Dar es Salaam. Waswahili wana usemi usemao, damu nzito kuliko maji, ndivyo unavyoweza kuamini namna damu ya Edward Massawe ilivyohangaika hadi viungo vya mwili wake vilivyokuja kugundulika baada ya kuziba kwa mfumo wa maji taka.
Kugundulika huko kulitokea takriban siku 190 tangu kutoweka kwake huko eneo la Kimbiji Wilaya ya Kigamboni Jijini Dar es Salaam, baada ya mpangaji wa nyumba hiyo kuripoti kwa mwenye nyumba juu ya kuziba kwa mfumo huo.
Pengine ni kutokana na uzito huo huo wa damu, Greyson Ulomi aliyekuwa akiishi katika nyumba hiyo, alifanya kosa la kiufundi alipohama katika nyumba hiyo kimyakimya bila kumjulisha mwenye nyumba, Nickson Kweka ambaye ni shemeji yake.
Hii ilimfanya awe mshukiwa wa kwanza katika mauaji ya Edward, ambapo polisi wakitumia mbinu za kikachero za kufuatilia mitandao ya simu, walibaini yupo Morogoro ambapo alifuatiliwa na kisha kukamatwa na kurejeshwa Kigamboni.
Ni kutokana na ushahidi mzito uliotolewa na mashahidi na maelezo ya kukiri kosa aliyoyatoa Polisi, Jaji Elizabeth Mkwizu wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, amemuhukumu Ulomi na mshirika wake, Andrea Blezi, adhabu ya kifo.
Simulizi ya namna marehemu alivyotoweka ilielezwa na shahidi wa tatu, Nickson Kweka, ambaye alieleza kuwa alitoka Mkoa wa Kilimanjaro na kuhamia Dar es Salaam mwaka 2008 ambako aliishi kwa ndugu wakati akiendelelea kutafuta kazi.
Kulingana na ushahidi wake, mwaka 2020 alihama kwa ndugu yake na kwenda kupanga na kuishi na mkewe, Lightness Ulomi ambapo mwaka 2021 alihamia katika nyumba yake iliyopo Kijaka Kigamboni katika kata ya Kibiti Jijini Dar.
Baada ya kuishi hapo kwa miezi minane, alihamia katika nyumba yake huko Mikocheni kutokana na kazi aliyokuwa akiifanya, na walipohama mkewe alimwacha mdogo wake Greyson Ulomi aendelee kuishi katika nyumba hiyo.
Aprili 2023, Edward Massawe (sasa marehemu), ambaye ni ndugu na shahidi huyo alifika Dar es Salaam kutokea Moshi akitafuta kazi ambapo alimfungulia Edward duka na akaamua kumnunulia Greyson mashine ya kuchomea vyuma.
Edward na Greyson waliishi pamoja katika nyumba ya Kweka lakini Mei 18,2023, Kweka alijaribu kumtafuta Edward kwa simu mara kadhaa akawa hampati, akampigia Greyson kumuulizia lakini akajibu kuwa hakuwa pamoja na Edward.
Siku hiyohiyo usiku saa 5:30, Kweka akisindikizwa na rafiki yake aitwaye Hemed Swai walifika katika nyumba hiyo na kukuta taa zinawaka lakini hakuna mtu ndani.
Walijaribu kuwaamsha majirani na kuvunja mlango na kuingia ambapo walikuta tu suruali ya Edward na viatu vya Greyson, ambapo Kweka aliamua kuangalia chumba cha mke wake kama kuna mashine ya kuchomea na akakuta hakuna kitu chochote.
Siku iliyofuata, Kweka akapata barua kutoka kwa uongozi wa mtaa na kutoa taarifa kituo cha Polisi Kimbiji kwamba Edward na Greyson wamepotea na kueleza kuwa mara ya mwisho kuzungumza na Edward kwa simu ilikuwa Mei 15,2023.
Viungo vya binadamu vinapatikana
Shahidi huyo anaendelea kueleza kuwa Novemba 20,2023 zikiwa zimepita siku 190 tangu atoe taarifa ya kutoweka kwa Edward na Nickson, Kweka alipokea simu kutoka kwa mpangaji wake, Sofia (shahidi wa 7) akimjulisha kuziba kwa choo.
Kweka akampigia simu fundi bomba, Fundi Pengo (shahidi wa 9) ambaye alifika kwenye nyumba kujaribu kuzibua mfumo huo wa majitaka bila mafanikio.
Katika jitihada hizo, fundi aliamua kuvunja zege katika shimo la kukusanyia majitaka, ambapo alikutana na shuka lililokuwa na madoa kama ya damu na nguo nyeusi iliyokuwa na mfupa wa mguu wa binadamu na fulana nyeusi.
Kutokana na kugundulika kwa vitu hivyo, Kweka aliagiza uzibuaji huo usimame ambapo alitoa taarifa kwa uongozi wa mtaa ambao waliwajulisha polisi ambao walifika na kutoa viungo vya binadamu katika shimo hilo la choo.
Novemba 24,2023 baada ya kupokea taarifa kuwa Greyson yuko Morogoro, walisafiri na Polisi hadi Morogoro na kumkamata na katika mahojiano alikiri kushiriki mauaji hayo na akamtaja mtu waliyeshirikiana naye kuwa ni Bleza.
