenye Uviko-19.
Ilitaja ongezeko hilo ni kutoka watu wawili kati ya 139 waliopimwa Februari, sawa na asilimia 1.4 hadi wagonjwa 31 kati ya watu 185 waliopimwa Aprili 2025, sawa na asilimia 16.8.
Hata hivyo, licha ya hali hiyo, Dk Erasto amesisitiza kuwa hakuna mlipuko wa Uviko19 hapa nchini kwani uliisha 2023, baada ya kutangazwa si mlipuko tena.
“Kuna virusi wengi tofauti, wanaougua wanatakiwa waende hospitali wapimwe. Mei 20 tulikuwa tunaonyesha kwamba tuliwafuatilia watu mbalimbali, tunapima aina ya virusi walivyonavyo na wapo tuliowabaini wana virusi vya Uviko19.”
Amesema kwa sasa wanaopata maambukizi, wana virusi mbalimbali wengine, hivyo lazima waende hospitali wapimwe wajue ni kitu gani.
“Uviko utakupa homa kidogo tu, lakini kinachowabana walio wengi ni virusi wengine. Virusi vya magonjwa ya upumuaji kuna influenza wa aina nyingi, wanakupa homa na kichwa kitamuuma, ni muhimu watu wakaenda kupimwa wajue ni kirusi gani, wasihisi tu Uviko19. Kuna vurusi zaidi ya 100 vinavyosababisha homa na magonjwa ya upumuaji,” amesema.
Dk Erasto ameongeza virusi hao huibuka kutokana na misimu tofauti, inategemea mazingira yanapobadilika kutoka kwenye joto kwenda baridi, msimu wa mvua kwenda msimu mwingine.
Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili katika baadhi ya vituo binafsi na vile vya umma, kumeonekana na ongezeko la wagonjwa wanaofika wakilalamika kichwa, homa, misuli kuuma na magonjwa mengine ya mfumo wa upumuaji, kwa mujibu wa wahudumu wa afya.
Baadhi ya wauzaji wa maduka ya dawa nao wameeleza kupata wateja wengi wanaougua mafua na kifua katika msimu huu.
Kufuatia hali hiyo, Daktari bingwa wa magonjwa ya mfumo wa upumuaji kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili, Alex Masao amesema hiyo ni changamoto inayowasumbua wengi kwa sasa.
“Watu wanatakiwa kujikinga, yeyote mwenye mafua anaweza kuambukiza, hii homa inaambukiza kwa njia ya hewa, jikinge kwa njia zote tulizojikinga na Uviko19 usipate maambukizi na ukipata nenda vituo vya afya, usijitibu kwa dawa za antibaotiki, unatengeneza usugu,” amesema Dk Masao.
Ushauri wa Dk Masao unafanana na wa Dk Elisha Osati, daktari bingwa wa magonjwa ya mfumo wa upumuaji MNH ambaye ameitaka jamii kufika vituo vya afya kuonana na wataalamu na kuwakinga wengine.
“Tunaotibu magonjwa ya hewa tunajua kwa sababu tuna uzoefu wa Uviko19, mtu ahakikishe akiwa na mafua makali asijichanganye na wengine au atumie barakoa ili asiambukize wengine, nawa mikono mara kwa mara na tumia sanitaiza kama utaweza,” amesisitiza na kuongeza;
“Tunajua watu wanatumia sana tangawizi na limao, hasa katika chai ya moto au vinywaji vya moto, tunashauri waendelee na waongeze matumizi maana vinasaidia kuzibua pua kidogo na kusafisha koo, hii ni njia nzuri ya kujikinga,” amesema.
Taarifa ya WHO imesema tangu katikati ya Februari 2025, kulingana na takwimu zinazopatikana kutoka kwenye vituo vya ufuatiliaji, kirusi aina ya SARS-CoV-2 kimesambaa na kuongeza idadi ya waathirika.
Imesema kuongezeka huku kwa maambukizi kunashuhudiwa hasa katika nchi za Kanda ya Mediterania ya Mashariki, Kusini-Mashariki mwa Asia na Ukanda wa Pasifiki wa Magharibi.
Tangu mwanzoni mwa mwaka 2025, mwenendo wa virusi aina ya SARS-CoV-2 duniani umebadilika kwa kiasi kidogo.
Kuongezeka hivi karibuni kwa virusi vya SARS-CoV-2 kunalingana kwa kiasi kikubwa na viwango vilivyoshuhudiwa katika kipindi kama hiki mwaka uliopita.
Hata hivyo, bado hakuna msimu maalumu unaoweza kutabirika wa mzunguko wa SARS-CoV-2, na ufuatiliaji wa maambukizi bado ni mdogo, hivyo kuhitajika ufuatiliaji endelevu.
WHO inashauri nchi wanachama wote kuendelea kutumia mbinu ya ufuatiliaji wa Uviko19 iznazozingatia tathmini ya hatari na inayoambatana na mifumo mingine ya afya, kama ilivyoelezwa katika mapendekezo ya kudumu ya mkurugenzi mkuu wa WHO.