Vyombo vya habari vyahimizwa kuzingatia usawa wa kijinsia

Dar es Salaam. Vyombo vya habari nchini Tanzania vimetakiwa kuzingatia usawa wa kijinsia kuanzia uratibu wa ndani ya vyombo hivyo hadi uripotiji wa habari zake.

Imeelezwa usawa unaanzia kwa wafanyakazi, habari zisizogandamiza jinsia sambamba na kusimamia vyema sera za jinsia za vyombo hivyo.

Wito huo umetolewa na Profesa Nancy Booker, Dean wa Shule ya wahitimu wa vyombo vya Habari na Mawasiliano, Chuo Kikuu cha Aga Khan Kenya, wakati akitoa mafunzo kwa waandishi wa habari kuhusu  usawa wa kijinsia katika siku tatu za mafunzo kwa kundi hilo yaliyoanza wiki iliyopita jijini Dar es Salaam.

Katika hilo vyombo vya habari, vimeshauriwa kuzingatia usawa wa kijinsia kwenye uhabarishaji na uelimishaji wa jamii, kuchochea maendeleo ndani ya jamii na kuepuka athari zilizopo ikiwemo ukatili na unyanyasaji wa kijinsia.

“Usawa unaanzia katika uandishi wa habari, picha, wahusika wanawake na wanaume lazima wahusishwe kwa pamoja na si jinsia moja pekee ipendelewe,” amesema.

Amesema usawa wa kijinsia ni haki ya kibinadamu na ulimwengu unaotaka kuendelea haupaswi kuacha jinsia moja nyuma kwani hali hiyo italeta ugumu kimaendeleo.

Katika kutekeleza hilo amesema si kazi inayopaswa kufanywa pekee na vyombo vya habari bali ushirikiano unahitajika kutekeleza usawa wa kijisnia kwenya jamii.

“Waandishi mnapaswa kutambua watu wote ni sawa. Hivyo muwe mabingwa wa kuripoti habari zinazozingatia usawa wa kijinsia,” amesema Profesa huyo.

Mkufunzi Pauline Muriuki kutoka Chuo Kikuu Cha Agha Khan, amesema usawa wa kijinsia katika jamii ni muhimu, kwani unasaidia kuchochea maendeleo kati ya wanawake na wanaume hususani kiuchumi, siasa na kijamii.

“Usawa wa kijinsia ukiwepo unawezesha wanawake na wanaume ndani ya familia kushirikiana katika kujenga uchumi, familia bora hasa katika malezi bora,” amesema.

Ili kufanikisha hayo waandishi wa habari wananafasi kubwa kuelimisha jamii juu ya masuala ya kijinsia ikiwemo uongozi, jamii na kiuchumi.

“Hata katika elimu usawa wa kijinsia ni muhimu kwani inasaidia kuongeza idadi ya wasomi wakike na kiume na kuwezesha serikali kuwahudumia kwa wakati sawa na idadi yao.”

Waandishi wanapaswa kuelimisha jamii kuzingatia usawa huo kuchochea maendeleo zaidi na kuwezesha jamii yote kupata haki sawa.

“Kwa sasa kwenye jamii bado kuna changamoto za ukatili wa kijinsia, hususan kwa wanawake katika masuala ya uongozi na mila kandamizi za Utamaduni kama ukeketaji. Hayo yote yakiwemo katika jamii inasababisha upungufu kimaendeleo,” amesema.

Kwa upande wake, Mkufunzi Theresia Method, amesema vyombo vya habari kuzingatia usawa wa kijinsia katika matangazo kuepuka udhalilishaji wa jinsia yeyote.

“Kuna matangazo ambayo yapo kinyume na maadili ya jamii ambayo yanaonyeshwa kukandamiza jinsia moja jambo ambalo huleta athari, hivyo ni muhimu vyombo vya habari vikawa sababu ya mabadiliko,” amesema.

Naye, mkufunzi Kisali Simba amesema jukumu kubwa linabakia kwa waandishi kubadilisha fikra ya jamii inayoamini mwanamke hawezi. Kupitia kampeni na uanzishwaji wa jitihada za elimu jamii itabadilika.

Simba amesema waandishi wanapaswa kutumia kalamu zao kukemea ukandamizaji wa mwanamke uliopo kuanzia kwenye fikra ya baadhi ya wanajamii.

“Waandishi wanapaswa kuwapa nafasi sawa wanawake kama vile wanavyo toa fursa hiyo kwa wanaume na kuwaandika vizuri, kwani hilo litawajenga wanawake zaidi na kuwapa nguvu.”

Mmoja ya washiriki wa mafunzo hayo Aisha Hassan, amesema: “Nimehudhuria mafunzo haya na nimejifunza mwanamke anaweza Kufanya jambo linalofanywa na mwanaume hasa katika vyombo vya habari, hivyo basi nawaasa watu wenye dhana na fikra potofu ya kuwa mwanamke hawezi wabadilishe mitazamo yao.”

Related Posts