Polisi walifanikiwa kumkamata Bleza na kuwarudisha hadi Kigamboni ambapo walihojiwa kikamilifu na kuandika maelezo yao. Ushahidi wake kuhusiana na eneo la tukio ulioana na ule wa mpangaji wake pamoja na fundi bomba aliyemtuma.
Mashahidi wengine walikuwa ni mtaalamu kutoka Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali aliyechunguza viungo vilivyopatikana na sampuli ya DNA kutoka kwa mama mzazi, daktari aliyefanya uchunguzi na Polisi waliopeleleza.
Katika utetezi wao, washitakiwa wote walikana kuhusika na mauaji hayo na kudai kuwa walikuwa hawajui kwa nini walikamatwa na Polisi na kuhusishwa na mauaji hayo, na kuiomba Mahakama iwaone hawana hatia na iwaachie huru.
Hukumu ya jaji ilivyokuwa
Jaji alisema ingawa hakuna shahidi hata mmoja wa Jamhuri aliyetoa ushahidi kuwa alishuhudia mauaji hayo, lakini ushahidi wa mazingira na maelezo yao wenyewe waliyoyatoa Polisi, yanathibitisha wauaji ni wao na hakuna mtu mwingine.
Katika hukumu yake aliyoitoa Mei 30, 2025 na kupakiwa katika mtandao wa Mahakama, Jaji Mkwizu alisema maelezo ya onyo ya washtakiwa, yanaeleza hatua hatua kuhusu mauaji yalivyotekelezwa na ushiriki wa kila mshtakiwa.
Jaji alisema katika maelezo yao, washtakiwa walikiri kushiriki mauaji hayo na kuficha mwili wa marehemu na mshtakiwa wa kwanza alisema alimuua kwa kumpiga kwa jiwe kichwani, majeraha yanayooana na ripoti ya uchunguzi wa daktari.
Kwa mujibu wa Jaji, mshtakiwa wa pili kwa upande wake, alieleza mwanzo mwisho namna alivyoshiriki mauaji hayo na kueleza kiini kikihusiana na fedha na alibainisha jinsi walivyomtupa kwenye shimo la choo baada ya kumuua.
“Ingawa washtakiwa wote wawili walipinga kupokelewa kwa maelezo hayo, mapingamizi yao kimsingi yalijikita kwenye taratibu na sio ukweli wa kimsingi wa maudhui yaliyomo kwenye maelezo yao hayo,”alieleza Jaji Mkwizu.
Mathalan, Jaji alisema mshtakiwa wa pili alijikita katika eneo la kuthibitisha maelezo, lakini hilo lilitolewa ufafanuzi na shahidi wa 12 aliyeandika kuwa mshtakiwa alikuwa na uelewa mdogo hivyo baada ya kuyaandika alimsomea.
Mbali na hilo, ushahidi wa Jamhuri unaonyesha maelezo yaliandikwa kati ya saa 12 na saa 1:00 jioni na yanajionyesha kwenye ushahidi wa shahidi wa 12 na yanaungwa mkono kwenye ukurasa wa kwanza wa kielelezo namba 7,”alisema.
“Ushahidi huu mzito haukupingwa wakati wote wa usikilizwaji wa kesi. Hakuna ushahidi wa utetezi ulitolewa katika hatua yoyote kupinga ushahidi huo au kuingiza ushahidi utakaotilia mashaka uchukuaji wa maelezo hayo”
“Zaidi ni kwamba hakuna mahali katika hatua yoyote ya usikilizwaji wa kesi hii ambapo washtakiwa walijiweka kando au kukana maudhui ya maelezo yao ya onyo,”alieleza Jaji Mkwizu katika hukumu yake na kuongeza kusema kuwa:-
“Kukosekana kwa jitihada za kupinga ukweli na usahihi wa maelezo hayo yanatoa taswira kuwa ni maungamo ya kweli. Hii inafanya maelezo yao yaaminike na kujenga msingi wa ushiriki wao katika mauaji hayo”
Jaji alisema, mathalan nguo zilizopatikana katika shimo hilo hususan fulana na kaptula ambazo zilitambuliwa na shahidi wa tisa kama nguo ambazo alizivaa marehemu alipomuona mara ya mwisho, inathibitishwa mwili ulitupwa makusudi.
Kulingana na Jaji, mara zote mahakama imeweka msimamo kuwa hatia ya mshtakiwa inaweza kupatikana kutokana na muunganiko wa shahidi mbalimbali kama ilivyo katika kesi hiyo, ambapo hakuna shahidi aliyeshuhudia mauaji.
“Ingawa upande wa utetezi unadai ushahidi ulikuwa ni wa mazingira, unakosa ushahidi wa moja kwa moja wa aliyeshuhudia mauaji, lakini ushahidi huu unahusisha maelezo yao, ripoti ya DNA na uchunguzi wa Polisi,”alisema Jaji.
Muunganiko huo unaohusisha ushahidi wa mashahidi wengine, unashawishi kuwa si kweli washtakiwa hawana hatia bali unathibitisha ushahidi wa Jamhuri usioacha mashaka kuwa walishiriki kila mmoja kumuua Edward.
Jaji alisema kwa sheria za Tanzania, mtu anayepatikana na hatia ya kuua kwa kukusudia, anakabiliwa na adhabu moja tu kulingana na kifungu cha 197 cha Kanuni ya Adhabu kama ilivyorejewa mwaka 2022, nayo ni adhabu ya kifo.