Unguja. Jeshi la Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi linawashikilia watu wanane kwa tuhuma za kujihusisha na matukio ya unyang’anyi, kati ya hao watatu walijihusisha na tukio la hivi karibuni lililosambaa katika picha mjongeo mitandaoni.
Picha hiyo ilionyesha mtu mmoja akivamiwa na kundi la watu waliovaa mavazi meusi ya mabaibui, wakiwa na silaha za mapanga na kuficha sura zao.
Walimshambulia Nassoro Suleiman Nassoro (33) kutoka Kisauni kwa kumpiga panga kisogoni, jambo lililomsababishia maumivu makali.
Akitoa taarifa kwa waandishi wa habari leo Jumapili Juni 1, 2025, Kamanda wa Polisi Mkoa huo, Richard Mchomvu, amesema kuwa baada ya kupokea taarifa ya tukio hilo walianza uchunguzi ili kubaini wahusika.
Kwa mujibu wa Kamanda Mchomvu, msako uliofanywa uliwezesha kukamatwa kwa watuhumiwa wanane, kati yao watatu wakiwa ni wahusika wa moja kwa moja katika tukio hilo.
“Watuhumiwa hao watatu ni Mohammed Jaha Khamis (17), Fahad Ali Mselem (16) na Ali Suleiman Rashid (22) wote wakazi wa Kisauni,” amesema Kamanda Mchomvu.
Pia, amesema kuwa Mei 19, 2025 saa 02:00 usiku katika barabara ya Masingini-Kijichi, Wilaya ya Magharibi A, Mkoa wa Mjini Magharibi, Unguja, kulitokea tukio lingine la unyang’anyi ambapo watuhumiwa wawili walimshambulia kwa mapanga Ahmed Othman Issa (30) na kumnyang’anya pikipiki.
Amesema pikipiki hiyo yenye thamani ya Sh3 milioni ilikamatwa baada ya Jeshi la Polisi kupokea taarifa za tukio hilo na kufanya operesheni iliyofanikisha kuwakamata watuhumiwa wakiwa na pikipiki hiyo.
Watuhumiwa waliokamatwa ni pamoja na Ali Khamis Ali (20), mkazi wa Daraja Bovu, na Abdallah Ame Hassan (22), mkazi wa Mtoni Kidatu.
Kwa mujibu wa Kamanda Mchomvu, upelelezi wa shauri hilo unaendelea, na utakapokamilika watafikishwa mahakamani.
Amesema Jeshi la Polisi linaendelea na ufuatiliaji ili kubaini na kuwakamata watuhumiwa wengine walioshiriki katika tukio hilo.
Hata hivyo, Jeshi la Polisi limewaomba wananchi kuendelea kushirikiana na vyombo vya usalama katika kufichua vitendo vya kihalifu na wahalifu, ili kuhakikisha usalama wa Taifa unadumishwa dhidi ya vitendo vinavyokiuka sheria.