Mwanga. Ili kukuza uchumi wa mtu mmoja mmoja na nchi kwa jumla Benki ya Mwanga Hakika imewahakikishia mazingira bora ya uwekezaji wanahisi wake.
Kwa mujibu wa Sheria ya Kampuni mwaka 2002 na Sheria ya Masoko ya Mitaji na Dhamana ya mwaka 2002 hisa ni sehemu ya rasilimali za kampuni.
Kununua hisa ni kununua sehemu ya umiliki wa kampuni na huwakilisha masilahi yako kwenye kampuni husika.
Jana Mei 31, 2025, wanahisa wa Benki ya Mwanga Hakika (MHB) wameeleza kuridhishwa na ongezeko kubwa la faida la asilimia 53 na mipango mkakati ya benki hiyo ya kuboresha huduma kwa wateja na kukuza uchumi wakati wa Mkutano Mkuu wa Mwaka (AGM) wilayani Mwanga, mkoani Kilimanjaro.

Wanahisa hao waliona uwekezaji wao una tija baada ya matokeo ya mwaka 2024, kuonesha ongezeko kubwa la asilimia 53 ya faida, kufikia Sh9.9 bilioni kutoka Sh6.5 bilioni mwaka uliopita 2023.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Benki ya Mwanga Hakika, Ridhuan Mringo amesema mafaniko yanatokana na mipango madhubuti ya benki hiyo.
Vilevile amemtaja kwa heshima mwanzilishi mmojawapo wa benki hiyo, Hayati Cleopa David Msuya, aliyekuwa Makamu wa Kwanza wa Rais na Waziri Mkuu mstaafu, akisema alikuwa zaidi ya muasisi katika benki na wataendelea kumuenzi.
“Tunajivunia mafanikio haya na kuboresha shughuli zetu na kuhakikisha benki hiyo inatoa huduma katika wigo mpana zaidi,” amesema Mringo.
Mzee Msuya alifariki dunia Mei 7, 2025 katika Hospitali ya Mzena, Kijitonyama jijini Dar es Salaam alipokuwa kipatiwa matibabu ya moyo na mwili wake ulizikwa Mei 13, 2025 katika Kijiji cha Chomvu, Usangi, wilayani Mwanga.
Mkuu wa Idara ya Fedha ya benki hiyo, Chomete Hussein amesema faida baada ya kodi iliongezeka hadi Sh14.6 bilioni, sawa na alisema 46.

Amesema Amana za wateja ziliongezeka kwa asilimia 51 hadi kufikia Sh214.8 bilioni, huku jumla ya mali ikifika Sh324.9 bilioni.
“Kwenye robo ya kwanza ya mwaka 2025, benki imepata faida ya Sh4.1 bilioni kabla ya kodi, na mali zimefikia Sh355.5 bilioni huku mikopo ikifikia Sh220 bilioni na amana zikiongezeka hadi Sh261.2 bilioni.
“MHB pia imeongeza mtaji wake kutoka Sh17 bilioni Sh26 bilioni, jambo lililosaidia kuongeza mtaji wa wanahisa hadi Sh48.3 bilioni, hali inayoimarisha uthabiti wa kifedha wa benki na uwezo wa kupanua huduma zaidi,” amesema.
Mkuu wa Kitengo cha Wateja Wakubwa, Projest Massawe alisema benki imeendelea kutoa huduma kwa wateje wakubwa, wadogo na wa kati, kwa kuendelea kuwapa huduma bora zaidi na zinao kidhi mahitaji yao.
Amesema mafanikio hayo yanatokana na ukaribu wa benki hiyo na jamii, “siku chache kabla ya mkutano huu, tumefanya zoezi la upimaji wa afya ya macho bure, pamoja na hutoa miwani kwa waliokutwa na changamoto ya afya ya macho bure, kwa wakazi Ugweno na Usangi, wilayani Mwanga.”