Takukuru yaeleza madudu yaliyoibuka mkoani Rukwa

Rukwa. Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Mkoa wa Rukwa, kupitia kwa Mkuu wake, Mzalendo Widege, imeelezea hatua mbalimbali zilizochukuliwa katika kudhibiti rushwa na kuimarisha uwajibikaji wa matumizi ya fedha za umma  katika kipindi cha robo ya kwanza ya mwaka 2025.

Akizungumza na Mwananchileo Mei 31, 2025 ofisini kwake, Kamanda Widege alisema Takukuru imebaini mapungufu makubwa katika utoaji na urejeshaji wa mikopo, pamoja na utekelezaji wa baadhi ya miradi ya maendeleo.

Katika kipindi hicho, Takukuru ilitembelea na kukagua jumla ya miradi 15 ya maendeleo yenye thamani ya zaidi ya Sh6 bilioni. Ukaguzi huo ulibaini dosari mbalimbali za kiutendaji, na taasisi hiyo ilitoa ushauri wa kitaalamu kwa mamlaka husika, ambao umeanza kufanyiwa kazi.

Aidha, taasisi hiyo ilifanya uchambuzi wa mfumo wa utoaji na urejeshaji wa mikopo ya asilimia 10 kwa makundi maalum vijana, wanawake na watu wenye ulemavu katika Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga. Uchunguzi huo ulibaini kuwa kiasi cha Sh224.9 milioni kilikuwa hakijarejeshwa.

Hata hivyo, kutokana na ufuatiliaji wa karibu uliofanywa na Takukuru, kiasi cha Sh38.5 milioni kimeweza kurejeshwa, huku Sh186.4 milioni  zikiendelea kufuatiliwa ili kuhakikisha zinarudi serikalini kwa ajili ya kusaidia maendeleo ya jamii.

Katika suala la utoaji elimu kwa umma, Takukuru Mkoa wa Rukwa imeendelea kutoa elimu kuhusu madhara ya rushwa kwa jamii pamoja na kuelekeza elimu hiyo kuelekea uchaguzi mkuu ujao.

Ambapo kamanda Widege ameiambia Mwananchi kuwa wataendelea kutoa elimu kwa wananchi ya namna ya kuepuka rushwa hasa kipindi cha uchaguzi sambamba na wagombea kuacha tabia ya kutoa rushwa ili wapate nafasi za uongozi.

“Tutatoa elimu ya rushwa ili wananchi wafahamu madhara ya rushwa katika kipindi cha uchaguzi na kujua kiongozi yupi anafaa kuwaongoza na sio watoa rushwa,” amesema Widege.

Aidha Widege amesema Katika kipindi husika, taasisi imefanikiwa kufikia jumla ya klabu 74 za wapinga rushwa katika shule na taasisi mbalimbali.

Takukuru imesisitiza dhamira yake ya kuendelea kushirikiana na wananchi, viongozi wa serikali na wadau wengine katika kuhakikisha vitendo vya rushwa vinatokomezwa kikamilifu mkoani Rukwa.

Fedha hizo zinatokana na asilimia 10 ya mapato ya ndani katika halmashauri ya wilaya ya Sumbawanga ambazo wamefanikisha kuzirejesha.

Nao baadhi ya wananchi akiwemo Sarah Mohamed mkazi wa Kaloleni ameliambia mwananchi kuwa elimu inahitajika kwa wananchi ili wafahamu madhara na athari zinazoweza kutokea pindi akipokea rushwa.

“Uelewa wa wananchi kuhusu rushwa bado ni mdogo Takukuru inapaswa kuongeza hamasa na elimu katika jamii,” amesema Sarah.

Ameongeza kuwa baada ya uchunguzi wa awali, fedha hizo zote zimerudishwa kwenye halmashauri husika ili ziendelee kutumika katika miradi ya maendeleo.

Mzee Steven Siwale mkazi wa kata ya Milanzi wakazi amepongeza hatua hiyo ya Takukuru akisema inaonyesha mwelekeo chanya katika vita dhidi ya vitendo vya rushwa.

“Hii ni hatua nzuri, lakini ni muhimu wale wote ambao hawarudishi mikopo wachukuliwe hatua za kisheria ili iwe fundisho kwa wengine wenye tabia kama hizo  kwa kuwa wanawachelewesha wananchi wengine kukopa na kurudisha nyuma maendeleo,” amesisitiza Mzee Siwale.

Naye Mwalimu  Hassani Shabani ametoa wito kwa  Takukuru kuongeza kasi na juhudi za kutoa elimu kwa wananchi juu ya mbinu za kuzuia na kuripoti vitendo vya rushwa.

Related Posts