Kisa kifuatacho kinafupisha tutakayodurusu hasa umbumbumbu, ujinga na unyama wa jinsia.
Huko Kunduz, Afghanistan, mwaka 2011, (CNN, 2012), Sher Mohamed, 29, akisaidiana na mama yake mzazi Wali Hazrata, alimuua mkewe kwa sababu alimzalia watoto wa kike watatu.
Hivyo, adhabu ya ‘kosa’ la kutozaa watoto wa kiume kwa huyu bwana na familia yake ni kifo!
Kwa mujibu wa NPR, mpaka mwaka 2016, nchini China, kulikuwa na mabachela au guang guan, yaani matawi yaliyovunjika milioni 30 waliokosa wachumba kutokana na upungufu wa wachumba.
Balaa hili lilisababishwa na sera ya China ya kila familia kuruhusiwa kuzaa mtoto mmoja iliyobabisha wazazi wengi kutoa mimba za watoto wa kike.
Mshindi wa Tuzo ya amani ya Nobel, mchumi Amartya Sen, anakadiria kuwa zaidi ya mimba milioni 100 za watoto wa kike zilitolewa hadi mwaka 2016.
Kurahisisha jinai hii, kuna kifaa cha umeme kiwezacho kutambua jinsi ya mtoto tumboni kinachogharimu kati ya dola za Marekani 10 hadi 20.
Hali hii imesababisha upungufu wa mabinti wa kuoa hadi kugeuka biashara. Mfano, ili kumtoa binti yao, kuna wazazi wanataka mahari isiyopungua dola 15,000, gari, na nyumba. Kwa wasio na uwezo, kuoa ni kama ndoto.
Kwa vile lengo letu siyo kuzama kwenye takwimu, tungependa kudurusu mambo ya kufanya ili kuepuka hiki tunachokiita unyama wa kijinsi.
Kwanza, jamii inapaswa kuwakubali, kuwalinda, na kuwathamini watoto wa kike sawa na wa kiume. Hii, haitasaidia kuondoa upungufu wa wachumba tu bali kuheshimu, kulinda, na kupenda watoto wa kike sawa na watoto wa kiume.
Kwetu, ni unyama na ujinga kubagua watoto. Hatusemi hivi kujiridhisha au kuwaridhisha wengine. Sisi tunao mabinti wanne na wavulana wawili.
Mbali nasi, wapo watu tena maarufu walioridhika na kuwa na watoto wa kike tu. Marais Bill Clinton na Barack Obama (Marekani) na Mauno Mauno Koivisto (Finland) walizaa wasichana tu. Lakini hawana shida wala kuhangaishwa na kupata watoto wa kiume.
Pili, jamii ielimishwe kuwa ‘kosa’ la kutozaa watoto wa kiume, kisayansi, ni la mwanaume, siyo mwanamke. Kwa waliosoma somo la uzazi, wanajua na wakumbuke kuwa mwanamme ana chromosomes X na Y ambazo hutegeneza watoto wa kiume.
Kama baba atatoa manii yenye X pekee yakaungana na yai la mama ambaye hubeba X tu, atazaliwa binti. Akitoa Y ikachanganyikana na X ya mama, anazaliwa mtoto wa kiume. Hivyo, wa kustahili kuuawa japo hatushauri, ni baba, siyo mama.
Je, kwanini watu wengi hawapendi watoto wa kike? Jibu ni rahisi, mabinti wakiolewa, hubeba na kuendeleza ubini wa familia nyingine. Je, ukiacha au kutoacha mrithi, inakusaidia nini zaidi ya ujinga na ukatili vya kawaida?
Tatu, kabla ya kuichomoa mimba ya binti, jiulize. Kama wakwe zako wangekuwa katili, wajinga, na wapumbavu kama vyako, ungeoa nani na wapi?
Japo tumeliona tatizo hili kama la bara la Asia, linaweza kutukuta kama hatutaacha ubaguzi, ujinga, ukatili, na unyama wa kijinsia.
Kuna njia mbili mujarabu za kuondosha balaa na kadhia hii. Kwanza, ni kutoa elimu ya uzazi kwa jamii ili kuepuka ukatili na upumbavu dhidi ya watoto wa kike. Pili, ni kutoa adhabu kali kwa wanaotenda jinai hii. Kama ingewezekana, wanaopatikana na makosa ya kuua vichanga wangefungwa maisha hata kuuawa kutoa onyo kwa ambao hawajatenda jinai hii.
Ujinga, ukatili, na unyama wa kijinsia ni matokeo ya kutoelimika na kustaarabika kwa jamii. Kama hazai watoto wa kiume, si umuache kuliko kumuua?
Wapo tunaowafahamu au kusikia walioacha au kuoa wake wengine baada ya wake zao kutozaa watoto wa kiume na baadaye wakawazaa. Wengi, Mungu aliwaeleleza.
Kwani, mabinti waliowakataa walitokea kuwa muhimu kuliko kaka zao. Mfano, nani anawajua kaka zake Margareth Thatcher, waziri mkuu wa zamani wa Uingereza?
Je, yeye na hao nani zaidi? Tuepuke umbumbumbu na ukatili wa kijinsia. Watu wote ni sawa na wana mchango sawa katika maisha.
Kwa mrejesho, tumia email hii tafadhalinesaa1977@ yahoo.com