Dar es Salaam. Kampuni ya huduma za usafiri wa anga nchini Tanzania, Swissport Tanzania PLC, imetangaza kupata faida kabla ya kodi ya Sh8.6 bilioni kwa mwaka wa fedha uliomalizika Desemba 31, 2024.
Hayo yamebainishwa na Kaimu Ofisa Mtendaji Muu wa Swissport Tanzania PLC, Shamba Mlanga katika Mkutano Mkuu wa 40 wa mwaka wa wanahisa uliofanyika jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki.
Mlanga amesema utendaji wa kifedha wa kampuni hiyo umeendelea kukua mwaka hadi mwaka na kuwawezesha kutoa gawio la Sh2.5 bilioni kwa wanahisa.
Amesema mapato ya kampuni yaliongezeka kwa asilimia 26 hadi Sh51 bilioni kutoka Sh40.5 bilioni yaliyorekodiwa mwaka 2023.
Mlanga amesema gharama za uendeshaji kwa jumla ziliongezeka kwa asilimia 22 na kufikia Sh42.1 bilioni kutoka Sh35.1 bilioni mwaka 2023.
“Tuliweza kupata faida kabla ya kodi ya Sh8.6 bilioni ukilinganisha na Sh5.5 bilioni mwaka 2023, ikiwa ni ongezeko la asilimia 47,” amesema Mlanga.
Amesema ukuaji wa Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL), ongezeko la idadi ya abiria, matumizi ya vyumba vya mapumziko (lounges), kuongezeka kwa shehena ya mizigo inayosafirishwa nje ya nchi, mazingira mazuri ya biashara, pamoja na ukuaji wa sekta ya utalii na usafiri wa anga, vimechangia mafanikio hayo.
Amesema chanzo kikuu cha ongezeko la mapato ya kampuni kilikuwa Twiga Lounge inayomilikiwa na Aspire katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA).
Ofisa Mkuu wa Fedha wa Swissport Tanzania PLC, Joshua Jonas amesema mapato kutoka Twiga Lounge yaliongezeka kwa asilimia 34, yakifikia Sh1.994 bilioni ikilinganishwa na Sh1.488 bilioni mwaka 2023. Swissport inaendesha jumba hilo kwa ushirikiano na ATCL.
“Ongezeko la gharama za uendeshaji liliendana na ukuaji wa mapato na lilichangiwa na kupanda kwa bei za bidhaa na gharama za ajira.
“Ili kupunguza athari za ongezeko hilo, kampuni ilitekeleza mikakati kadhaa ya kupunguza gharama kwa lengo la kuongeza faida,” amesema Jonas.
Huduma kwa wateja zilitolewa kulingana na viwango vilivyobainishwa katika Mikataba ya Kiwango cha Huduma (SLA).
Jonas amesema changamoto zozote za kutokufuata SLA zilitatuliwa kupitia majadiliano na wateja na kuchukuliwa hatua stahiki. Mbinu hiyo iliimarisha ubora wa huduma na uhusiano wa kampuni na wateja wake.
Pia, amesema hakukuwa na tukio kubwa la kiusalama au uharibifu wa ndege au majeraha ya kupoteza muda wa kazi, jambo linaloashiria utamaduni thabiti wa usalama.