Mkongwe wa siasa, rafiki wa Nyerere afariki dunia akiwa na umri wa miaka 100

Dar es Salaam. Mwanasiasa mkongwe na shujaa wa harakati za uhuru wa Tanganyika, Alhaj Mustafa Mohamed Songambele, amefariki dunia siku chache baada ya kutimiza umri wa miaka 100, akiwa ameacha historia ya kipekee, ikiwemo kumbukumbu ya kumchekesha Mwalimu Nyerere hadi kudondoka sakafuni kwa kicheko.

Alhaj Songambele, amefariki dunia usiku wa kuamkia leo Juni Mosi, 2025 jijini Dar es Salaam.

Taarifa ya kifo chake imethibitishwa na binti yake Dorah Songambele, ambaye amesema maandalizi ya kuusafirisha mwili wa marehemu kwenda Songea kwa maziko yanaendelea, huku msiba ukiwa nyumbani kwake Mwananyamala.

Jumapili, Mei 25, 2025, Alhaj Mustafa Mohamed Songambele alitimiza umri wa miaka 100, ambapo familia yake iliandaa sherehe ya Maulid nyumbani kwake, Mwananyamala, jijini Dar es Salaam, kama ishara ya kumshukuru Mungu kwa neema ya maisha marefu.

Sherehe hiyo ya Maulid ilifanyika wiki chache baada ya kurejea nyumbani kutoka hospitalini alipokuwa amelazwa.

Aprili 2, 2025, Alhaj Songambele alitembelewa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Simbachawene, aliyekwenda kumjulia hali katika Hospitali ya Aga Khan.

Katika historia ya siasa za Tanzania, jina la Alhaj Songambele haliwezi kufutika.

Aprili 2, 2025 Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Simbachawene, alifanya ziara ya kumjulia hali mwanasiasa mkongwe Alhaji Mustafa Songambele aliyelazwa Hospitali ya Aga Khan kwa matibabu.

Alikuwa miongoni mwa waanzilishi wa chama cha TANU, ambacho kiliongoza harakati za kudai uhuru wa Tanganyika. Alikuwa mmoja wa wanachama wa kwanza 30 wa chama hicho, na alipokea kadi ya uanachama namba 27.

Alhaj Songambele aliweka rekodi ya kuwa Mkuu wa Wilaya wa kwanza nchini Tanganyika baada ya uhuru, ambapo aliteuliwa kuongoza Wilaya ya Pwani, eneo ambalo kwa sasa ni sehemu ya Wilaya ya Ilala, jijini Dar es Salaam.

Safari yake ya uongozi haikuishia hapo. Kutokana na uaminifu, weledi na uzalendo wake wa dhati, Mwalimu Nyerere alimteua kuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, nafasi aliyoitumikia kwa uadilifu mkubwa.

Songambele hakuwa tu kiongozi wa kisiasa, bali pia alikuwa miongoni mwa watu wa karibu sana na Mwalimu Nyerere.

Alikuwa miongoni mwa watu waliouona na kuushiriki kwa vitendo mchakato wa ukombozi wa Tanganyika, akiwa bega kwa bega na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere.

Hakuwa tu kiongozi wa kisiasa, bali pia alikuwa rafiki wa karibu na mshauri wa Mwalimu, akihusishwa moja kwa moja na nyakati muhimu za historia ya Taifa.

New Content Item (1)
New Content Item (1)

Historia inamkumbuka kama mmoja wa wakazi wa Dar es Salaam waliompokea Mwalimu Nyerere kwa heshima kubwa baada ya kuacha kazi ya ualimu, hatua iliyomuwezesha kujitosa kikamilifu katika harakati za kudai uhuru wa Tanganyika.

Ni yeye aliyemsaidia Mwalimu kupata kiwanja cha kujenga nyumba katika eneo la Magomeni Mikumi, nyumba ambayo leo hii ni kumbukumbu hai ya maisha ya Baba wa Taifa, na imegeuzwa kuwa makumbusho rasmi yanayohifadhi historia ya harakati za ukombozi wa Taifa.

