Dar es Salaam. Wanafunzi wa vyuo vikuu vya Tanzania na wakufunzi wameibuka washindi katika Shindano la Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) linaloendeshwa na kampuni ya teknolojia nchini China, Huawei.
Fainali hizo za kimataifa kwa mwaka 2024/25 zilifanyika mjini Shenzhen, China huku wanafunzi kutoka Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT), Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom) walitwaa tuzo ya juu na Tuzo ya mshindi wa pili.
Washindi wa tuzo ya juu ni Vida Mapunda (DIT), Joseph Msuya (UDSM) na Sigfrid Michael (Udom).
Washindi wengine ni Paul Nkingwa, Godlove Hipolite na Felix Kuluchumila wote kutoka Udom.
Shindano hilo la Huawei pia liliwatambua wakufunzi bora akiwamo Jumanne Ally kutoka DIT na Dk Alex Mongi kutoka Udom akishika nafasi ya pili katika kitengo cha mfukunzi bora.
Katika shindano hilo, linaloandaliwa kila mwaka na Huawei Technologies, linalenga kuwapa wanafunzi ujuzi wa kufanya kazi katika mifumo ya kompyuta ikihusisha eneo la cloud computing big data na akili AI.
Kwa mwaka huu wanafunzi na wakufunzi zaidi ya 200,000 walishiriki kutoka duniani kote.
Lengo la kukutanisha vipaji hivyo ni kutoa majawabu ya kiubunifu ili kutatua changamoto za ulimwengu hasa katika sekta kama vile kilimo, huduma za afya na elimu.
Akizungumza katika fainali za tuzo hizo mwishoni mwa wiki, Mkurugenzi wa Mkakati wa Tehama na Maendeleo ya Biashara wa Huawei, Ritchie Peng amesema shindano hilo linaunga mkono maono mapana ya kampuni hiyo ya kuwa na dunia inayotumia AI ifikapo mwaka 2030 kwa kuhamasisha ujumuishwaji wa kidijitali katika kufkia maendeleo endelevu.
“Tumeendelea kuendeleza muundo wa shindano ili kuendana na malengo ya uvumbuzi wa kimataifa,” amesema Peng.
Akizungumzia ushindi wake, mwanafunzi Vida Mapunda kutoka DIT amesema tuzo hizo zinawapa motisha ya kuendelea kufanya kazi kwa bidii na kudhihirisha kuwa vipaji vya Watanzania vinaweza kushindana kimataifa.
Mkuu wa Chuo cha Teknolojia kutoka ndaki ya Habari na Mawasiliano (CoICT) ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Baraka Maiseli amepongeza uwekezaji wa Serikali katika miundombinu ya Tehama.
“Vyuo Vikuu vyetu sasa vimejipanga vyema kutoa mafunzo kwa vitendo na msingi huo umewezesha mafanikio haya,” amesema Profesa Maiseli.
Mwakilishi wa Udom, Dk Florence Rashidi amepongeza jitihada zinazofanywa na Huawei katika kusaidia sekta ya elimu kwa kuwawezesha wanafunzi kutoka vyuo vikuu mbalimbali vya Tanzania kushiriki katika mafunzo ya vitendo na mashindano ya kimataifa.
Huu ni mwaka wa pili mfululizo kwa wanafunzi wa Kitanzania kufanya vyema katika shindano la Tehama la Huawei.
Mwaka 2023/24, wanafunzi watatu kutoka nchini pia walitambuliwa kwa ufaulu wao bora.
Washiriki katika hafla ya mwaka huu walitoka zaidi ya nchi kumi na mbili, zikiwemo China, Brazil, Algeria, Morocco, Nigeria, Ufilipino, Singapore na Serbia huku Tanzania ikiibuka washindi wa kwanza katika eneo la mafunzo kwa vitendo, ubunifu na Programming.