Wazazi wengi hutumia adhabu kama nyenzo muhimu ya malezi. Tunapozungumzia adhabu tunamaanisha chochote kinachomsababishia mtoto maumivu kama matokeo ya kosa alilofanya.
Unapomfinya mtoto, kwa mfano, unapomchapa, unapomtenga na kumkasirikia, unapompa kazi ngumu kumuumiza kama matokeo ya kosa lake, hapo unakuwa umemuadhibu.
Upande mwingine wa adhabu ni kumsababishia maumivu kwa kumnyang’anya kile unachojua anakifurahia.
Mfano, unapomzuia kuangalia televisheni, unapomzuia kutoka nyumbani, hapo unakuwa umemsababishia maumivu kwa kuondoa kile anachokipenda.
Umewahii kufikiri kiwango cha juu kabisa cha maumivu unachoweza kumsababishia mwanao kama adhabu? Unachora wapi mstari kutenganisha adhabu yenye manufaa na adhabu inayoweza kuleta madhara kwa mtoto?
Umewahi kujiuliza kwa nini tumezoa adhabu na hatufikiri kabisa mbadala wake? Kwa nini mtoto anapokosea, cha kwanza kinachokuja kwenye kichwa cha mzazi ni kumuadhibu?
Matumizi ya adhabu, kwa tafsiri yangu, ni utamaduni uliozoeleka katika jamii unaotufanya tuamini kuwa bila kumsababishia mtoto maumivu hawezi kusikia tunachotamani akisikie.
Utamaduni, kwa hakika, ni mkusanyiko wa maelekezo tunayoyarithi kutoka vizazi na vizazi kuonesha namna tunavyopaswa kutenda, wakati mwingine, bila kufikiri.
Mwanzoni mwa miaka ya 1960, Stanley Milgram wa Chuo Kikuu cha Yale alifanya utafiti maarufu kwa jina la “The Milgram Experiment.” Milgram alitaka kuangalia nini hasa kinachangia mtu kutii mamlaka hata katika mazingira ambayo utii huo unaweza kusababisha madhara kwa binadamu mwenzake.
Unaweza kujiuliza kwa nini nimeufikiria utafiti huu? Nakupa jibu. Utamaduni ni utaratibu unaoendesha maisha ya watu kwa namna inayofanana na maelekezo anayoweza kuyapewa mtu kutekeleza.
Adhabu, kwa kawaida, ni kiashiria cha utii wa maelekezo tuliyoyarithi tukiamini ndivyo tunavyopaswa kufanya.
Tunachoadhibu, wakati mwingine hatufikiri madhara yake. Tunatekeleza kile tunachoamini ni sahihi na hatufikiri mbadala wake.
Katika utafiti wa Stanley Milgram, washiriki waliaminishwa wanashiriki utafiti wa kuangalia uhusiano wa kumbukumbu na ujifunzaji na wao wanashiriki kama ‘walimu.’
Jukumu lao lilikuwa ni kusoma swali na kufanya uamuzi wa kumuadhibu mwanafunzi papo kwa hapo ikiwa jibu analotoa si sahihi. Wanafunzi hawa, kwa upande mwingine, walikuwa wandani wa mtafiti na walijua siri ya utafiti.
Adhabu waliyotakiwa kutoa hawa ‘walimu’ ni kubonyeza kitufe kinachoachia shoti ya umeme kwa mwanafunzi. Kadri kosa linavyofanyika, mwalimu alipewa maelekezo ya kuongeza kiwango cha shoti kutoka volt 15 mpaka 450 kulingana na idadi ya makosa yanayofanywa.
Ikumbukwe volt 450 ingeweza kutoa uhai wa mwanafunzi, ingawa katika mazingira halisi, hapakuwa na madhara yoyote kwa mwanafunzi.
Kilichokuwa muhimu hapa ni mamlaka ya mtafiti. Kwa hivyo, mtafiti aliwekewa mazingira ya ‘madaraka’, kwa kuvaa koti la maabara, akionekana kuwa msomi, na ndiye aliyekuwa anatoa amri kwa mshiriki.
Mwanafunzi, anayejua lengo la utafiti, alikaa chumba kingine na mara nyingi alitoa majibu yasiyo sahihi (ili aadhibiwe) na ikiwa mwalimu alibonyeza kitufe cha shoti, mwanafunzi alitoa sauti ya kuugulia maumivu makali akimsihi mwalimu kuacha kumuumiza.
Kama mwalimu alisita kuadhibu, mtafiti hakuonekana kujali na aliamuru zoezi liendelee. Kilichoangaliwa hapa ni utayari wa mwalimu kufuata maelezo na kuyatii bila kujali matokeo yake kwa binadamu mwenzake.