Kumchekesha Mwalimu Nyerere

Julai 8, 2013, Alhaj Songambele alipokuwa akizungumza na baadhi ya wafanyakazi wa Idara ya Itikadi na Uenezi katika Ofisi Ndogo ya Makao Makuu ya CCM, Lumumba, jijini Dar es Salaam, alisimulia kisa cha kihistoria kuhusu namna alivyomchekesha Mwalimu  Nyerere hadi akadondoka sakafuni kwa kicheko, hali iliyomfanya karibu akamatwe na walinzi wa Mwalimu kutokana na tafrani hiyo isiyotarajiwa.

Kwa mujibu wa Alhaj Songambele, wakati akitoa simulizi hiyo akiwa na umri wa miaka 88, alieleza kuwa mwaka 1970, alipokuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam na pia Katibu wa TANU wa mkoa huo, alienda nyumbani kwa Mwenyekiti wa Chama, Mwalimu Nyerere, kwa ajili ya mazungumzo maalumu.

Alisema kuwa, wakati wakiwa katika mazungumzo, alitamka maneno yaliyomchekesha sana Mwalimu Nyerere kiasi kwamba alidondoka sakafuni huku akibubujikwa na machozi kwa kicheko.

Mzee Songambele alieleza kuwa, baada ya Rais kuondoka kurejea ofisini kwake, maofisa usalama walimfuata na kuanza kumhoji wakisema: “Kwa nini umemchekesha Rais hadi kudondoka chini? Yaani, ulitaka Rais afe halafu sisi tupate shida ya kueleza kwamba alikufa kwa kicheko? Inabidi tukukamate na kukuweka ndani!”

Mei 25, 2025 ilifanyika Maulid kwa ajili ya shukranu baada ya Alhaji Songambele kutimiza umri wa miaka 100. Maulid ilifanyika nyumbani kwake Mwananyamala jijini Dar es salaam.

Alisema kuwa, baada ya walinzi kutoa kauli hiyo, alilazimika kujitetea kwa kusema: “Mimi nilizungumza tu, sikuwa najua kama Mwalimu atacheka sana kiasi kile. Sasa hili si kosa langu, naomba mnisamehe.

“Nilipoona wanatafakari, nikapanda ngazi hadi ofisini kwa Rais. Nilipomkuta, akasema: ‘Bwana, nimeshacheka sana, inatosha basi.’ Nikamjibu: ‘Mwalimu, mimi sikuja kukuchekesha tena, lakini hawa walinzi wako wanataka kuniweka ndani kwa sababu wewe umefurahi. Sasa nimekosea nini?’” alisimulia Mzee Songambele.

Alisema kuwa, baada ya Mwalimu Nyerere kusikia malalamiko hayo, aliwaita walinzi wake na kuwaagiza wamwache huru, hatua iliyomwokoa na kumruhusu kuondoka salama.

Katika mazungumzo hayo na wafanyakazi wa Idara ya Itikadi na Uenezi, Alhaj Songambele pia alitabiri kuwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kitaendelea kutawala kwa muda mrefu, licha ya kuwepo kwa vyama vingi vya siasa, akisisitiza kuwa nguvu hiyo inatokana na historia imara ya chama ambayo si rahisi kufutika.

Songambele alitoa wito kwa CCM kujiimarisha zaidi ili kuendeleza misingi thabiti ya chama hicho, kwa lengo la kuhakikisha hakiwezi kuyumba wala kuyumbishwa na vuguvugu lolote la upinzani.

Alisisitiza kuwa katika kujenga na kudumisha misingi hiyo, vijana wanayo nafasi kubwa na ya kipekee, hivyo wanapaswa kupewa nafasi na kuhamasishwa kushiriki kikamilifu katika harakati za kuendeleza chama.

Related Posts