Arusha. Katika kukabiliana na madhara yatokanayo na kuzagaa kwa taka za plastiki nchini, serikali imewaita wadau wa sekta binafsi kushirikiana kupunguza tatizo hilo ikiwemo kufanya bunifu mbalimbali zenye kuzirejesha katika matumizi.
Tanzania inakadiriwa kuzalisha zaidi ya tani milion 20 za taka ngumu kila mwaka, ikiwa ni wastani wa kilo 300 kwa mtu mmoja kwa mwaka huku maeneo ya mijini ikiongoza.
Hata hivyo asilimia 70 ya taka ngumu zinazozalishwa nchini zinaweza kurejelezwa au kurekebishwa na kutumika tena (recyclable) ikiwemo plastiki lakini ni asilimia10 tu ya taka hizo zinazorekebishwa.
Akizungumza katika uzinduzi wa wiki ya maadhimisho ya mazingira duniani leo Mei 31,2025, Mkuu wa kitengo cha udhibiti wa taka na usafi wa mazingira Jiji la Arusha James Lobikoki amesema kuwa kiwango kidogo cha urejelezaji kinatokana na utekelezaji hafifu wa dhana ya 3R (Punguza, tumia tena na Rekebisha), hasa katika sekta binafsi.
“Katika kupunguza uchafuzi wa mazingira kwa plastiki, tumeanza kuzuia matumizi ya plastiki yasiyo ya lazima kwa wananchi wetu lakini pia tunawaalika sekta binafsi na watu wote kushirikiana na serikali kuondoa tatizo hili.
“Kwanza kuendelea kufanya bunifu zenye kuhitaji malighafi za taka za plastiki lakini pia teknolojia za urejelezaji wa taka za plastiki kwani uhitaji wake utapunguza kuzagaa mitaani, lakini pia wananchi wetu wapunguze matumizi ya vitu vya plastiki na bidhaa za plastiki yasiyo ya lazima, “amesema
Katika maadhimisho hayo yenye kauli mbiu ‘mazingira yetu, Tanzania ijayo tuwajibe sasa kudhibiti matumizi ya plastiki’ yalikwenda sambamba na kufanya usafi katika maeneo mbalimbali ya soko kuu, stendi kubwa ya mabasi na mitaa mbalimbali ya Jiji la Arusha.
Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Joseph Mkude amewataka wananchi wa Arusha kuhakikisha wanaishi na kufanya biashara katika maeneo masafi Ili kutunza mazingira,kuepukana na magonjwa lakini pia faini ndogo ndogo.
“Kuanzia sasa hivi tutafanya operesheni za mara kwa mara, ukikutwa unaishi, unafanyabiashara au umekaa eneo chafu lenye taka zozote unatozwa faini ya papo kwa hapo sh50,000 na kuamriwa kufunga biashara au nyumba na kufanya usafi kwanza” amesema Katibu tawala Wilaya ya Arusha Jacob Julius Rombo, kwa niaba ya mkuu wa wilaya.
Mwenyekiti wa huduma za maendeleo ya jamii Jiji la Arusha Issaya Doita amesema kuwa usafi umesaidia Jiji hilo kuondokana na magonjwa ya milipuko ambayo Arusha ilikuwa inakumbana nayo miaka ya nyuma hasa msimu wa mvua