Arusha. Rais mpya wa Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu (AfCHPR) anatarajiwa kujulikana Jumatatu, wakati jopo la majaji wa Mahakama hiyo litakapofanya uchaguzi wa viongozi wapya wa taasisi hiyo ya juu ya haki barani Afrika.
Uchaguzi huo utafanyika katika Kikao cha 77 cha Kawaida cha Mahakama kinachotarajia kuanza muhula wake mpya Jumatatu Juni 2, 2025.
Mahakama hiyo inayoongozwa kwa sasa na Rais wake Mtanzania Jaji Imani Daud Aboud anahitimisha rasmi majukumu yake ya kuongoza mahakama hiyo kwa kipindi cha miaka minne.
Mbali na jaji Aboud, pia makamu wake wa kiti cha urais Jaji Modibo Sacko wa Mali anaachia kiti hicho rasmi baada ya kuongoza vipindi viwili vya miaka miwili.
Wawili hao walichukua nafasi hizo za juu mwaka 2021 katika kikao cha 61 cha Mahakama na kuhitimisha muhula wao wa kwanza mwaka 2023 kabla ya kuchaguliwa tena kuongeza kipindi kimoja ambacho ndio ukomo kwa mujibu wa taratibu na Sheria ya mahakama hiyo isiyoruhusu mtu kuongoza zaidi ya vipindi viwili.
Jaji Imani Aboud, ambaye pia ni mwanamke wa kwanza kutoka Afrika Mashariki kushika nafasi ya juu katika chombo hicho cha kimahakama, alichukua nafasi ya Jaji Sylvain Oré wa Côte d’Ivoire, wakati Jaji Sacko alichukua nafasi ya Jaji Ben Kioko wa Kenya.
Kwa mujibu wa utaratibu wa Mahakama hiyo, Rais na Makamu wake huchaguliwa na jopo la majaji 11 kwa kura ya siri.
Majaji wanaotarajia kupiga kura hiyo ya Siri kuwapata viongozi wapya ni pamoja na Jaji Imani Daud Aboud (Tanzania), Jaji Modibo Sacko (Mali), Jaji Blaise Tchikaya (Congo-Brazzaville ), Jaji Rafaâ Ben Achour (Tunisia).
Wengine ni Jaji Tujilane Rose Chizumila (Malawi), Jaji Dumisa Ntsebeza (Afrika Kusini, Jaji Stella Isibhakhomen Anukam (Nigeria), Jaji Angela Mudukuti (Zimbabwe), Jaji Naceesay Salla-Wadda (Gambia), Jaji Koffi Afande (Togo), Jaji Aboudou Assouma (Benin).
Rais mpya atakayeibuka ataiongoza Mahakama hiyo kutoa maamuzi ya mashauri saba ya kihistoria yaliyojadiliwa katika vikao vya 76 na 77.
Pia, atasimamia utekelezaji wa maamuzi ya Mahakama ikiwa ni pamoja na yale ya jamii ya Ogiek dhidi ya Kenya, na mashauri yanayohusiana na watu wenye ualbino nchini Tanzania.