Washiriki wawili kati ya watatu (65%) ‘walitii sheria bila shurti’, wakitoa adhabu ya shoti hadi kufikia volti 450 ambayo walijua ingeweza kumuua mwanafunzi.
Ingawa wakati mwingine walifanya hivyo kwa masikitiko makubwa, uwepo wa jamaa mwenye madaraka pale uliwafanya wakawa hawana namna nyingine zaidi ya kutii na kutekeleza amri wanayojua inaweza kuleta madhara kwa binadamu mwenzao.
Stanley Milgram aligundua utii wa mwalimu uliongezeka zaidi mamlaka ya mtoa amri yalipoongezwa (namna alivyojitambulisha na kuvalia) lakini pia ukaribu uliokuwepo kati yake na mwanafunzi (mfano mwalimu kuona mateso anayoyapata mwanafunzi wake badala ya kusikia sauti pekee).
Milgram alitafsiri matokeo hayo kwa jicho la hatari ya madaraka katika kugeuza tabia za watu na kuwaingiza kwenye migogoro mikubwa ya kimaadili.
Unapomuweka mtu wa kawaida kabisa kwenye mazingira yenye kumpa mamlaka, kwa mfano, unakuwa umempa shinikizo la kuhalalisha mamlaka iliyo juu yake badala kuheshimu dhamira, miiko binafsi na misingi inayoheshimu utu wa mwingine.
Hii ina maana kwamba kuna mazingira yanaweza kuchochea tabia ya ukatili kwa mtu na kumsukuma kufanya kitendo cha kikatili usiofikirika.
Mazingira haya, kwa kiasi kubwa, yana uhusiano mkubwa na kuhalalisha mamlaka na madaraka ya watu fulani fulani na uwezo wao wa kusema kitu na kikatekelezeka.
Kwa mara nyingine, Milgram anatuonesha madhara yanayotokana na madaraka hasa yanapotumiwa kutoa amri zisizoongozwa na misingi ya utu wala maadili.
Katika mazingira haya ya kulinda mamlaka, mtu mwema ayekuzwa katika mazingira ya utu, anaweza kabisa kutumika na kugeuka kuwa mtu katili asiye na chembe ya utu na akajitetea kuwa hakuwa na uchaguzi mwingine zaidi ya kutekeleza alichoamrishwa kutekeleza.
Ingawa utafiti huu ulishambuliwa vikali kwa kuwadanganya washiriki, kutweza hisia zao na kuwafanya wajione ni watu katili, bado tunaweza kuutumia kuelewa uhusiano baina ya wenye mamlaka na wasio na mamlaka. Unaweza kuelewa, kwa mfano, hatari ya kuwa na mtu mbabe kwenye mifumo ya dini, siasa, ajira na kwingineko kwenye mamlaka.
Hata hivyo, ni vigumu kutumia utafiti huu kuhalalisha ushiriki wa watu ‘wema’ kwenye maovu yanayofanywa kitaasisi. Je, ni kweli amri inatosha kukusukuma kumuumiza binadamu mwenzako?
Je, unaweza kusema nilidhihaki maumivu ya binadamu mwenzangu kwa sababu tu nilijua wakubwa zangu wanaamini katika mabavu, ubabe na ukatili?
Wakati upi dhamiri ya mtu inaweza kumchochea kupingana na amri batili anazojua zinakwenda kinyume na misingi anayoiamini? Milgram hana majibu na anakosolewa vikali.
Mshunuzi Ginna Perry, kwa mfano, anafikiri wingi wa watu waliotii amri hiyo ya kikatili (wawili kati ya watatu) huenda ulitokana na ukweli kuwa walishtukia zile shoti za Milgram hazikuwa za kweli na ndio maana hawakuona shida kubonyeza mpaka kitufe cha mwisho kumaanisha walijua hakuna mtu anayekufa pale. Hata hivyo, bado marudio mengine mengi ya utafiti kama huo yanaonesha kuwa kiwango cha utii kilikuwa kikubwa ingawa asilimia zinatofautiana.
Katika malezi, utafiti huu unatusaidia kuelewa kwa nini wakati mwingine wazazi hufanya uamuzi unaowaumiza watoto bila kufikiri? Kwa nini tunawaza adhabu muda wote? Hatari moja wapo ya adhabu ni kutokuwepo kwa mipaka.
Unapomuadhibu mtoto kwa sababu tu unaamini huo ni utamaduni uliokulea na wewe, unakuwa huna tofauti na ‘walimu’ wa Stanley Mlgram waliobonyeza kitufe kumuadhibu ‘mwanafunzi’ bila kuikiri madhara yake. Tatizo la adhabu, kama tulivyoona, ni hatari ya kutengeneza tabia ya ukatili kwa watoto.